http://www.swahilihub.com/image/view/-/1416324/medRes/365205/-/bkbwm6/-/TFBayreuth-Swahilihub201.jpg

 

Said Ahmed ameandika vitabu 55, anasema mambo bado

Profesa Said Ahmed Mohammed

Profesa Said Ahmed Mohammed Khamis. PICHA/HISANI 

Na HEZEKIEL GIKAMBI akiwa Bayreuth, Ujerumani

Imepakiwa - Tuesday, May 29  2012 at  20:26

Kwa Muhtasari

Umewahi kusoma tamthilia kama vile Pungwa, Amezidi au Kitumbua Kimeingia Mchanga? Ikiwa ni kweli, basi umekumbana na kazi za mwandishi mashuhuri Said Ahmed Mohammed. Orodha ya vitabu alivyoandika au kuchangia ni ndefu. Anasimulia kuhusu maisha na kazi yake.

 

Katika Kongamano la 25 la Kiswahili la Chuo Kikuu cha Bayreuth lililofanyika katika jumba la Iwalewa, mjini Bayreuth Ujerumani wiki iliyopita niliweza kuhudhuria na kukutana na mwandishi mashuhuri zaidi wa fasihi ya Kiswahili ambaye ameandikia nyanja zote. Si riwaya, si tamthilia, si mashairi, si kazi za watoto, si vitabu vya shule. Huyu si mwingine ila ni mwenyeji wa kongamano hili lililoandaliwa mahsusi ili kumuenzi anapostaafu kutoka chuo hicho-Profesa Daktari Said Ahmed Mohammed Khamis.

Swali: Jina Said Ahmed Mohammed ni jina kubwa sana katika fasihi ya Kiswahili. Wasomaji wangependa kumfahamu mtu huyu. S.A.M. ni nani?

Jibu: Mimi ni binadamu wa kawaida. Nilizaliwa Pemba, mnamo Tarehe 12 Disemba 1947. Nilijiunga na shule ya Msingi ya Darajani ambayo iko Zanzibar mjini na baadaye nikaendelea na masomo yangu ya /sekondari katika Shule ya Upili ya Gulioni iliyokuwa kitambo ikiitwa King George the VI. Baadaye nilijiunga na chuo cha ualimu cha Nkrumah TTC, mjini Zanzibar mwaka wa 1966.

Nilipofuzu chuoni nilifundisha shule ya Msingi ya Kizimbani kwa wiki mbili tu halafu nikahitajika kuenda kufundisha Shule ya sekondari ya Utaani baina ya 1969 na 1974. Nilikuwa nikifundisha masomo ya Biolojia, Hesabu na Kemia na pia Kiswahili. Kwa kuwa nilikuwa bado nikiandika hadithi fupi zilizosomwa katika vituo vya BBC na DW Welle, hapa ndipo nilipopata wazo la kuandika Asali Chungu.

Baadaye nilijiunga na kidato cha 5 na 6 (A-level) nikipanga kuendelea kufanya masomo ya sayansi. Palikosekana vifaa vya kufanyia masomo ya utekelezi wa kisayansi (practicals) na hivyo nikachagua kufanya masomo ya kisanaa.

Swali: Kwa hivyo Profesa ungepata shule yenye vifaa hivyo, tungekuwa na Said Ahmed Mohammed mwanasayansi na labda Kiswahili kingekosa mwandishi kama wewe.

Jibu: (Kicheko)Aaah! Sidhani hivyo. Uandishi umekuwa katika damu yangu tangu utotoni. Hujaona watu wanaoandika na bado ni wanasayansi au wanafanya kazi tofauti? Kwa mfano kuna Daktari Yusuf Dawood n.k. Mimi nilipenda kusoma na kutunga mashairi na hadithi fupi. Hata hadithi zangu zilisomwa redioni katika idhaa za BBC-Swahili, DW welle.

Nilipokuwa darasa la tano mashairi yangu yalitumiwa na walimu katika kuchambua na kufundishia madarasa ya juu. Nilifanyiza kazi talanta yangu.Nafikiri bado ningekuwa mwanasayansi mwandishi. Nashukuru Mungu nilifanya vyema katika kila somo.

Swali: Ni lini ulipojiunga na chuo kikuu na uliendeleaje?

