http://www.swahilihub.com/image/view/-/4802712/medRes/2142251/-/geyru4z/-/fau.jpg

 

‘Nyumba salama’ kuwanusuru wanawake, watoto

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile  

Na Waandishi Wetu

Imepakiwa - Friday, October 12  2018 at  11:43

Kwa Muhtasari

Ukatili wa kijinsia unafanywa na watu wa karibu wa familia

 

 

Dar/ Pwani. Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile amesema Serikali itaweka utaratibu wa ‘nyumba salama’ itakayotumika kuwahifadhi wanawake na watoto waliokimbia vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Amesema nyumba hiyo salama itawahifadhi watu hao kwa muda, wakati Serikali ikifuatilia kwa karibu na kuchukua hatua stahiki ya sababu zilizochangia ukatili wa jinsia

Dk Ndugulile ambaye pia ni Mbunge wa Kigamboni alieleza hayo jana wakati akifunga mjadala wa kitaifa wa siku tatu uliohusu changamoto za ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni.

Alisema ukatili wa kijinsia unafanywa na watu wa karibu wa familia na ikitokea amefanyiwa na baba, babu au mjomba, mtoto husika anajikuta anashinikizwa kubadilisha maelezo yake ili undugu au ukoo usivunjike.

“Wakati Serikali inayafanyia kazi matukio haya, mtoto atakaa katika nyumba hii salama katika mikono ya Serikali na wadau hadi pale shauri lake litakapokuwa limekamilika,” alisema Dk Ndugulile.

Pamoja na mambo mengine, Dk Ndugulile alisema mwakani kutakuwa na tuzo maalumu kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala watakaokuwa wakisimamia vyema vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Pia, tuzo hizo zitawahusisha pia waandishi wa habari wa runinga, redio, magazeti na mitandao ya kijamii itakayoripoti na kufichua vitendo hivyo.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo anayehusika na Maendeleo ya Jamii, Dk John Jingu alisema mjadala huo ulioshirikisha wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini na umetokana na maazimio 10 yakatayokabidhiwa kwa wakuu wa mikoa ambayo ina changamoto ya ukatili wa kijinsia.

Huko Kisarawe mkoani Pwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Mussa Gama alisema wanafunzi 41 wa shule za msingi na sekondari katika wilaya hiyo walikatishwa masomo yao baada ya kupata ujauzito kati ya Januari 2017 na Septemba 2018.

Alisema hali hiyo imesababishwa na umbali mrefu kutoka makazi wanayoishi, wanajamii kutojua vyema kuhusu ukatili kwa watoto wa kike, unyago pamoja na mikusanyiko ya usiku ikiwamo vigodoro.

Hayo yalisemwa jana wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike katika wilaya hiyo yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Kazimzumbwi.

“Ndiyo tulitoa mapendekezo kuwa itungwe sheria ambayo itawabana wanandugu na jamii inayomzunguka mtoto huyo ili kuweza kuwabaini watu hawa na kuwachukulia hatua zinazotakiwa,” alisema Gama.

Alisema pia wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitumia fedha zao kuzima kesi pindi wanapowapa watoto hao mimba ili wasiweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Hii inaonyesha jinsi gani tatizo hili ni kubwa katika wilaya yetu kwa sababu hao tumeweza kuwabaini kutokana na kukatishwa masomo, vipi kwa wale ambao hawako katika mfumo rasmi wa elimu?” alisema Gama.

Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), John Ambrose alisema licha ya kuwapo kwa kampeni mbalimbali zinazohamasisha utokomezaji wa mimba za utotoni na ukeketaji, bado kuna mambo sita ambayo yakifanyiwa kazi azma hiyo itafanikiwa.

Mambo hayo ni miundombinu dhaifu ya maji, kutopata nafasi ya utulivu wa kujisomea baada ya shule, watoto wengi kushiriki katika mikusanyiko hatarishi wakati wa usiku, kudhibiti rushwa kwa wale wanaowapa mimba wanafunzi, wasichana kukosa masomo siku za hedhi pamoja na wanajamii kutojua kuhusu ukatili kwa watoto wa kike.