http://www.swahilihub.com/image/view/-/4929370/medRes/2220425/-/s6l46e/-/aweso.jpg

 

Aweso aagiza vyeti vya wahandisi

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso 

Na Stella Ibengwe, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  15:36

Kwa Muhtasari

Ili kubaini uwezo wa kitaaluma katika ushauri, usimamizi na utekelezaji wa miradi

 

Shinyanga. Serikali imeagiza uhakiki wa vyeti vya kitaaluma vya wahandisi wa maji kote nchini ili kubaini uwezo wao kitaaluma katika ushauri, usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maji.

Agizo hilo lilitolewa juzi mjini Shinyanga na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi ya maji mkoani Shinyanga.

“Kuna wasiwasi kuhusu uwezo wa baadhi ya wataalamu na wahandisi wa maji kutokana na ushauri wao wanaotoa serikalini na kwenye miradi ya maji kushindwa kutatua tatizo la maji vijijini licha ya mamilioni ya fedha kutumika kutekeleza miradi hiyo, hasa uchimbaji wa visima.”

“Miradi ya maji vijijini imekosa usimamizi mzuri wa kitaalamu licha ya kila halmashauri kuwa na wahandisi wa maji; mfano hai kwa mkoa wa Shinyanga ni mradi wa maji katika kijiji cha Mwakitolyo na ule wa kisima kirefu katika kijiji cha Bubiki,” alisema Aweso.

Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema miradi ya maji ni kati ya huduma muhimu isiyo na mbadala kwa wananchi huku akitaja wilaya ya Kishapu kuwa miongoni mwa maeneo yenye changamoto kubwa kutokana na kutokuwa na mabwawa.

Kwa mujibu wa katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela, wakazi 900,000, sawa na asilimia 56 ya zaidi ya wakazi 1.7 milioni kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ndio wanaopata maji safi na salama mkoni humo.

Asilimia 52 ya watu hao wanahudumiwa na Mamlaka ya Maji wakati asilimia nyingine nne wanategemea vyanzo vya asili vya maji, mabwawa na viisma.