Uchambuzi wa Leo: Afya ya masikio yetu ni muhimu, jitihada za kuiokoa jamii ziongezeke

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu 

Imepakiwa - Wednesday, March 6  2019 at  11:28

 

 Hivi karibuni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema wizara yake kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), watahakikisha wanadhibiti uingizwaji wa spika za masikio (head phone) ambazo hazina ubora kwa sababu ni chanzo kikubwa cha tatizo la upotevu wa usikivu.

Ummy alisema, “Nimeshuhudia watu wamekuwa kama matahira kwa kuweka spika za masikioni hasa vijana, hebu tupunguze kwa kiasi kikubwa matumizi hayo kwa sababu tusipokuwa makini tunaweza kuwa na wimbi kubwa la watu wenye matatizo ya upotevu wa kusikia nchini.”

Waziri huyo aliyasema hayo Machi 3 katika Siku ya Usikivu Duniani iliyofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Mloganzila jijini Dar es Salaam iliyokuwa na kaulimbiu isemayo “Chunguza usikivu wako”. Lengo la siku hii lilikuwa ni kuhamasisha kila mtu kuchunguza usikivu wake ili kujua uwezo wake wa kusikia upo kwa kiwango gani aweze kuchukua hatua stahiki ya kuendelea kujikinga au kutibiwa, iwapo utakuwa umetetereka.

Ukosefu wa usikivu ni hali ya kupoteza uwezo wa kusikia na miongoni mwa dalili kwa watoto na watu wazima ni kutoshtuka au kutazama kunapokuwa na sauti za watu, kelele ya mlango, mathalan na sauti zitokazo katika runinga.

Vilevile dalili nyingine inachangiwa na kushindwa kuongea, kupata ugumu wa katika kujifunza mambo mbalimbali ikiwamo kusoma na kujibu tofauti wakati mtu anapoongea na mtu mwingine.

Kwa mujibu wa watalaamu, inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia tano ya watu wote duniani ambayo ni sawa na watu milioni 466 wana ukosefu wa usikivu ambapo milioni 432 ni watu wazima na milioni 34 watoto. Inatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2050 zaidi ya watu milioni 900 watakuwa na kukosefu wa usikivu.

Katika Bara la Afrika kwenye nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara inakadiriwa kuwa kuna watu milioni 518, ambapo inakadiriwa kuwa watu milioni 1.2 ambao ni watoto wa kati ya umri wa miaka mitano hadi 14 wanakabiliwa na ukosefu wa usikivu.

Kwa hapa nchini, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wagonjwa waliohudumiwa kwenye idara ya masikio, pua na koo kati ya Novemba 2018 na Januari 2019 ni 5,959 kati yao 454 (sawa na asilimia nane) walikuwa na ukosefu wa usikivu.

Inashauriwa kwamba wagonjwa wanapaswa kuhudhuria kliniki ili kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ikiwamo ugonjwa wa kaswende na magonjwa mengine, kupata chanjo dhidi ya magonjwa ya surua na uti wa mgongo na kwa watoto wenye wazazi wenye historia ya matatizo ya kusikia na uziwi wapelekwe katika vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi.

Waziri Ummy anasema katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imeendelea kuchukua hatua ikiwamo tiba kwa kutumia mashine za kukuza mawimbi ya sauti, upasuaji wa kuziba tundu la ngoma ya sikio pamoja na kupandikiza vifaa vya kusaidia kusikia.

Katika kipindi cha mwaka 2018 takriban wagonjwa 117 walipatiwa vifaa vya kukuza mawimbi ya sauti na 43 walifanyiwa upasuaji wa kuziba tundu la ngoma ya sikio. Pia kuanzia Juni 2017 hadi Desemba 2018 watoto 21 wameweza kupandikizwa vifaa vya kuwasaidia kusikia. Kwa Hospitali ya KCMC iliyopo mjini Moshi kwa kipindi cha 2018 iliweza kuwaona wagonjwa 300 wenye matatizo ya kusikia na kati yao wagonjwa 20 walipewa vifaa vya kukuza mawimbi ilhali 45 walifanyiwa upasuaji ili kuziba tundu la ngoma ya sikio.

Binafsi naamini kwamba watendaji wa Wizara ya Afya watahakikisha kunakuwapo na takwimu za kitaifa za upotevu wa usikivu na zitengwe za watoto na watu wazima ili zisaidie katika uhamasishaji kwa jamii ili kujikinga na ugonjwa huo. Hata hivyo, kwa upande mwingine wamiliki wa kumbi za starehe nchini nao wanao wajibu wa kuhakikisha wanaweka vifaa vya kudhibiti sauti katika kumbi zao kwa sababu kelele kupita kiasi zinasababisha mtu apate tatizo la upotevu wa usikivu.

Pia watendaji wa halmashauri na kila kiongozi wawajibike kuchukua hatua kwa mmiliki yeyote wa ukumbi wa starehe ambaye ukumbi wake utakuwa na kelele kupita kiasi, wambane kisheria kupitia sheria ndogo ambazo zinapaswa kutungwa na kila halmashauri.

Ni vyema pia watumiaji wa spika za masikioni wakahakikisha kuwa wanapunguza matumizi yake ili kujihakikishia afya ya masiko yao.