http://www.swahilihub.com/image/view/-/5026334/medRes/2281742/-/n3vhol/-/lipumba+pic.jpg

 

Lipumba awashukia Maalim Seif, Lowassa na Chadema

 

Na Kalunde Jamal na Bakari Kiango, mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Friday, March 15  2019 at  10:11

 

 Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba jana alitumia muda mwingi wa hotuba yake kuwashambulia katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Chadema.

“Seif hatutakii mema, tulimdekeza kwa muda mrefu akajiona yeye ni Sultani, analolitaka lazima apewe. Amewapotosha watu wengi. Hata wabunge wetu wa viti maalumu tunawaita katika vikao yeye anawazuia badala yake wanakwenda katika mkutano wa Chadema,” alisema katika hotuba hiyo ya shukurani kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa saba wa chama hicho waliomchagua tena katika nafasi hiyo.

Alisema upande wa Maalim Seif uliweka vizingiti vingi ili mkutano huo ambao pia uliohudhuriwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza usifanyike.

“Naishukuru kamati ya maandalizi kwa kufanikisha mkutano huu na wajumbe tupo hapa tukiwa na sare. Kwa hali iliyokuwa ngumu kufanikisha jambo hili haikuwa kazi rahisi. Zimefunguliwa kesi takribani 39 zenye lengo la kukisambaratisha chama. Leo hii mkutano huu ulitaka kuzuiliwa, lakini tunamshukuru kwa kiburi chake, badala ya kufungua kesi dhidi ya baraza kuu la uongozi la Taifa, yeye akafungua dhidi ya Lipumba, Magdalena Sakaya.”

Alisema Maalim Seif hakujua kama Lipumba hana uwezo wa kuitisha mkutano mkuu wa CUF, bali ni baraza kuu la taifa la chama hicho na kudokeza kwamba endapo angelishtaki baraza hilo, mkutano huo usingefanyika.

“Kutokana na kiburi chake, amekwenda mchomo kwa sababu amemshtaki mtu asiyestahili. Leo tunafanya mkutano wetu mkuu,” alisema.

Profesa Lipumba alisema CUF inafanya mkutano mkuu kikiwa kimepitia katika mgogoro aliodai kuwa umesababishwa na Maalim Seif kutokana na ubinafsi wake.

Mwelekeo mpya

Kuhusu mwenendo wa chama hicho, Profesa Lipumba alisema kitakuja na sera mpya -- Furaha Haki Sawa kwa Wote-- (Furaha) yenye lengo la kujenga msingi bora kwa Watanzania na kuwafanya wafurahi.

Aliwataka wajumbe hao kuendeleza moto na demokrasia katika maeneo mbalimbali na kuwa askari katika kuhakikisha CUF inazaliwa upya sanjari na kuisambaza vyema sera ya chama hicho ya haki sawa kwa wote.