http://www.swahilihub.com/image/view/-/4012174/medRes/1699822/-/f0xv36/-/hu.jpg

 

Afrika Giza kabarikiwa kipaji cha muziki na uigizaji

Afrika Giza

Mwanamuziki Afrika Giza. Picha/MARY WANGARI  

Na MARY WANGARI marya.wangari@gmail.com

Imepakiwa - Wednesday, July 12   2017 at  12:16

Kwa Mukhtasari

Msanii aliyetupambia ukumbi wetu leo anafahamika kama Afrika Giza kwa lakabu yake ya kisanii na kando na kuimba muziki aina ya Hip hop yeye pia ni mwandishi wa michezo ya kuigiza.

 

MSANII aliyetupambia ukumbi wetu leo anafahamika kama Afrika Giza kwa lakabu yake ya kisanii na kando na kuimba muziki aina ya Hip hop yeye pia ni mwandishi wa michezo ya kuigiza.

Msanii huyu mwenye talanta ya kipekee vilevile ametunga wimbo kuhusiana  na kitabu maarufu cha mchanganuzi tajika wa maswala ya kisiasa Mutahi Ngunyi ‘The Hard Tackle.’

Alitutembelea katika ukumbi wetu ambapo alitufahamisha mengi zaidi kumhusu jinsi ifuatavyo;

SWALI: Tufahamishe zaidi kukuhusu

JIBU: Jina langu halisi ni Kelvin Gitangara, nina umri wa miaka 33. Mashabiki wangu wananifahamu kama Afrika GIZA kwa lakabu ya kisanii. Mimi ni mzaliwa wa pili katika familia ya watoto wanne, wasichana wawili na wavulana wawili.

SWALI: Uligundua lini na vipi kwamba una kipaji cha mziki?

JIBU: Niligundua talanta yangu tangu utotoni nikiwa katika shule ya msingi ya St Annes Kisaju.  Nilipokua shuleni, nilikuwa nikishiriki mashindano ya nyimbo za kitamaduni na pia katika michezo ya kuigiza au ukipenda drama.

Baadaye nilijiunga na shule ya upili ya Ol-Kejuado ambapo niliendelea kutia makali kipaji changu kupitia nyimbo za kiasili na michezo ya kuigiza.

SWALI: Ulijiendeleza vipi kimuziki baada ya masomo?

JIBU:Baada ya shule ya upili, nilijiunga na kundi lililokuwa likiitwa Ukoo Flani. Baadaye pamoja na wenzangu wengine, tuliunda kikundi cha wasanii kilichoitwa 115 Crew kwa lengo la kufanya mziki na kuandaa tamasha mbalimbali.

Hatimaye niliamua kwenda solo hadi hii leo.

SWALI: Kwa nini ukachagua jina Afrika GIZA, nini maana yake?

JIBU: Nilichagua jina hili kwa sababu Afrika ni nchi yangu, mahali ninapotoka huku GIZA ikiwa akronimu zenye maana ya Great Inspired Zeal to Achieve.

SWALI: Kuna mwanamuziki yeyote katika familia yako ambaye pengine ulimrithi?

JIBU: Naam, nafikiri nilimrithi mamangu katika uimbaji. Alikuwa akiimba nyimbo maarufu za injili katika enzi zake na kujirekodi. Alikuwa akiimba nyimbo za wasanii tajika kama vile Munishi.

SWALI: Umetoa albamu yoyote kufikia sasa?

JIBU: La hasha. Sina albamu yoyote kwa kuwa mtindo wangu ni  wa Freestyle.  Hata hivyo kufikia sasa nina nyimbo nane.

SWALI: Nini hasa kinachangia maudhui ya nyimbo zako?

JIBU: Aghalabu mimi hutunga nyimbo zangu kutokana na ninayoona, kuhisi, au matukio ya kila siku maishani mwangu. Nyimbo zangu zinasisitiza mno Uhuru wa mawazo.

SWALI: Unamaanisha nini kwa ‘uhuru wa mawazo'?

JIBU: Naamini kuwa ikiwa jamii imekombolewa kimawazo, yaani ina uwezo wa kufikiri kivyake bila shinikizo lolote, basi  tunaweza kufanikisha mengi zaidi pasipo vurugu na fujo.

SWALI: Umewahi kupokea mafunzo yoyote ya muziki?

JIBU: La, kwangu mimi usanii ni kipaji nilichozaliwa nacho.

SWALI: Kando na uimbaji, ni yapi mengine unayofanya kuhusiana na usanii?

JIBU: Naam, mimi pia huandika nakala za michezo ya kuigiza.

SWALI: Unacheza ala yoyote ya muziki

JIBU: Mimi ni mchezaji wa gitaa.

SWALI:  Umefanya kolabo yoyote?

JIBU: Naam, nimefanya kolabo na wanamziki kama vile YODA, Alfaisal, Kalahari, Funzo Kuu, Cham na Onya.

SWALI: Ni nani anayekupa motisha zaidi maishani?

JIBU: Mwanamziki Tupac kanikosha mno kwa sababu nyimbo zake zinasawiri maisha halisi nan i taswira ya maisha halisi ya kila uchao.

SWALI: Ni msanii yupi ungelipenda kufanya kolabo naye na kwa nini?

JIBU: Ningependa kufanya kolabo na msanii Mejja. Ana ubunifu wa hali ya juu sana.

SWALI: Ni changamoto zipi unazokumbana nazo kama msanii?

JIBU: Changamoto kuu ni uthabiti kama msanii. Hii ni kwa kuwa wakati mwingine unaopaswa kuwa kwenye studio lakini unalazimika kutafuta riziki ili kujikimu kimaisha.

Tatizo lingine ni kwamba, ni watu wachache mno walio tayari kuwakubali wasanii wa mtindo wa Freestyle ikilinganishwa na walio na albamu.

Bila shaka changamoto lingine ni uhaba wa fedha ambapo ni sharti ujumuishe usanii na shughuli nyingine za kutafuta riziki.

SWALI: Ni tamasha gani za kisanii ulizoshiriki?

JIBU: Nimeshiriki tamasha mbalimbali mathjalan katika Sarakasi Dome, Power 254 na Hip hop Hookup Limuru.

SWALI: Kando na mziki, una shughuli nyingine yoyote ya kujikimu kimaisha?

JIBU: Ninamiliki duka la nguo lenye mitindo ya kisasa hasa miongoni mwa vijana.