http://www.swahilihub.com/image/view/-/4706324/medRes/1353404/-/iaag68z/-/msangi.jpg

 

Baba mzazi ampiga mwanae hadi kufa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi  

Na Twalad Salum

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  10:45

Kwa Muhtasari

Alimpiga kwa mchi (mtwangio) sababu ya utoro

 

Misungwi. Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Sumbugu wilayani hapa Mkoa wa Mwanza, Mariamu Tabu amefariki kwa tuhuma za kupigwa na baba yake mzazi kwa kutohudhuria shule.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema mtuhumiwa anashikiliwa na polisi kituo cha Misungwi na atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

Mama mzazi wa binti huyo, Kija Mashauri alisema Agosti 6 mwaka huu mwanaye alikwenda shuleni lakini hakurudi nyumbani badala yake alirejea Agosti 7 jioni.

“Aliporudi baba yake alimuuliza alipokuwa na kuanza kumpiga kwa mchi (mtwangio), wakati akimpiga niliona kipigo hicho ni kikubwa nikaenda kuomba msaada kwa jirani ambaye ni mwenyekiti wa kijiji (Samweli Mtobela).

“Mume wangu alitaka kukimbia lakini walimkamata na kumpeleka mtoto zahanati ya Sumbugu kisha kituo cha afya cha Mbarika, wakiwa njiani wanakwenda mwanangu alifariki dunia,” alisema Mashauri.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mtobela alisema: “Tulimpeleka mtuhumiwa kituo cha polisi na kurudisha mwili nyumbani.”

Mwalimu mkuu msaidizi wa sekondari ya Sumbugu, Vincent Mugunga alisema Mariamu alikuwa kidato cha nne. Alisema kwa mujibu wa daftari la mahudhurio, hakufika shuleni tangu Julai 30 mwaka huu.

Alisema baba yake alifika shuleni hapo Agosti 6 kumuangalia lakini hakumkuta.