Imepakiwa - Tuesday, April 2  2019 at  08:55

 

Kwa takriban miezi mitatu maduka ya ubadilishaji fedha za kigeni yamekuwa yakipitia hatua mbalimbali ikilinganishwa na ilivyozoeleka kabla ya hapo.

Ilianzia mjini Arusha na baadaye Dar es Salaam ambako Serikali ilifanya ukaguzi maalumu katika maduka hayo ili kujiridhisha kama yanaendesha shughuli hiyo kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.

Katika operesheni hiyo maduka mengi yalifungwa baada ya kubainika kuwa yanakiuka taratibu, kisha Serikali ikatawangazia wahitaji wa huduma hiyo kutumia benki za biashara.

Mbali na hatua hiyo, jana Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitoa tahadhari kwa wananchi kutojihusisha na biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kwa njia zisizo halali.

Dk Mpango alisema watu saba wamekamatwa na kufikishwa mahakamani wakituhumiwa kuhusika na biashara haramu ya ubadilishaji wa fedha hizo.

Tunaunga mkono na kupongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha biashara ya ubadilishaji fedha inazingatia sheria na taratibu za nchi ili kila upande upate haki stahili. Imewahi kuelezwa mara kadhaa kuwa baadhi ya wafanyabiashara hulitumia soko la udalishaji fedha kama kichaka cha utakatishaji pesa ili kujipatia masilahi ya harakaharaka.

Hata hivyo, kwa kuwa biashara ya kubadili fedha siyo haramu kulingana na sheria za nchi, ni vyema fursa ikatolewa kwa walio tayari kufuata utaratibu ili wapate haki hiyo.

Ingawa wapo wafanyabiashara wanaochafua sifa nzuri ya biashara hiyo, tunaamini kwamba hali hiyo haiondoi ukweli kwamba uwepo wa uhuru wa kuchagua sehemu ya kupata huduma kwa kuzingatia masilahi yatokanayo na ushindani wa soko unahitajiwa na wananchi.

Jambo la msingi ni kwa mamlaka husika kutoa sifa, utaratibu na vigezo stahili vinavyohimilika vinavyopaswa kufuatwa kikamilifu kuhakikisha wafanyabiashara walio tayari kufanya biashara hiyo wanaifanya.

Tunasema hivyo tukizingatia kwamba umuhimu wa soko la ubadilishaji fedha unabeba uchumi wa nchi, na hatuoni tatizo kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa ingawa zimekuwa zikilalamikiwa katika baadhi ya maeneo na baadhi ya wafanyabiashara kuwa ni kali mno na zimekuja kwa haraka.

Kwa upande wa wale wanaotekeleza operesheni ya kuwasaka wafanyabiashara wanaokiuka sheria na utaratibu unaoongoza biashara hiyo, ni vyema wahakikishe wanaitekeleza bila ya kuwaonea watu wala kutanguliza masilahi binafsi tofauti na yale yaliyokusudiwa na Serikali.

Kama kuna wafanyabiashara watakaoonekana kwenda kinyume na sheria au utaratibu unaoongoza biashara hiyo na kulazimika kuchukuliwa hatua, basi ni vyema watendewe haki.

Kwa upande wa wananchi hasa wale wanaohitaji huduma ya kubadilisha fedha wazingatie miongozo inayotolewa na Serikali ambayo lengo lake ni kusimamia haki na kuhakikisha wanapata kile wanachostahili.

Kila mmoja anatambua kuwa maeneo ya mipakani ndiko kuliko na mahitaji zaidi ya huduma hiyo, hivyo ni muhimu nguvu kubwa ikaelekezwa huko kuhakikisha huduma inapatikana kwa ukamilifu.

Ni wajibu wa kila mmoja iwe Serikali, wananchi au wafanyabiashara kuzingatia utaratibu tuliojiwekea kisheria.