Jibu: Mnamo 1976 nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea shahada ya kwanza ya BA katika Elimu-nikimakinikia Isimu na Fasihi ya Kiswahili. Baada ya kufuzu katika shahada hiyo nilirejea nyumbani Zanzibar na kuwa mwalimu mkuu wa Shule za Msingi na Upili za Hamamni kwa miaka mitatu. Nilikuwa na wasaidizi kama watatu hivi kila moja akiwa na kiwango maalumu cha kusaidia kama shule ya Msingi, ya upili, utawala na kadhalika.Nilirudi tena Chuo kikuu cha Dar es Salaam na kujisajili kusomea shahada ya Uzamili yaani MA katika Isimu tekelezi nilipoangazia kazi za mwenzangu Mohammed Said Mohammed.

Nilipokuwa nikisoma hapa, kipawa changu kilimvutia mwalimu wangu wa kutoka Ujerumani aliyefundisha Isimu linganishi na ya Kihistoria Bw.Sigmund Brauner. Hapa ndipo fursa ya kuelekea Ujerumani kufanya shahada ya Uzamifu yaani PhD na pia kufundisha ilipotokea. Nilijiunga na Chuo Kikuu cha Karl Marx Leipzig hapa Ujerumani mwisho wa mwaka wa 1981 na kukamilisha mwaka 1985.Sasa nikawa Daktari. Hapa nilikuwa pamoja na familia yangu.

Swali: Ulipokamilisha shahada hii muhimu, ulibakia Ulaya kufundisha?

Jibu: La hasha! Niliteuliwa na Rais wa Zanzibar wakati huo Mzee Idris abdul Wakil na kurejea nyumbani Zanzibar na kuwa Mkurugenzi wa pili wa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) baadaye iliyokuwa  Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kwa miaka miwili. Niliondoka kwa sababu za kisiasa na fitina za watu ambao sikuwafahamu.

Baadaye nilienda Kenya mnamo 1987 na kuwa mwenyekiti wa kwanza wa Idara ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Moi mjini Eldoret na baadaye kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi, ndaki ya Kikuyu hadi mwaka wa 1990. Nilipotoka Nairobi nilielekea Japan katika Chuo Kikuu cha Osaka idara ya lugha za kigeni. Nikiwa Japan ndipo nilipata uprofesa. Nilipotoka Osaka, Japan ndipo nikaja hapa Chuo Kikuu cha Bayreuth tangia 1997 hadi wa sasa nafundisha hapa.

Swali: Wengi wamekutaja kama mwandishi mashuhuri zaidi Afrika Mashariki na hata Afrika nzima ukiwa umeweza kuandika riwaya, tamthilia, mashairi, kazi za watoto na hata vitabu vya shule na vyuo. Je, umeandika vitabu vingapi?

Jibu: Vingi tu! Nafikiri nimeandika vitabu zaidi ya hamsini na vitano (55). Kuna vya Mashairi kama Sikate Tamaa (1980), Kina Cha Maisha (1984), Jicho la Ndani (2002), na tamthilia kama Pungwa (1988), Kivuli Kinaishi (1990), Amezidi (1995), Kitumbua Kimeingia Mchanga (2000), pamoja na rafiki yangu Prof.Kitula King’ei tumeandika Posa za Bi Kisiwa (2007), na riwaya kadha kama vile Asali Chungu-1977, Utengano-1980, Dunia Mti Mkavu-1980, Kiza katika Nuru 1988,Tata za Asumini 1990, Babu alipofufuka-2001,Dunia Yao- 2006,  na ya majuzi zaidi Nyuso za mwanamke- 2010 na vingine kadha. Baadhi ya kazi zangu zimetafsiriwa kwa lugha za kigeni pia.

Pia kuna miswada ambayo itachapishwa hivi karibu ya riwaya ya Mkamadume, Mhanga nafsi yangu na kitabu cha kusomwa katika darasa la saba hivi kiitwacho Gharama ya Amani kiachoangazia  fujo za kisiasa zilizotokea Kenya.

 

Swali: Ni gani miongoni mwa hivi vyote kwa maoni yako unachofikiria ni kitabu maarufu zaidi au unachokipenda kuliko vyote ulivyowahi kuandika?

Jibu: Wewe si wa kwanza kuniuliza swali hilo. Nitasema kuwa kazi za uandishi ni kama watoto wangu. Siwezi nikakwambia nampenda huyo na simpendi huyo mwingine. Lakini nafikiri Nyuso za Mwanamke (2010) ni riwaya ambayo ilinipeleka mbele sana kama mwandishi na kunipa ujasiri zaidi. Pia wachapishaji wananiambia vile kuinavyonunuliwa na vile kinavyorudiwa kutolewa Nakala haraka ni ishara ya kuwa kinasomwa sana. Hata yasemwayo na wahakiki ni muhimu kwangu.

Swali: Je, nini maoni yako kuhusu mchango wa Muungano wa Afrika Mashariki katika kukuza lugha ya Kiswahili?

