http://www.swahilihub.com/image/view/-/4930290/medRes/716477/-/nhi8lw/-/balozi.jpg

 

Balozi Iddi aonya vurugu mapinduzi

Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi 

Na Muhammed Khamis, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, January 11  2019 at  10:28

Kwa Muhtasari

Mkorofi yeyote atakayeamua kujiingiza katika mtego atakiona cha mtema kuni

 

Pemba. Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi ameonya kwamba Serikali haitasita kumchukulia hatua kali mtu au kikundi cha watu watakaovuruga amani hususan katika kipindi hiki cha kuelekea Maadhimisho ya Miaka 55 ya Mapinduzi.

Amesema wamebaini kuna njama zimekuwa zikiandaliwa na baadhi ya watu za kutaka kuwafitinisha wananchi na Serikali yao na kuonya vyombo vya dola vipo macho havitavumilia vitendo hivyo.

Balozi Iddi alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kiuyu Minungwini mkoa wa Kaskazini Pemba jana, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kusheherekea miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964.

“Mkorofi yeyote atakayeamua kujiingiza katika mtego wa watu hao na ajaribu kama hakukiona cha mtema kuni,” alisema.

Balozi Iddi aliwataka Wazanzibar wenye mapenzi mema na nchi yao waendelee kulinda amani na mshikamano wa Taifa ili visiwa hivyo viendelee kuwa tulivu na kupiga hatua za haraka za maendeleo.

Awali, waziri wa nchi ofisi ya makamu wa pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed aliwataka wananchi kuendelea kuenzi mila na desturi zao.

“Wananchi wa Zanzibar ni mashuhuda wa maendeleo makubwa ikiwamo ya michezo yaliyofikiwa ndani ya miaka 55 ya Mapinduzi Matukufu,” alisema.

Baadhi ya wananchi wa shehia hiyo walisema kwenda kwa viongozi wa Serikali katika eneo hilo kunawafariji na kujihisi ni miongoni mwa watu muhimu katika nchi yao.