Mvua zaja, tahadhari ichukuliwe

Imepakiwa - Wednesday, April 24  2019 at  11:07

 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa angalizo la uwepo mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi vitakavyoacha athari katika shughuli za kijamii, kiuchumi, uvuvi na usafiri baharini pamoja na baadhi ya makazi kuzingirwa na maji.

TMA imeitaja mikoa inayotarajiwa kukumbwa na hali hiyo kuwa ni ile yote ya ukanda wa pwani ikiongozwa na Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Lindi, Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Kwa mujibu wa angalizo lililotolewa na meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri wa TMA, Samwel Mbuya juzi, wananchi wanatakiwa kujiandaa kwa kuwa kutakuwa na hali ya mawimbi makali katika ukanda wa Bahari ya Hindi, upepo mkali na mvua kubwa.

Kama tulivyosema hapo juu miongoni mwa madhara yanayoweza kutokea kufuatia mvua hizo ni sehemu za makazi kuzungukwa na maji, ucheleweshwaji wa usafiri na kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Pia kutakuwa na kutawanyishwa au kupeperushwa kwa takataka mitaani, kuanguka kwa majani na matawi madogomadogo ya miti, kuathirika kwa baadhi ya shughuli za uvuvi na usafiri baharini pamoja na ugumu wa upatikanaji wa samaki kutokana na hali ya hewa kuvurugika.

Tunaipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa kuendelea kutoa tahadhari kila inapobaini kuwapo kwa hali ya sintofahamu kuhusu hali ya hewa nchini, lakini tunasikitika kwamba baadhi ya wanaopaswa kuzifanyia kazi taarifa za taasisi hiyo ni kama hawajali.

Hii ni kuanzia kwa wananchi na baadhi ya mamlaka za kiserikali. Kwa mfano, wapo wananchi ambao ni kama wamegoma kuhama kutoka katika makazi yanayokumbwa na mafuriko au athari za mvua, na kila mvua zinaponyesha huonekana wakiokoa mali na maisha yao. Hii ni ishara tosha kwamba hawataki kutoka katika maeneo hayo ambayo zinaponyesha kwa wingi hugeuka kuwa mabwawa. Si wao tu, bali pia kuna mamlaka za kiserikali zikiwamo halmashauri ambazo nazo zimeshindwa kuwashurutisha kuhama. Hizi nazo ni tatizo.

Lakini kwa upande wa halmashauri hizo zimeshindwa kutengeneza miundombinu ya maeneo husika ili iweze kusaidia kuwaondolea kero hii wananchi wanaotaabishwa na mvua. Hizi nazo ni tatizo jingine.

Wakati TMA imekwishatoa tahadhari ambayo kila mmoja kwa nafasi yake kuanzia wananchi hadi taasisi na mamlaka za kiserikali wanapaswa kuizingatia, tunashauri hatua zianze kuchukuliwa mapema ili kuendana na angalizo hilo.

Tunasema hivyo kwa sababu hali ya kutochukua hatua kwa wakati na kusubiri mpaka mvua zinyeshe, ipo siku itatutokea puani pale zitakaponyesha ghafla tena kwa wingi na kutotoa fursa kwa wananchi kuokoa mali wala maisha yao. Hili litakuwa ni janga na pigo kubwa kwa Taifa.

Kama nchi tunapaswa kujifunza kutokana na athari ndogondogo zinazojitokeza pale inaponyesha mvua ndogo ya wastani, ambapo tunachoshuhudia ni athari kubwa, seuze siku itakaponyesha kubwa bila kutarajiwa.

Kwa wananchi, huu ni wakati wa kuhama mabondeni na kuchukua tahadhari kwa wale waishio katika maeneo hatarishi hususan yanayotuamisha maji.

Kwa mamlaka na taasisi za Serikali ni vyema zijiandae mapema kukabili athari, ikiwamo kujenga na kukarabati miundombinu ya mvua ili itakaponyesha, maji yasiathiri maisha na mali za wananchi.