http://www.swahilihub.com/image/view/-/4801542/medRes/716477/-/1gs1wmz/-/balozi.jpg

 

Makontena yatelekezwa bandarini Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi  

Na Haji Mtumwa

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  16:37

 

Zanzibar. Uongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar umeagizwa kuyaondoa makontena yote yaliyopo katika Bandari ya Malindi ambayo hayana bidhaa ili kuondoa msongamano wa mizigo katika eneo hilo.

Agizo hilo lilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara ya kushtukiza bandarini hapo kwa lengo la kuangalia utendaji kazi na kushuhudia mrundikano wa makontena.

Balozi Iddi alisema hatua hiyo mbali ya kuondoa msongamano katika eneo hilo, lakini pia itasaidia kuchukua tahadhari mapema kabla ya kusubiri matatizo kutokea.

“Moja ya hatua mnazoweza kuzichukua kwa sasa ni kuwatoza kodi za ziada wanaochelewa kutoa makontena yao kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa,” alisema.

Balozi Iddi aliushauri uongozi huo kulitumia eneo la pembezoni mwa hoteli ya Bwawani kuweka makontena yasiyo na mizigo ili kuepusha msongamao.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Abdullah Juma Abdullah alisema kwamba bandari hiyo hupokea makontena 5,000 kila mwezi wakati uwezo wake ni makontena 4,180. Alisema kwamba kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao wameligeuza eneo hilo kama sehemu ya kuhifadhia makontena yao na kueleza kuwa wameanza kulishughulikia suala hilo pamoja na agizo walilopewa.