http://www.swahilihub.com/image/view/-/4802612/medRes/2138350/-/2ix6jj/-/kike.jpg

 

Tukijipanga fursa kwa kila msichana inawezekana

Mkurugenzi Mkuu wa Tasisi ya Her Initiative, Lydia Charles akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kawe wakati  wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani kwa kutoa elimu ya afya ya Uzazi na kuwapima afya wanafunzi   

Na Maniza Zaman

Imepakiwa - Friday, October 12  2018 at  10:57

Kwa Muhtasari

Asilimia 40 ya wasichana wanaoingia sekondari ndio humaliza kidato cha nne

 

Baada ya kumaliza shule, Calista, akiwa na umri wa miaka 18, alianza kujishughulisha na biashara ya kuuza matofali ya udongo kijijini kwao mkoani Mbeya.

Alishindwa kwenda sekondari kwa sababu wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumlipia ada. Hata hivyo, Calista alielewa kuwa uuzaji wa matofali haikuwa kazi aliyoipenda kwa dhati.

Alichopenda yeye kilikuwa ni kuwa fundi umeme. Wengi wakawa wanamcheka alipowaeleza kuhusu ndoto yake hiyo, wakimwambia kwamba ufundiumeme ilikuwa kazi ya wanaume.

Kilichomsaidia ni kwamba alikuwa na bahati ya kuwa na mama ambaye alimtia moyo wa kuitimiza ndoto yake. Na kweli ikawa hivyo baada ya kumwandikisha chuoni.

Calista alitumia miezi tisa kufundishwa juu ya kuunganisha umeme, kuweka nyaya za umeme na kutengeneza vifaa vya umeme.

Hatimaye alihitimu mafunzo yake na kuwa fundi umeme anayeaminika kijijini kwao. Tangu wakati huo, Calista amekuwa akijiwekea akiba ya fedha kidogokidogo kwa lengo la kununua ardhi na kujijengea nyumba. Lengo hilo, nina hakika, litatimia. Ikiwa jana mataifa yote nchini yaliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, nakumbuka maisha yangu mwenyewe ya huko nyuma.

Mimi kama mtoto kike, nilikuwa na fursa nzuri. Nilikuwa na fursa ya kuchagua kufanya nilichotaka. Nilikulia kwenye mazingira salama. Nilitiwa moyo na kuungwa mkono na wazazi wangu wote pamoja na walimu na jamii iliyonizunguka. Ilikuwa ni fursa iliyoje.

Siishi kujiuliza; hivi maisha yangu yangekuwa vipi nisingekulia katika mazingira haya? Ningefanya nini iwapo katika kila hatua niliyopiga kulikuwa na vizingiti, huku nikiishi kwa hofu? Hapa Tanzania, robo ya wananchi wake ni wasichana wenye umri wa chini ya miaka 18. Hawa wana ndoto na matumaini. Wanachohitaji ni fursa, kusikilizwa na kuungwa mkono katika kujifanyia uamuzi sahihi. Tunapaswa kuwa kitu kimoja katika kuhakikisha kwamba kisa cha binti wa Kitanzania ni kisa cha matumaini, kisiwe kisa cha fursa zilizokosekana.

Takwimu zinaonyesha kwamba ni asilimia 40 tu ya wasichana wanaoingia sekondari, huendelea hadi kumaliza kidato cha nne. Asilimia kama 30 ya wasichana wa Tanzania huolewa wakiwa na chini ya umri wa miaka 18, huku asililmia 27 wakipewa ujauzito wangali wadogo.

Ukatili na ushambuliaji wa kingono dhidi ya wasichana unafikia asilimia 11 kwa mabinti wenye umri kati ya miaka 15 na 19. Asilimia 80 ya vijana wadogo wanaopata maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi (VVU) ni wasichana. Hali hii haifai iachwe kubaki hivi ni lazima ibadilike!

Kwa mwaka 2018, maudhui ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ni “Tuwe Naye: Binti Mwenye Ujuzi”. Huu utakuwa ni mwanzo wa juhudi za mwaka mzima za kuwaleta pamoja wadau katika kuangalia mahitaji makuu na fursa kwa manufaa ya wasichana.

Msisitizo uliowekwa na Serikali juu ya umuhimu wa kuwajengea vijana uwezo, unatoa fursa ya kuleta mabadiliko na kuboresha mwelekeo wa maisha ya mabinti wa Kitanzania.

Mabadiliko haya yanahitaji moyo na kila mmoja wetu kuona thamani na uwezo wa msichana

Yatahitaji kila mmoja wetu aone umuhimu wa kumlea badala ya kumdhalilisha au kumshambulia; tumhamasishe kuliko kumwadhibu.

Tumsikilize binti zaidi ya vile tunavyompa amri, tumpe nafasi na kumshirikisha na kumwacha huru zaidi.