http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119468/medRes/2346313/-/6ktn4c/-/kisarawe+pic.jpg

 

Kisarawe watenga bajeti ya taulo za kike

Na  Tumaini Msowoya, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  10:54

 

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo amesema katika kutekeleza mkakati wa wilaya hiyo wa ‘Tokomeza Zero’ na kuinua kiwango cha elimu, wamefanikiwa kutenga bajeti kwa ajili ya taulo za kike kwa wanafunzi.

Amesema kati ya mambo yanayotajwa kuchangia wanafunzi wengi wa kike kutohudhuria masomo kati ya siku tatu hadi nne kila mwezi ni ukosefu wa vifaa vya kujihifadhia wakati wa hedhi.

Akizungumza wakati wa mdahalo uliokuwa ukijadili usawa wa kijinsia unavyoweza kuchoche maendeleo ulioandaliwa na shirika la Plan International jijini hapa jana, Jokate alisema: “Utengaji wa bajeti kwa ajili ya taulo za kike utasaidia kuongeza ufaulu kwa wilaya yetu.”

Awali, Mkurugenzi Mkazi wa Plan International, Gwyneth Wong alisema ndoa za utotoni, mimba za utotoni na ukeketaji ni kati ya changamoto zinazokwamisha ndoto za wasichana wengi nchini na kutoa wito kwa jamii kuungana kutokomeza vitendo hivyo.