Azam Marine imeonyesha mfano wa uokoaji

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, April 5  2017 at  14:14

Kwa Mukhtasari

Tukio la juzi la msichana Hudhaimu Salum Abdarahaman kujirusha katika Bahari ya Hindi na baadaye kuokolewa na mabaharia wa Azam Marine  limetuma ujumbe kwa watumishi wa vyombo vya usafiri majini kwamba wanatakiwa kuwa tayari kwa dharura wakati wote.

 

TUKIO la juzi la msichana Hudhaimu Salum Abdarahaman kujirusha katika Bahari ya Hindi na baadaye kuokolewa na mabaharia wa Azam Marine  limetuma ujumbe kwa watumishi wa vyombo vya usafiri majini kwamba wanatakiwa kuwa tayari kwa dharura wakati wote.

Msihana huyo aliyekuwa safarini kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar akiongozana na wajomba zake alidaiwa kujirusha majini kwa sababu ambazo polisi wanazichunguza.

Si lengo la maoni haya kuzungumzia sababu za binti huyu kujitupa baharini wala iwapo alikuwa na lengo la kujiua au vinginevyo, hali kuangalia jinsi gani watumishi wa boti hiyo waliyojitokeza haraka na kufanikiwa kuokoa maisha yake.

Kulingana na taarifa zilizotolewa  na mashuhuda wa tukio hilo kupitia vyombo vya habari, binti huyo aliyekuwa akirudishwa nyumbani Unguja kwa nguvu kutokana na matatizo ya wazazi wake, aliwaomba wajomba zake kwenda kupunga upepo eneo la nje ya boti ndipo akachukua uamuzi wa kujirusha majini.

Kwa mtazamo wa haraka, hapo kuna udhaifu mkubwa katika suala la mtu ambaye anarudishwa nyumbani kwa nguvu kuachiwa peke yake akapunga upepo. Wajomba walitakiwa kuwa makini zaidi kumwangalia ili kuhakikisha anafika salama.

Hata hivyo pamoja na kasoro hiyo, wafanyakazi wa boti hiyo baada ya kupata taarifa au kusikia kelele kama ilivyodaiwa  walichukua uamuzi wa haraka kama wanavyotakiwa  kuhakikisha maisha ya binti aliyejirusha majini yanaokolewa.

Taarifa zilizopatikana ni kwamba  baada ya watumishi hao  kujiridhisha kuwa kuna mtu amejirusha majini walisimamisha boti wakashusha boti ndogo na kumfuata kwa kuogelea hadi wakamkuta akilea na kumuokoa, licha ya mtazamo wa watu wanaofahamu masuala ya kuogelea kuwa binti huyo alikuwa mtaalamu wa kuogelea kwa jinsi alivyokuwa akielea juu ya maji.

Ni nadra kusikia matukio kama hayo ya mtu kujirusha majini na maisha yao kuokolewa wakiwa hai ingawa matukio ya namna hiyo huwa yanaripotiwa  baada ya muda.

Pia wafanyakazi wengi kama si wote  wa vyombo vya majini hupata mafunzo ya umahiri katika kuogeleana uokoaji kinachotakiwa kujengwa ni  ari ya kujitolea kwa haraka na dharura.

Katika mazingira ambayo tumeyazoea ya ajali za majini ambazo zilikuwa zikisababisha vifo vya watu wengi kutokana na kukosekana kwa wataalamu wa uokoaji na vifaa vya kusaidia uokoaji isingedhaniwa kama si juhudi za watumishi hao wa Azam Marine, mtu akiyejirusha baharini ghafla bila kumtonya mtu yeyote angeweeza kupatikana haraka akiwa hai.

Kizungumkuti

Tukio hili lilikuja wakati katika kumbukumbu zetu yako matukio ya meli au boti kuzama ama baharini au kwenye maziwa lakini uokoaji ukawa kizungumkuti na watu wengi kupoteza maisha  kutokana na nchi yetu kutokuwa na wataalamu na vifaa vya uzamiaji.

Mathalan katika tukio la kuzama kwa meli ya MV Spice Islander iliyokuwa ikitoka Unguja kwenda Pemba mwaka 2011 baadhi ya watu waliokolewa na wengine hawakuonekana na hadi sasa  hakuna ripoti kamli inayothibitisha idadi ya wasafiri waliokuwamo  ukilinganisha na waliokufa na waliookolewa.

Pia Watazania hawajaondoa vichwani mwao ajali ya MV Buoba iliyotokea Mei 21, 1996 na kuua watu zaidi ya 800 katika Ziwa Victoria lakini idadi kubwa  ya abiria hawakuonekana.

Ni kutokana na hali hio ndiyo maana tunasema Azam Marine wameonyesha mfano unaoostahili kuigwa na vyombo vyote vya majini.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

Tanzania.