http://www.swahilihub.com/image/view/-/4929294/medRes/2220376/-/lx9kqsz/-/isack.jpg

 

Ataka vidhibiti mwendo magari ya Serikali

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe 

Na Tumaini Msowoya, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  14:42

Kwa Muhtasari

Wakati mwingine polisi huko barabarani wanatuheshimu sana lakini wakizidisha ndiyo tunaumia

 

 

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema ipo haja kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra) kufunga mfumo wa ufuatiliaji wa mwenendo wa mabasi (VTS) kwenye magari ya Serikali ili kudhibiti ajali.

Amesema mwaka jana kulikuwa na ajali nyingi zilizohusisha magari ya Serikali ambazo zilipoteza maisha ya baadhi ya watumishi wa umma wakiwamo vijana wadogo.

Tayari Sumatra imefanikiwa kufunga mfumo huo kwa zaidi ya mabasi 2,840 tangu ulipoanza kutumika kama majaribio mwaka 2016.

Kamwelwe alisema kuna umuhimu wa magari hayo kufungwa vifaa hivyo kama ilivyo kwa mabasi kwa sababu ajali nyingi zinasabishwa na mwendo kasi.

“Wakati mwingine polisi huko barabarani wanatuheshimu sana lakini wakizidisha ndiyo tunaumia, kuna umuhimu magari ya Serikali yafungwe vifaa hivi,” alisema Kamwelwe.

Kuhusu malalamiko ya utekelezaji wa sheria inayodhibiti uzito wa maroli iliyoanza kutumika Januari 1, mwaka huu, Kamwele alisema wanaolalamika hawakuwa wakihudhuria vikao.

Awali mkurugenzi mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema ufungwaji mfumo huo ni utekelezaji wa sheria inayotaka mabasi kufungwa vifaa vitakavyosaidia kutambua mwenendo wa gari.

Meneja wa mradi huo, Godfrey Msato alisema ni rahisi kufuatilia gari lolote lililofungwa mfumo huo na kupata taarifa sahihi.