http://www.swahilihub.com/image/view/-/3445526/medRes/1482813/-/ic1bb1/-/WAL.jpg

 

GWIJI WA MWAKA; WALLAH BIN WALLAH: Mwandishi mashuhuri, mwalimu wa walimu na bingwa wa nasaha

Wallah bin Wallah

Mwanzilishi wa Tuzo za WASTA Bw Wallah Bin Wallah. Picha/ CHRIS ADUNGO 

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, December 28  2017 at  14:25

Kwa Mukhtasari

NIMEJIHISI mabruki kuwa miongoni mwa watu wa kwanza baada ya Mrembo ES ESS Estallah, Kapteni Jittu Kamaliza Ndedah na Nahodha Hassan Kauleni mwana wa Ali kusoma vitabu Utamu wa Sarufi, Utamu wa Insha na Utamu wa Ufahamu ambavyo ni vya maana sana maishani.

 

Vitabu hivi alivyoviandika Doyen wa Kiswahili, Guru Ustadh Wallah Bin Wallah kwa kushirikiana na mwalimu Abubakar Tsalwa vilichapishwa mnamo 2017 na kampuni ya Herald chini ya usimamizi wa Bw David Amiani Omuruli.

Ni vitabu vya kutia moyo na kumshajiisha yeyote mwenye azma ya kujiendeleza maishani na kitaaluma. Waandishi wamegusia kwa kina mambo mengi matamu yanayopania kumchochea mwanafunzi pamoja na mwalimu kujitambua kisha kujiboresha katika jitihada za kuyasaka malezi bora ya kiakademia.

Mvuto na mguso uliomo ndani ya vitabu hivi una uwezo wa kubadilisha kabisa mkondo wa fikira na mitazamo ya wengi wasiofahamu uzito, ukubwa na utamu wa thamani ya kujifunza Kiswahili bora.

Nina hakika hapo ulipo, hutabaki jinsi ulivyo wala kuendelea kuwaza kwa namna ulivyozoea pindi utakapofanikiwa kusoma ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho wa vitabu Utamu wa Sarufi, Utamu wa Insha, Utamu wa Ufahamu na Utamu wa Msamiati.

MABADILIKO
Kumbuka mabadiliko ya kweli huanzia kwa mtu binafsi, na upekee wa vitabu hivi ni kwamba mbali na kukuwajibisha kwa asilimia 100, pia vitakufunza kusema “chanzo cha mabadiliko yangu ni mimi”.

Waandishi wowote wale - wa habari, magazeti, vitabu au sanaa yoyote inayoambatana na utunzi - wana mwanzo! Kuna kipindi walipoanza kutambaa kabla ya kusimama dede katika safari ya uandishi. Walitamani sana kuandika vizuri na kuwa bora, wakashindwa pa kuanzia wala kumalizia.

Walitamani kuinua majina yao yasomeke miongoni mwa wasomaji na waandishi wenzao, lakini walijikuta wakibweta bila mafanikio. Kazi ya uandishi ni ngumu, yenye kuhitaji uvumilivu na kujifunza sana. Mwandishi chipukizi huwa katika mazingira ya aina hiyo.

Kumbuka kipaji pekee hakiwezi kutoa kitabu bora. Unastahili kukifanyia kazi kipawa chako na kusoma sana ili uwe tajiri wa lugha kwa sababu vitabu ni benki zinazobeba akiba ya elimu na maarifa. Ukitaka kuwa mshairi, tunga mashairi. Ukitaka kuwa mkulima, lima uboreshe ujuzi wako!

Kwa uzoefu wa miaka ya kutagusana na kutangamana na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, nimejifunza, kuona na kusikia machache mazito kutoka kwake. Nimeonja ukubwa wa mafao ya Kiswahili na kujifunza kwamba asiyejua ngeli hajui Kiswahili.

Nimejifunza kuwa mafanikio hutafutwa na ubora wa mtu umo ndani ya mtu mwenyewe. Nimejifunza kupirikana kwa sababu wakati hukatika na kazi ni kipimo cha utu.

