http://www.swahilihub.com/image/view/-/4567902/medRes/1977051/-/dhwfx5/-/anzeki.jpg

 

Askofu Ndingi Mwana a'Nzeki amepoteza uwezo wa kukumbuka

Ndingi Mwana a'Nzeki

Askofu Mstaafu Ndingi Mwana a'Nzeki aomba Septemba 18, 2009, katika hafla moja Limuru. Picha/PHOEBE OKALL 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, May 18  2018 at  10:37

Kwa Muhtasari

Kiafya, Askofu Mstaafu Raphael Ndingi Mwana a’Nzeki ana Dementia, kumaanisha hana uwezo wa kukumbuka matukio mengi yake ya kimaisha.

 

WENGI katika imani ya Kikatoliki wanamkumbuka Askofu Raphael Ndingi Mwana a’Nzeki kwa hisia za upendo kufuatia msimamo wake wa dhati katika mkondo wa ukweli na haki, upendo na umohja kama nguzo muhimu za kijamii.

Kukutana kwa Swahilihub na askofu huyu Jumatatu nyumbani kwake chini ya uelekezi wa Askofu Benson Kuria hakukuwa na maana kubwa isipokuwa kumwona tu anaendelea kung’ang’ana na maisha.

Zama zile akiwa buheri wa afya, alikuwa akisuta kwa maneno makali unafiki wa kiuongozi na mwaka wa 1992 akiwa Askofu Nakuru, aliteta vikali kuwa kuwa kulikuwa na siasa za umwagikaji damu.

Alitumia jukwaa lake la uchungaji kukemea siasa za ukabila na upiganishaji wa jamii kwa msingi wa uhasama huo.

Alitoa habari za ujasusi kwa washirika wake kanisani kuhusu njama hizo, akitahadharisha kuwa hangekubali kuwa Askofu wa kushuhudia mauaji ya kikabila na mahangaiko ya Wakenya popote pale.

Anakumbukwa pia katika upande mwingine wa doa la huduma mwaka wa 2008 ambapo alichaguliwa katika kamati ya kuzima ghasia za baada ya uchaguzi na ambapo akiwa na wengine, wengi wao matapeli wa kiuchumi na kisiasa, walijipa marupurupu ya ulaghai katika harakati hizo yaliyozidi usaidizi waliotoa kutoka kwa bajeti iliyotolewa.

Tangu kamati hiyo ivunjwe, Ndingi mwana a'Nzeki kwa sasa akiwa na umri wa miaka 93 huishi maisha ya uzee mkuu wa kuathirika kiafya katika mtaa wa Lavington.

Alihudumu kwa miaka 25 katika Dayosisi ya Nakuru, kati ya 1971 na 1997.

Kinyume na hali yake ya awali akiwa mwingi wa nguvu za utumishi kwa Mungu, wakati alikuwa akikumbuka matukio kwa urahisi, leo hii amepoteza weledi huo na Swahilihub ilipata mambo kwa kiduchu tu.

Kukumbuka

Ameorodheshwa kimatibabu kama anayeugua kutokana na hali ijulikanayo kama Dementia, kumaanisha hana uwezo wa kukumbuka matukio mengi yake ya kimaisha.

Alizaliwa katika kijiji cha Masaku na ameorodheshwa kama waliojiunga na utumishi wa Kikatoliki kwa hiari ya mapenzi ya dhati ndani ya nafsi yake.

Kwa kawaida, usiuliaze kuhusu mke wake wala watoto wake kwa kuwa imani yake hii ya Kikatoliki katika uhalisi wake wa uzinduzi haikubalii mapadre kuoa wala kuweka mipango pembeni ili kujipa watoto, hali ambayo imekuwa ikizua ukaidi mkuu na mipasuko ndani ya imani hii.

Akiwa darasa la nane, alisajiliwa katika shule ya upadre ya Kiserian na mwaka wa 1961 akateuliwa kuwa mchungaji katika Kaunti ya Machakos.

Mwaka wa 1992 ambapo ghasia za kikabila Nakuru zilisababisha vifo vya watu 2,000, Ndingi akiwa katika ziara rasmi Marekani alirejea ghafla na akazindua misururu ya kukemea serikali na maafisa wote waliokuwa na uwajibikaji, akiwaita watumishi wa 'kishetani' na ambao moto wa Jahanamu ulikuwa unawangoja.