http://www.swahilihub.com/image/view/-/3517546/medRes/1534947/-/g7p9hez/-/saa.jpg

 

Ali Hassan Joho hupenda kujiita Sultani

Hassan Joho

Gavana wa Mombasa Hassan Joho aikashifu serikali ya Jubilee kuihangaisha aila yake kwa kutofautiana na Rais Uhuru Kenyatta Januari 13, 2017. Picha/WACHIRA MWANGI  

Na MWANGI MUIRURI na KABRASHA LA HISTORIA

Imepakiwa - Tuesday, June 12  2018 at  16:16

Kwa Muhtasari

Ali Hassan Joho ni mwanasiasa ambaye amejaliwa ujasiri wa kipekee.

 

GAVANA wa Mombasa, Ali Hassan Joho kwa madoido yake yote na mbwembwe za kupamba siasa zake hujitambulisha kama 'Gavana 01' na kwingine, Sultani.

Ni mwanasiasa ambaye amejaliwa ujasiri wa kipekee.

Mwaka 2017 alipapurana na Rais Uhuru Kenyatta eneo la Pwani katika kutoleana cheche.

Hata hivyo, amesema tangu kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga na Rais Kenyatta kunyoosheana mkono wa maridhiano katika kile kiliitwa handshake, Joho amesema kiongozi wa nchi "umekaribishwa Pwani".

Katika siasa zake za upinzani kwa Rais Kenyatta, Joho alikuwa akisisitiza kuwa alikuwa tayari kupoteza wadhifa wake, bora tu Rais Kenyatta asichaguliwe kwa awamu ya pili katika kura hiyo ya 2017.

Moto ulipozidi, Joho akaanza kuvizia hafla za rais eneo la Pwani na kujitokeza kumzomea hadharani kwa msingi wa kutenga eneo la Pwani.

Wasaidizi wa Rais nao wakijibu mipigo kupitia kumzuia Joho kufika katika hafla hizo, mara kwa mara akijipata amezuiliwa aidha nyumbani kwake au katika afisi yake hadi Rais aondoke Pwani kwa hiari.

Ni mwanasiasa ambaye alizaliwa Februari 26, 1976, na ambapo historia yake ya elimu kwa sasa ni utafsiri wa mahakama ambapo kumewasilishwa kesi ikipinga uhalali wake wa kielimu.

Licha ya utata huo, ana ufasaha wa lugha zote mbili zikiwa ni Kiswahili na Kingereza—lugha rasmi za taifa na afisi hapa nchini Kenya.

Mbunge wa Kisauni

Kabla ya kuingia afisini kama gavana mwaka wa 2013, Joho alikuwa mbunge wa Kisauni na pia alikuwa amehudumu kama naibu waziri katika serikali ya nusu mkate ya Mwai Kibaki.

Ni mkwasi ajabu ambapo ameorodheshwa kama mmoja wa wanaomiliki mali kwa kiwango cha maajabu, ambapo biashara zake ni nyingi zikijumuisha sekta za ujenzi, uchukuzi na gesi.

Huku siasa zake na rais Kenyatta zikichacha, rais alinukuliwa akimwambia Joho “ukome kunifuatafuata kiola mahali. Unanifuata kwani mimi ni bibi (mke) yako?"

Majibizano hayo yaliishia Kamishna wa Mombasa Evans Achoki kutoa onyo kali kwa Joho akimtaka aelewe kuwa “rais sio wa rika lako.”

Alikemea mtindo wa Joho wa “kutoa vitisho na makataa kwa Rais ukiwa na washirika wako.”

Malumbano hayo yanasemwa na wadadisi wa kisiasa kuwa yaliishia kumjenga pakubwa Joho kwa kuwa alionekana kuwa shujaa wa ujasiri na aliyekuwa akisaka kusimama na ukweli wake kwa kila hali akitetea mtu wa Pwani".

Baada ya kutwaa ushindi, Joho ametulia tuli na hasikiki katika siasa za malumbano au za kupingana na serikali, licha ya kuwa husemwa kama aliye na uwezo wa kurithi uongozi wa upinzani kutoka kwa Raila Odinga ambaye ndiye mshirika wake wa dhati kisiasa.

Hata hivyo, akiwa anajiandaa kujipanga upya kisiasa kwa msingi kuwa hatawania awamu nyingine ya ugavana kwa mujibu wa katiba inayomzima kwa awamu ya pili, Joho anasemwa kuwa yuko mawindoni ya kusaka kesho yake kisiasa, kutulia kwake kukisemwa kuwa hataki kujiweka nje ya Jubilee au nje ya upinzani, akidadisi atue wapi kwa mikakati yake ya baadaye.

Joho kwa sasa ni mume kwa Madina Joho na ambapo wamejaliwa watoto wanne.