http://www.swahilihub.com/image/view/-/2709800/medRes/855729/-/cfrte1z/-/DNEALA0305A.jpg

 

John Mbadi: Kiungo thabiti kwa Raila Odinga kisiasa

John Mbadi

Mwenyekiti wa ODM John Mbadi. Picha/EMMA NZIOKA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Saturday, December 30  2017 at  12:39

Kwa Mukhtasari

Mtaje John Mbadi Ng’ongo na utapata taswira ya mwanasiasa shupavu ambaye uaminifu wake kwa sera za kinara wa National Resistance Movement (NRM), Raila Odinga sio wa kupimika kwa kuwa utavunja ratili kwa uzani.

 

MTAJE John Mbadi Ng’ongo na utapata taswira ya mwanasiasa shupavu ambaye uaminifu wake kwa sera za kinara wa National Resistance Movement (NRM), Raila Odinga sio wa kupimika kwa kuwa utavunja ratili kwa uzani.

Ni mwanasiasa ambaye akikupata unamshambulia makonde Odinga, yeye ndiye atahisi uchungu wa makali na atalia kwa niaba ya Odinga.

Kwa sasa ndiye kinara wa walio wachache bungeni, hivyo basi ndiye macho na masikio pamoja na misuli ya ‘Baba’ ndani ya bunge la kitaifa.

Ni hivi majuzi tu Spika Justin Mutur alimtimua kutoka bunge kwa muda wa saa kadha baada ya kukataa katakata kutambua kuwa taifa hili liko na Rais halali kwa jina Uhuru Kenyatta.

Alikataa katakata kuonywa, akakataa kuomba msamaha, akakataa kuondoa usemi huo wake usinakiliwe rasmi katika hifadhi ya bunge na hata alipoelezewa kuwa angetimuliwa, akasema kutimuliwa kungempa raha badala ya kumtambua Rais Kenyatta.

Kando na hayo, akiitwa kwa maandamano na Odinga ya kutetea hili au lile, hata wote waingize baridi ya kupambana na vitoa machozi na milio ya risasi wakityawanywa,Mbadi ndiye huonekana akiwa wa mwisho kutorokea usalama wake, akiwa amehakikisha kuwa Odinga ameondoka akiwa salama.

Mbadi ni mzawa katika kijiji cha Seka, kata ndogo ya Lwala huko Suba ndani ya Kaunti ya Homa Bay.

Alizaliwa mwaka wa 1972 akiwa kitinda mimba katika familia ya watoto saba.

Uasi

Mbadi kwa uaminifu wake aliteuliwa na Odinga kuwa mwenyekiti wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) ili kuzima mawimbi ya uasi yaliyokuwa yakianza kujipenyeza ndani ya uwaniaji wa Odinga katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Ana shahada kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi ya Somo la Biashara. Ameiongeza uzito na ana shahada ya uzamili katika somo lilo hilo.

Mbadi alihudhuria masomo yake ya Sekondari katika shule ya upili ya Kokuro, hiyo ikiwa ni baada ya kuhitimu elimu ya msingi katika shule ya msingi ya Ligongo.

Katika uchaguzi wa 2008, Mbadi aliteuliwa na Odinga kuwania ubunge wa Suba na kwa urahisi akaibuka mshindi na tena kwa awamu ya pili akaibuka mshindi mwaka wa 2013 na sasa bado yuko afisini akihudumu kwa awamu ya tatu kama mbunge .

Mbadi sio tu mwanasiasa wa ujana wa kuonekana akicheza ngoma na kusakata lele za mrengo wa Odinga, bali ni kamilifu kifamilia ambapo ni mume kwa wanawake wawili.

Wanawake hao ni Catherine Achieng Onyango-Mbadi na ambaye kwa pamoja wamejaliwa watoto watatu kwa majina Benjamin, Natalie Mbadi na Maxwell Mbadi.

Kwa mapenzi ya maulana ajuaye sababu katika hali zote, aliaga dunia Februari 2016 kutokana na kulemewa na makali ya saratani, akimfuata mamake mzazi mheshimiwa Mbadi, Mama Slermina Yambo Ng’ongo aliyeaga dunia Septemba 2015.

Mke wa pili anaitwa Rhoda Mbadi.

Taifa likielekea katika uchaguzi wa 2017, kulizuka patashika ya aibu kati ya Mbadi na na mwenzake wa Rarieda, Nicholas Gumbo (alianguka).

Mbadi alijitokeza hadharani akimtaka Gumbo amuombe msamaha kwa kumsengenya kuwa “una mke ambaye ni tasa asiye na uwezo wa kukuzalia mwana”.

Mbadi alisema kuwa Gumbo alitoa madai hayo katika mahojiano ya redio inayotangaza kwa lugha ya Dholuo.

Gumbo alijitetea kuwa “tofauti zetu na Mbadi sio kubwa lakini yeye huzigeuza kuwa za kibinafsi”.

Gumbo alisema kuwa hajawahi kushambulia bibi ya Mbadi kwa lolote la aibu “lakini huwa nikisema ukweli kwa kuwa ukweli huo unaweza ukathibitishwa.”

Alisema: “Mbadi huwa na utoto wa kisiasa na huwa anapendelewa na Odinga kiasi cha kupewa uongozi wa ODM bila kutoa jasho.”

Huku siasa za ukaidi dhidi ya utawala wa Jubilee zikitarajiwa kuendelezwa ndani ya Mwaka Mpya wa 2018, jina la Mbadi litakuwa kiungo muhimu kwa Odinga, ndani na nje ya bunge.