Bandarini bado panahitajika jicho la ziada

Na GAZETI LA MWANANCHI

Imepakiwa - Monday, December 4  2017 at  14:26

Kwa Muhtasari

Kutokana na idadi ya matukio yanayoibuliwa na  viongozi wakuu wa nchi wanapotembelea Bandari ya Dar es Salaam, tunaweza kusema kuwa kwa uhakika yamekuwa sugu na yanahitaji nguvu ya ziada.

 

Katika mlolongo wa matukio hayo, tangu Awamu ya Tano ilipoingia madarakani chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, ni hili la kutumia jina la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kujaribu kuingiza matrekta 48 bila kulipiwa kodi ndilo linalotisha zaidi.

Ni jambo la kupongeza kwamba matukio haya ya sasa yanafahamika kwa umma pengine bandarini kulikuwa kichaka kizito cha wafanyabiahsra kupitisha makontena na mizigo mingine kinyemela kwa miaka mingi.

Ni jambo la rahisi la kujiuliza kama katika miaka hii miwili tu  yamebainika matukio megi makubwa  likianzia na la kupitisha makontena kwa maelfu bila kulipiwa na kuondoka bila kuacha kumbukumbu zozote na mafuta kupakuliwa bila kutumia mita.

Hatujasahau pia kuwa hivi karibuni Rais Magufuli alibaini kuwepo kwa injini za treni zisizo na mwenyewe lakini zikiwa na nembo ya Shirika la Reli Tanzania. Pia wiki hii imebainika kuwa kulikuwepo na magari mengi yakiwemo ya polisi yaliyoingiza nchini kwa kutumia jina la Ofisi ya Rais.

Wakati vumbi la haya yote  halijatulia,  na wahusika hawajajulikana , limeibaki hili la matrekta ambalo walau lina watuhumiwa na hivyo kuna sehemu ya kuanzia.

Matukio haya yote yanaashiria kuwepo kwa mchezo unaoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam kwa muda mrefu na tayari ulikuwa umeota mizizi na kugeuka mchwa  sugu wa mapato ya Serikali.

Hii natupa shaka kwamba  hata kwa haya matukio machache, bado kuna vichaka vingi vya kumulikwa katika bandari hiyo na nyingine nchini kuhakikisha kuwa mchwa hao wanabainika na kuangamizwa.

Bila shaka wapo baadhi ya viongozi ambao wana tabia ya kutoa ‘vimemo’ kwa watendaji ili kuwasaidia. Mchezo wa namna hiyo hufanyika na wanatakiwa kutambua ujumbe wa Waziri Mkuu kwa viongozi wa bandari kwamba wafanye kazi kwa mijibu wa sheria na kutowasikiliza wafanyabiashara wanaodai kupewa vibali vya misamaha na viongozi wa juu serikalini.

Waziri Mkuu alitoa kauli kwamba,”Mtu asije hapa akasema kwamba amepewa kibali na Rais Magufuli , Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan au Waziri Mkuu cha kutaka kutoa mzigo wake bila ya kufuata taratibu,” alisema Waziri Mkuu.

Hatuna shaka kwamba kulingana na maagizo hayo, mtu yeyote atakayetumia majina ya wakubwa hata nje ya bandari atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. Vilevile kama kuna viongozi ambao bado wana ‘vimemo’ nao ujumbe utakuwa umewafikia.

Ni imani yetu kwamba kuanzia sasa havitakuwepo tena ‘vimemo’ vinavyodhaniwa kutoka kwa wakuu wa nchi. Vyombo vya ulinzi na usalama viendelee kubaini madudu ya ufisadi na rushwa na kulisafisha eneo hili ili kuhakikisha kuwa mapato ya Serikali yanakusanywa kama inavyotakiwa.