JAMVI: Msimu wa kuumbuana na kubobojoka ndio huu

William Ruto

Naibu Rais William Ruto kwenye kampeni ya kuhamasisha wenyeji wa Webuye, kaunti ya Bungoma kujisajili kuwa wapiga kura Januari 23, 2017. Picha/JARED NYATAYA 

Na WANDERI KAMAU

Imepakiwa - Sunday, July 9  2017 at  14:52

Kwa Mukhtasari

HUKU kampeni za uchaguzi zikiingia kipindi cha lala salama, 'Jamvi laSiasa’ limezamia tathmini baadhi ya semi ambazo zimekuwa zikitumika na wanasiasa kupapurana na kukashifiana kwa lengo la kuwavutia wapiga kura kwenye majukwaa tofauti ya kisiasa.

 

Rais Uhuru Kenyatta:

Ni mgombea urais wa Chama cha Jubilee (JP). Mpinzani wake mkuu ni Raila Odinga, ambaye anasaka kiti hicho kupitia muungano wa Upinzani, NASA. Baadhi ya kauli zake ni: “Msimchague huyo Msichague mtu wa vitendawili (Odinga). Kazi yake ni kuwachezesha mpira ambao haujulikani utaishia wapi. Bw Odinga hupenda kutumia mafumbo ya vitendawili katika kampeni zake.

Akimtaja Odinga kama kiongozi asiye na ajenda ya maendeleo, Bw Kenyatta alisema: “Amehudumu serikalini kwa karibu miaka 30, wakati Naibu Rais (William Ruto) alikuwa angali katika Kidato cha Kwanza. Sasa anasema kwamba atawaletea Wakenya mabadiliko. Ni mabadiliko yapi hayo ataleta baada ya miaka 30 ambayo hakufanya?”

Alijipiga kifua kuhusu ushindi wake wa 2013.

“Tuliwashinda licha ya kuwa msituni (ICC). Wengine (Raila na Kalonzo) walikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mtawalia. Lakini tuliwashinda licha ya kuwa nje ya serikali. Ni mara hii wanadhani watatushinda? Aaaai…tuambiane ukweli. Hawawezi tukiwa serikalini. Tutawashinda saa mbili asubuhi.”

Naibu Rais William Ruto

Akimsuta Odinga kuhusiana na ahadi yake ya kuwapeleka Wakenya “Kanani” kama “Joshua.”

“Juzi alisema atahalalisha pombe ya Chang’aa na Busaa. Katika Biblia, Kanani tunayofunzwa ni ile ya nyama na maziwa. Lakini hii Kanani yake ni bandia kwani inaonekana kuwa ya Busaa na Chang’aa. Huyu ni Joshua Bandia. Wakenya wanapaswa kuepukana na hadaa zake. Mnataka kazi ianze ama kitendawili kiendelee?”

Akimkejeli Bw Odinga kuhusu umri wake:

“Wajua Rais Kenyatta ni muungwana. Tumehakikisha tutatenga fedha za kutosha ili kuona kuwa yule mzee wa kitendawili (Odinga) ametengewa pensheni ya kutosha ili asiteseke atakapostaafu kwani ni dhahiri tutamshinda kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura.”

Akimkabili Kalonzo  kwa madai ya kupotoshwa na Odinga kisiasa kuwa mgombea-mwenza wake.

“Nimeshangazwa sana na ndugu yangu Kalonzo kukubali kupotoshwa na huyo mzee wa hadithi nyingi (Odinga) kiasi kwamba anakaa kitako barabarani…Kalonzo aliyekuwa Makamu wa Rais wakati wa Serikali ya Muuungano ya Kibaki. Namhurumia sana. Namwomba ajiunge nasi (Jubilee) ili angaa apate upenyu wa kisiasa.”

Mbunge Moses Kuria akimsuta Odinga kwa ziara yake katiika Kaunti ya Kiambu.

“Ni vizuri sana kwa Raila Odinga 'kufurahisha nafsi yake’ kwa kuzuru Kiambu. Ninachojua ni kwamba hakuna kura hata moja aliyopata. Msisimko alioshuhudia ni wa watu waliomhurumia kwani hawawezi kushawishika.”

Raila Odinga (Mgombea urais wa muungano wa NASA)

Akijitetea dhidi ya madai ya kuwa 'adui’ ya jamii ya Agikuyu:

“Mmeambiwa na viongozi wenu kwamba mimi ni adui yenu na mwendawazimu (Muguruki). Hata hivyo, nilimuunga mkono kikamilifu Rais Mstaafu Mwai Kibaki mnamo 2002, kwa kauli ya 'Kibaki Tosha.’ Wakati huo mliniita 'Mutoongoria Njaamba’; yaani 'kiongozi shujaa’. Je, nilikuwa mwendawazimu wakati huo? Nawaomba kufungua macho na kuona kule nchi inapoelekezwa na uongozi wa Rais Kenyatta,” akasema Odinga wakati akihutubu katika Kaunti ya Kiambu majuzi.

Odinga alisisimua wakazi kuhusu mradi wa Reli ya Kisasa.

“Sisi na Kibaki ndiyo tuliipachika mimba (kuianzisha) reli ya kisasa ambayo wanajidai wameianzisha. Miradi yote ya barabara ni sisi tuliianzisha. Kwa hivyo, hakuna lolote ambalo wamewafanyia Wakenya, isipokuwa kuwafilisi kwa kuwanyima hata unga! Mimi ndio baba wa miradi hiyo yote.”

Kalonzo Musyoka, mgombea-mwenza, NASA

Akimkabili Ruto kwamba alikuwa akifadhiliwa na mfanyabiashara Jimi Wanjigi anayekumbwa na utata.

“Anayejua ukweli kamili kumhusu Ruto ni Jimim Wanjigi. Ndiye aliyekuwa akimfadhili, hadi pale walikosana, baada yake (Ruto) kujawa na kiburi wakati alipoingia serikalini. Tutaufichua ukweli huo.”

Gavana Ali Hassan Joho wa Mombasa (akiwakabili UhuRuto)

“Mara hii hatutarudi kwa Wakenya kuwaambia kura zetu zimeibwa. Hilo naomba mtuachie. Sisi ndio majenerali wa Raila Amollo Odinga. Tulimwambia atuachie kibarua cha kuwakabili Rais Uhuru na Bw Ruto.”

Joho akiwatahadharisha Wakenya dhidi ya kujiunga na Jubilee, akiitaja kama “matatu ya mkosi.”

“Unapoingia matatu, unapaswa kutahadhari sana. Ikiwa matatu hiyo inaendeshwa na mlevi, na kondakta wake ni mwizi, basi haina usalama hata kidogo. Hivyo ndivyo Kenya ilivyo.”

Mbunge Junet Mohamed (Suna Magharibi) akimsuta Ruto kwa kumrai Kalonzo ajiunge na Jubilee.

“Nashangaa sana kumsikia Ruto akijipigia debe hata kabla hajajua matokeo ya 2017 yatakuwa vipi. Anapaswa kujiunga nasi ili Bw Kalonzo ampe kazi mnamo 2022, atakapoingia Ikulu.”

Kiongozi wa ANC  Musalia Mudavadi akiwasuta UhuRuto kwa ufisadi nchini.

“Nasa hao (UhuRuto)! Wanase hao! Hatutaki kuona Wakenya wakihadaiwa kwa miradi mikubwa mikubwa ilhali hawawezi kupata ugali! Nasa hao!”