Jibu: Kila siku nasema kuwa hakuna njia ya kukiua Kiswahili?  Wapo watu wanaodhania kuwa lugha zao zinawafaa zaidi kiuchumi na wanafikiri Kiswahili hakiwezi baadhi ya mambo.Kiswahili kinaweza kutumika na muungano huu kufungua nafasi za kiuchumi.

Kiswahili ni nyenzo ya kiuchumi na sio kisiasa. Hasa kikienda pole pole kwenye mitaala na kufundishia masuala ya kitaaluma. Nimesafiri Japan, China, Korea na nimeona mantiki ya jambo hilo. Wamepiga hatua kubwa kimaendeleo kutumia lugha zao. Nani kasema sayansi ni ya Kingereza au Kifaransa tu? Nafikiri pale Tanzania ilipokosea ni pale ilipokuza Kiswahili tu na kupuuza alichokiita Mwalimu Nyerere-Kiswahili cha Dunia- alimaanisha Kingereza. Ni bora kushika zote ili tuweze kupiga hatua.

Nchini Kenya, hali ni tofauti kwani walishika Kiingereza na sasa wameweka mikakati ya kukuza Kiswahili kama lugha rasmi. Muungano uibuke na sera bainifu za lugha ya Kiswahili na kuzioanisha katika Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki.

Swali: Nashukuru kuwa ulimakinikia wasilisho langu kuhusu Swahilihub. Je, unafikiri tovuti kama yetu ina fursa gani katika kueneza Kiswahili kote ulimwenguni?

Jibu: Mwanzo ni muhimu watu watambue kuwa hili ni jambo kubwa sana ambalo Shirika la Nation Media limefanya na mtaona uzuri wake. Si jambo dogo. Pili, ifahamike kuwa njia ya kiteknolojia au kidijitali ndiyo ya kipekee katika karne hii ya kuweka lugha katika kila medani. Hatua yenu ni taji kwa Kiswahili. Nawapa hongera tovuti ya www.swahilihub.com

Swali: Je, Profesa una familia?

Jibu: Ndiyo. Yupo mke wangu Rahma nimpendaye na watoto wetu wawili, msichana na mvulana. Binti anaitwa Najima jina linalomaanisha nyota. Naye bwana mdogo aitwa Mahir- neno la Kiarabu kumaanisha mwenye ujuzi. Wote wamekamilisha masomo ya shahada ya kwanza. Najima anajipanga kuendeleza masomo yake naye Mahir ataka kupata kazi mwanzo. Tunashukuru Mungu.

Swali: Leo unastaafu kutoka Chuo hiki cha Bayreuth baada ya kufundisha kwa miaka 13. Unaelekea wapi sasa na je, ulitimiza uliyoyalenga hapa?

Jibu: Inshallah, mimi narudi nyumbani Zanzibar yaani kwangu Pemba ili niweze kuketi na kutulia nikilenga kupanua nafasi za kiubunifu katika maandishi. Hapa nitaweza kuandika niliyoyawazia kwa kuwa muda utakuwepo sasa. Hapa Bayreuth, nimekuwa na malengo ya chuo na ya Kibinafsi. Alhamdulilahi, yote yametimia.

Upande wa chuo, nimekuwa Profesa wa Fasihi za Kiafrika katika Lugha za Kiafrika na hakuna profesa mwingine katika eneo hilo Uropa nzima. Pia nimegundua kuwa zipo fasihi nyingi tu, ila mimi nimekuwa balozi wa aina hiyo ya fasihi huku Ulaya. Kazi zangu zinaenda sambamba na za mwandishi mashuhuri wa Ujerumani Günter Wilhelm Grass.

Pia nimewashauri wanafunzi wengi wa Phd kutoka Kenya na kwingineko. Aidha nimeingiza somo la nadharia na kuamsha usomi wa wanafunzi hapa chuoni na hata kuweza kulinganisha fasihi za Afrika Mashariki na Afrika Magharibi.

Kwa upande wangu, nimesoma mwenyewe na kufungua macho yangu kuhusu mambo ambayo nisingeweza hata kuyafikiria. Kuwa kwangu hapa kumenijifunza uhusiano wa kimataifa, kufikiriana, kusaidiana na kutoana unyama uletwao na kudhulumiana. Nawashauri vijana waangalie watu katika jamii walio vilelezo bora na wafuate nyayo zao kwa kufanya bidii na kujitolea. Vijana waunge mtandao na wasomi wengine wanaoweza kuwashika mkono maishani.

Bw Gikambi ni Meneja wa Mradi wa Swahili Hub