Bado wapinzani hawazitumii mahakama kudai haki zao

Imepakiwa - Wednesday, March 27  2019 at  09:12

 

Hakuna mwanasiasa wa upinzani aliyeisumbua Serikali mahakamani kama Mchungaji Christopher Mtikila. Miongoni mwa kesi za kikatiba alizowahi kuzifungua ni pamoja na ile ya kutaka wagombea binafsi kuruhusiwa katika mfumo wa uchaguzi.

Mchungaji Mtikila ambaye alifariki dunia Oktoba, 2015 kwa ajali ya gari huko Msolwa, Chalinze mkoani Pwani, ameacha alama ya mapambano kupitia mahakama jambo ambalo hata vyama vya upinzani vilivyopo vinaweza kuitumia mbinu hiyo.

Tangu vyama vingi viliporejeshwa mwaka 1992 na hatimaye uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo huo kufanyika 1995, ilionekana wazi kwamba CCM ndio iliyokuwa ikinufaika kutokana na kuwa na rasilimali fedha, miundombinu yakiwamo majengo, viwanja na mali nyinginezo ambazo vyama vya upinzani havikuwa nazo.

CCM pia ilinufaika kisheria kwani Rais ambaye ndiye mwenyekiti wa chama hicho ameendelea kuwa na madaraka makubwa ya kuteua viongozi wa Serikali wanaoratibu hata utendaji wa kila siku wa vyama vya siasa.

Rais anateua viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi na viongozi wa idara mbalimbali za Serikali.

Kama hiyo haitoshi anateua pia viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wakati yeye mwenyewe ni mgombea na chama chake kina wagombea tangu Serikali za Mitaa na wabunge.

Ni sawa na timu mbili zishindane, lakini mojawapo itoe mwamuzi wa mechi. Kwa jumla, ni mfumo ambao umekuwa ukilalamikiwa kwenye demokrasia.

Sasa katika mfumo kama huo na kwa kuwa Katiba bado inautambua kuwa wa demokrasia ya vyama vingi, vyama vya siasa vinaweza kudai haki ya usawa kisiasa.

Kwa muda mrefu, vyama vya upinzani vimekuwa vikikimbizana na uchaguzi, kuliko kudai haki ya usawa katika demokrasia. Ni mara chache tu vyama hivyo vimekuwa vikipambana mahakamani kudai haki ya kufanya siasa.

Bahati mbaya, siku zinavyokwenda mbele, ufanyaji wa siasa unazidi kuwa mgumu. Tumeona siku za karibuni vyama vikizuiwa kufanya mikutano na maandamano.

Hata ile mikutano ya ndani iliyoruhusiwa, sasa nayo inaingiliwa na viongozi wa upinzani na makada wao kukamatwa na kufunguliwa kesi.

Kwa mfano sasa, wabunge wa Chadema zaidi ya 10 wana kesi mahakamani, wawili (Joseph Mbilinyi, Sugu - Mbeya na Peter Lijualikali-Kilombero) wameshaonja jela na wengine wameshawekwa rumande kwa miezi kadhaa huku kesi zao zikiendelea.

Ni muhimu mbinu mbadala zitumike zisizovunja sheria za nchi na za kimataifa. Miongozi mwa mbinu hizo ni kuzitumia mahakama hizohizo kudai haki.

Inaonekana wapinzani wamekuwa wakisubiri kushtakiwa tu na kuishia kulalamika, lakini wao hawashtaki.

Kwa mfano, kuzuiwa kufanya mikutano na maandamano haiwezi kuwa kesi? Hata kama walishtaki wakashindwa, bado wangeendelea kusaka haki mahakamani.

Kuna kesi inayoendelea iliyofunguliwa na Bob Wangwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) akipinga wakurugenzi wa halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa niaba ya NEC.

Tayari Serikali imeshashindwa kwenye hatua ya awali baada ya pingamizi lake la kutaka kesi hiyo isisikilizwe kutupwa.

Kesi kama hizi ndizo zinaweza kuwasaidia kukosoa mifumo na uamuzi unaofanywa na viongozi au kudai haki za kikatiba.

Baadhi ya wanasheria wanasema hakuna linaloshindikana maana kila kitu kina mbinu na njia yake.

Kumekuwa na malalamiko kwamba zipo sheria zinazokwenda kinyume cha Katiba. Wasiishie kulalamika, hizo ni fursa kwa wapinzani kwenda mahakamani kuhoji.

Tatizo lipo kwa wapinzani kutoitumia fursa hii adhimu na hawawezi kuwa na kisingizio. Mara ngapi mahakama imewatendea haki wapinzani?

Ilitakiwa kila mbunge wa upinzani awe na kesi yake mahakamani wakidai hili na lile. Kwa kufanya hivyo, naamini kwamba sheria nyingi zingebadilishwa na mfumo wa vyama vingi ungebadilika.

Wanaweza kufanya hivyo siyo katika mahakama za ndani tu, kuna Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) na Mahakama ya Afrika, hayo yote ni mawanda mapana kwa wapinzani kudai haki zao.

Kwa sababu hizo, nadhani sio jambo jema kuishia kulalamika wakati sheria za nchi zimetoa fursa ya kudai haki ambayo wote tunaiamini kwamba inatimiza wajibu wake kwa watu wote.

0754 897 287