Nimejifunza kwamba jana si leo na siri ya maisha imo ndani ya maisha kwa sababu kesho yako imo ndani ya leo yako. Nimejifunza kujipa moyo wa matendo na kuwauliza wajuao kwa sababu siri ya kujifunza ni kujifunza tu kwa bidii.

UBORA
Panapo afya, uzima na uhai, ninaamini ulimwengu mzima utazidi kuambukizwa utamu na ubora wa mbinu ya kalamu ya Guru Ustadh zaidi ya haya machache ambayo nimejifunza kwa kipindi kifupi.

Kupitia kwa Wallah Bin Wallah, nimejifunza kwamba ualimu ni mwito, Kiswahili ni ajira na uandishi ni kipaji.

Vipaji navyo huzidiana! Kwa maoni yangu, kati ya viatu vikubwa zaidi vya utunzi ambavyo waandishi wengi huogopa sana kuvalia kwa hofu ya kushindwa kutoshea kirahisi, ni jinsi ya kueleza kwa mafanikio kabisa namna wenye lugha yao wanavyoitumia au wanavyostahili kuitumia badala tu ya kutoa mwongozo wa ni vipi lugha hiyo itumike. Si kwa Guru Ustadh!

Wallah Bin Wallah ana uwezo wa hali ya juu wa kuzichota hisia zako akakurudisha nyuma mamia ya miaka hadi ukajihisi kuwa sehemu ya jamii isiyojua dini za kileo, nguo za Kimagharibi, motokaa, vyakula na masuala mengine ya tamaduni za ng’ambo tunazozikumbatia na kuabudu hivi sasa kwa kukumbatia lugha za kigeni badala ya Kiswahili kilicho kitambulisho chetu!

Kwa ufundi wake wa lugha na ujenzi wa taswira, Wallah Bin Wallah ametumia vifungu vingi katika kitabu Utamu wa Ufahamu kukupeleka katika dunia ya mababu iliyojali utu, kuwaheshimu wazee, kuthamini kazi na kutawaliwa na miungu, mizimu na ‘mafundi wa ndumba’ kufu ya Abubakar Tsalwa!

Gazeti hili liliwahi kuangazia historia fupi ya maisha ya Wallah Bin Wallah katika chapisho la Machi 10, 2016. Guru Ustadh ndiye aliyekuwa mtakadamu wa ukumbi huu wa GWIJI WA WIKI, safu iliyoanzishwa na usimamizi wa Taifa Leo kwa nia na madhumuni ya kutambua juhudi za wapenzi na watetezi wafia-lugha pamoja na upekee wa michango yao katika majukwaa mbalimbali ya makuzi ya Kiswahili.

Kupitia kwa ualimu na uandishi wake wa miaka mingi, Guru Ustadh Wallah Bin Wallah amebadilisha pakubwa sura ya usomaji na ufundishaji wa Kiswahili ndani na nje ya Afrika Mashariki.

Si ajabu kuelewa kiini cha msukumo wa kujihimu, kujihini na kujitolea kwake sabili kutuza ufasaha miongoni mwa watumiaji wa Kiswahili katika sherehe za kila mwaka za Kumi-Kumi zinazodhaminiwa na WASTA Kituo cha Kiswahili Mufti.

NASAHA YA GURU USTADH
Katika maisha, hakuna mafanikio bila kujitolea. Ukitaka kwenda mbali, ni lazima utoke mbali. Ukimwona mtu amefika mbali, ujue ametoka mbali. Umbali wa maisha ni kuishi, si kuisha. Hakuna lisilowezekana katika maisha. Yasiyowezekana, huwezekana. Ukiyaweza yasiyowezekana, ujue kwamba wewe ni mweza. Mtu anayeweza hujiweza pia!

Mti hauendi ila kwa nyenzo na maisha hayaendi ila kwa stahamala. Vumilia kujifunza, utavuna!
Kufanikiwa au kutofanikiwa ni uteuzi wa mtu kwa kuwa ndiye wa pekee mwenye uhuru na mamlaka ya kuamua aina ya maisha anayoyataka.

