http://www.swahilihub.com/image/view/-/4309092/medRes/1829884/-/d92r22/-/cyril.jpg

 

Afrika Kusini: Mahindi hukuzwa kwa wingi

Cyril Ramaphosa

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini. Picha/AFP 

Na SAMMY WAWERU na MASHIRIKA

Imepakiwa - Wednesday, May 16  2018 at  12:45

Kwa Muhtasari

Punje za mahindi huwa katika kigunzi na hupukutwa kabla ya kutumiwa kwa kuchanganya na maharagwe kupika pure au kusagwa kuwa unga.

 

MAHINDI ni aina ya nafaka inayosagwa kupata unga wa kupika ugali, na hata uji.

Punje zake huwa katika kigunzi na hupukutwa kabla ya kutumiwa kwa kuchanganya na maharagwe kupika pure au kusagwa kuwa unga.

Ugali ni mchanganyiko wa unga wa nafaka hiyo, maji yaliyotokota kisha ukaiva kiasi cha kulika kwa kuandamana na mboga, nyama au maziwa.

Pure ni chakula kilichoundwa kwa kuchanganya mahindi, maharagwe ama kunde.

Uji nao ni mchanganyiko wa unga na mahindi, japo mwepesi unaonywewa kwa kutia bidhaa kama sukari.

Nafaka hiyo pia huliwa kwa kuchomwa au kuchemshwa.

Afrika, mahindi yana walaji wengi Kenya ikiwa mojawapo. Afrika Kusini ndio mkuzaji mkuu wa mahindi Barani Afrika. Nchi hiyo imeorodheshwa ya 10 bora kote duniani katika kilimo cha mahindi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ya Mei 2017, Marekani inaongoza katika ukuzaji wa mahindi duniani ikifuatwa kwa karibu na China, Brazil, Ukraine na Argentina. Katika orodha hiyo ya 10 bora, nchi za Mexico, Indonesia na Ufaransa pia ziko.

Afrika Kusini ndio taifa la 10 katika kilimo cha mahindi duniani.

“Afrika Kusini huvuna karibu magunia tani milioni 15.5 za mahindi kila mwaka,” ikanukuu FAO.

Nafaka hiyo hasa hukuzwa Kaskazini na Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo. Mikoa ya Guateng, Kaskazini Magharibi, Mpumalanga, KwaZulu-Natal na Orange Free ndiyo inayokuza mahindi kwa wingi Afrika Kusini. Aidha nafaka hiyo hupandwa kati ya mwezi wa Septemba na Desemba, na kuvunwa Aprili hadi Juni.

Mwaka 2017 kwa sababu ya kupokea mvua chache, nchi hiyo ilivuna tani milioni 9.507 kutoka tani milioni 6.098 zilizovunwa 2016.

“Hiyo ilikuwa ongezeko la tani milioni 3.408,” ikaeleza ripoti ya FAO.

Wizara ya kilimo Afrika Kusini inapania kuuza zaidi ya tani 870,000 za mahindi meupe nje ya nchi hiyo kwenye mazao ya 2017/2018.

Ongezeko

Inasema huenda ikawa ongezeko la asilimia 48.1. Kufuatia mavuno ya 2016/2017, taifa hilo liliuza tani 587,423 ya mahindi hayo nje ya nchi.

Mahindi ya manjano yaliyouzwa nje ya Afrika Kusini baada ya mavuno ya 2016/2017, yalikuwa tani 438,879.

Aidha, Afrika Kusini inakadiria kuwa mavuno ya mahindi hayo 2017/2018 yatakayouzwa nje ya nchi hiyo huenda ikawa tani 1.31, hiyo ikiwa ni ongezeka la asilimia 198.49 kutoka mwaka 2017.

Mwaka wa 2015, taifa hilo lilishuhudia mvua ya masika yaliyosababisha uzalishaji wa mahindi kupungua. Zao hilo lilikuwa adimu, na kusababisha bei yake kupanda kiasi cha kuuzwa Randi 5,000 pesa za Afrika Kusini.

Kilimo nchini humo kimebuni nafasi ya ajira kwa zaidi ya watu 638,000.

Mbali na mahindi, Afrika Kusini pia hukuza kwa wingi matunda aina ya mizabibu, bizari (mbegu za ufuta), makonge, mtama, na wimbi.

Afrika Kusini ina ukubwa wa kilomita 1,219,912 mraba, na ekari milioni 1.3 hutumika kufanya kilimo cha unyunyiziaji maji mashamba.

Inakadiriwa kilimo cha mahindi nchini humo huendeshwa kwenye ekari kati ya milioni 1.91 hadi 2.43.  Asilimia 50 ya maji Afrika Kusini hutumika kufanya shughuli za kilimo.

Kilimo cha mahindi nchini humo kimestawi kutokana na kuimarika kwa mfumo wa kisasa wa kuendesha shughuli hiyo kama, kulima kwa matrekta, mashine za upanzi, kupalilia, kupulizia dawa na kuvuna. Kwa jumla, teknolojia ya kilimo Afrika Kusini imestawi, na kuwa na wataalamu waliobobea maswala ya kilimo.

Afrika Kusini ndio nchi kubwa ya Afrika ya Kusini na inayokadiriwa kuwa na zaidi ya watu milioni 54.

Aidha, imepakana na Namibia, Botswana, Zimbabwe, Msumbiji na Uswazi. Nchi nzima ya Lesotho iko ndani ya eneo la Afrika Kusini. Mji wake mkubwa ni Johannesburg.

Nchi hiyo ambayo ni koloni ya Waholanzi, ilipata rasmi uhuru wake 1994, kupitia mpiganiaji wake Marehemu Rais Nelson Mandela. Rais wake kwa sasa ni Bw Cyril Ramaphosa, aliyemrithi Jacob Zuma baada ya kujiuzulu Februari 2018 kwa kuhusishwa na sakata za ufisadi.