Watumishi wasimamishwa kazi sakata la gari la kubeba wagonjwa kukutwa na mirungi

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  

Imepakiwa - Friday, July 13  2018 at  16:26

Kwa Muhtasari

Iwapo wakibaika hawana hatia watarudi kazini

 

Dar es Salaam: Sakata la gari la kubeba wagonjwa la Halmashauri ya Mji wa Tarime, kukutwa na kilo 800 za mirungi, limewasimamisha kazi watumishi wanne wa halmashauri hiyo akiwamo Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Innocent Kweka.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa jana aliwasimamisha kazi watumishi hao ikiwa ni siku moja baada ya gari hilo kukamatwa eneo la Bunda, likiwa na mirungi.

Pamoja na Kweka wengine waliosimamishwa kazi ni Kaimu mganga mfawidhi Amir Kombo, Katibu wa hospitali, Rwegasira Karugwa na dereva wa gari hilo George Matai.

Juzi, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema dereva huyo alipigiwa simu akitakiwa kumsafirisha mgonjwa kutoka Hospitali ya Tarime kwenda Bugando lakini akasema ana tatizo la kifamilia na pia gari halina mafuta.

Hata hivyo, gari la polisi lililowabeba wagonjwa hao kuwapeleka Bugando lilikutana na gari hilo na walipolisimamisha ndipo walipokuta shehena ya mirungi.

Mkurugenzi huyo alisema ofisi yake haiwezi kuvumilia kitendo hicho kwani kimechafua jina la halmashauri hiyo na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kushiriki.

“Watumishi watatu watasimamishwa kazi hadi uchunguzi utakapokamilika na wakibainika hawana hatia watarudi kazini, lakini dereva wa gari hilo akimalizana na polisi atafukuzwa kazi mara moja,” alisema Ntiruhungwa.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewaagiza waganga wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanasimamia malengo ya magari hayo.

“Nawaagiza waganga wakuu wa mikoa na wilaya kote nchini kusimamia matumizi ya magari ya kubeba wagonjwa. Kesho kutwa tutatoa tamko rasmi nini makusudi ya kuwapo na yanatakiwa kufanya shughuli gani. Ni marufuku gari la wagonjwa kubeba kitu tofauti,” alisema na kuongeza;

“Yeyote ambaye tumemkabidhi gari la wagonjwa tutamchukulia hatua kali pale atakapokiuka mwongozo.”