Akili uliyonayo ni wenzo muhimu wa kukufanya ufaulu endapo utakitumia kipaji chako vilivyo na kukifanyia kazi njema.
Endapo utatumia akili, hisia na imani yako kwa hekima, maisha yako yatakuwa na mabadiliko makubwa ya heri.
Safisha akili yako kwa mawazo mazuri. Jiamini, jione imara na uiambie nafsi yako kwamba utafanikiwa katika mambo yote uliyoyapanga.

Kuwa mtu anayependa kuwajali wengine, mwaminifu katika shughuli pamoja na familia yake. Ukweli na ujasiri ni sifa muhimu na za lazima kwa yeyote anayesaka ufanisi kuwa nazo maishani.

Usiruhusu mawazo ambayo hayana tija ya maendeleo maishani mwako. Usiwe mwepesi wa kukata tamaa. Kuwa na msimamo, enda na wakati na usiwachukie washirika wako. Hakuna kitu kibaya zaidi katika maisha ya mtu kuliko chuki!

Utakapobadili tabia yako ya ndani, hata ya nje itajibadili. Mawazo yana nguvu. Mawazo ya hofu ni ishara ya kushindwa. Jifunze kushinda hofu ili uwe salama. Utakaposhinda hali ya kutokuwaza kushindwa, utapata ushindi.

Upole na heshima ni nguzo muhimu zitakazokupa mwongozo mwafaka wa kukabiliana na vita vikali vya kila siku kati ya wema na uovu.

Kuna kanuni moja inayotawala mawazo: huwezi kufikiri kitu hiki na kuzalisha kingine. Mwanadamu anaweza kufanikiwa mara nyingi kadri anavyoielekeza akili yake kuyafikia mafanikio.

Kila kazi au uzoefu unaopata ni somo muhimu katika maisha. Elekeza umakini wako wote katika kukamilisha malengo uliyojiwekea na mambo mengine yatafuata. Muhimu ni kuelewa wewe ni nani.

Ili ufanikiwe, ni vyema kuwa na nidhamu katika hisia zako. Kupitia hisia, utajifunza vitu vingi. Endapo hisia zako zitalenga kwenye mafanikio, basi utafanikiwa. Iwapo zitakuwa kinyume, matokeo yake ni masikitiko, upweke, unyonge, kudhoofika kwa mwili na kifo!

Ili ufanikiwe, unatakiwa kuwa na digrii ya subira. Kila jambo haliji kwa wakati mmoja! Kukwea mlima kunahitaji ujasiri, ustahimilivu, nidhamu na imani. Uvumilivu utakujengea kiota cha matumaini kisha ushindi. Matokeo mazuri huwa ni zao la subira!

Unapokuwa na wenzako, usijione bora kuliko wao. Hakuna mtu hata mmoja aliyekamilika. Ota ndoto za mafanikio, zenye thamani na malengo makubwa. Hakutakugharimu kitu kufanya hivyo.

Unapohitaji jambo kubwa kutokea maishani, unatakiwa kuwa na maono mapya yenye matarajio kisha ujiwekee malengo ya mara kwa mara yatakayokuchochea kuyaboresha ya sasa.

Vyovyote uwazavyo, ndoto inainua na kuweka kitu kipya katika maisha. Chukua hatua ambazo zitaifanya ndoto yako kuwa ya kweli. Ndoto inaanza unapokuwa na wazo. Kumbuka watu huvutiwa na wenye maono makubwa. Baadhi ya watu wanapoteza muda wao kwa kuwa na malengo ambayo hayatawasaidia.

Dunia imejaa vipaji vingi na uwezo ambao hautumiwi. Unatakiwa kulima kwa bidii na kupalilia ili upate mavuno bora. Tumia kipaji chako kabla hujakipoteza. Unaweza kudhani kwamba huna kipaji chochote, si kweli. Ni wewe hujakigundua! Maisha yamejengwa katika msingi wa kanuni hiyo. Kuna mifano mingi ya kupoteza au kupata. Huo ndio ukweli wa ukweli!!!