Bajeti itekelezwe kama itakavyopitishwa na Bunge

Na MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, June 9  2017 at  09:45

Kwa Mukhtasari

SERIKALI Alhamisi iliwasilisha bungeni bajeti yake ya mwaka 2017/18 ambayo ni ya pili tangu Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani.

 

Kama ilivyokuwa mwaka 2016/17, bajeti ya mwaka mpya wa fedha iliwasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango ikionyesha matumaini kwa Watanzania kwa kuwa imeelekeza fedha nyingi kwenye shughuli za maendeleo.

Miaka ya nyuma tulishuhudia fedha nyingi zikielekezwa katika matumizi ya kawaida lakini tangu Rais John Magufuli aingie madarakani kumekuwa na mabadiliko ambayo tunatumaini ni ya kuungwa mkono.

Kuwasilishwa kwa bajeti hiyo ni jambo moja. Bado kuna hatua nyingine zinazotakiwa kufuatwa za kuijadili, kuipitisha na kuitekeleza kwa jinsi ambavyo  itakuwa na matokeo chanya yaliyokusudiwa.

Ukiondoa vipengele vya utekelezaji na usimamizi wa bajeti ambavyo kwa miaka mingi vimekuwa na matatizo kadha wa kadha, maeneo ya mjadala wa Bunge na upitishaji wake hayatarajiwi kuwa na matatizo makubwa kutokana na utaratibu na mfumo uliopo.

Vilevile kwa hatua ambazo Serikali ya Magufuli imekuwa ikichukua katika usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma pamoja na udhibiti wa vitendo vya rushwa na ubadhirifu hapana shaka kuwa usimamizi a bajeti hii utafanyika kwa umakini mkubwa kwa lengo la kutimiza malengo yaliyowekwa.

Hata hivyo, kilio cha wananchi kimeendelea kusikika katika utekelezaji wa bajeti kwamba fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni kidogo zikiwa pungufu ya asilimia 50 ya fedha zilizopitishwa na Bunge.

Tumefuatilia mjadala wa bajeti za wizara mbalimbali tangu mkutano huu wa bajeti uanze na kubaini kuwapo kwa fedha nyingi zilizotengwa na Bunge kutopelekwa katika maeneo husika.

Pia kulikuwapo na malalamiko kwamba wakati mwingine Serikali iliamua kupeleka fedha maeneo tofauti na yale yaliyomo kwenye bajeti mambo ambayo hayatakiwi kwani sheria ya bajeti ni lazima iheshimiwe.

Vilevile pamoja na hatua zinazofanywa na Rais Magufuli, kilio cha muda mrefu katika eneo la matumizi na udhibiti wa fedha zinazoelekezwa kwenye shughuli za maendeleo zimeendelea kujitokeza katika Ripoti ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka uliopita.

Kama ilivyokuwa, ripoti ya CAG ya mwaka jana ilionyesha namna fedha za umma ama zilivyotafunwa au upungufu mwingine uliojitokeza katika utunzaji wa hesabu za fedha.

Miongoni mwa matatizo yaliyobainishwa ni kuhamisha fedha kutoka eneo zilikopangwa na kuzipeleka maeneo mengine  jambo ambalo limepgiwa kelele sana na wabunge.

Tunaamini kuwa bajeti iliyowasilishwa jana itapunguza vilio hivyo vya kila mara na kuweka misingi imara ya utekelezaji itakayolingana na vipaumbele vilivyoidhinishwa kwa kuheshimu uamuzi wa Bunge.

Kuamua vipaumbele vingine baada ya Bunge kupitisha bajeti ni  sawa na chombo hicho kutokuwa na umuhimu wowote wa kutumia fedha za walipa  kodi.

Pia watekelezaji wa bajeti hawana budi kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha  zilizotolewa ili zitumike kwa kadri zilivyokusudiwa badala ya kuishia kwa wajanja wachache na kuwaacha wananchi wakiendelea kuteseka.