http://www.swahilihub.com/image/view/-/4928896/medRes/2220161/-/obmt20/-/salt+bae.jpg

 

Ben Pol kama Salah kwa Salt Bae

Nusret Gökçe ‘Salt Bae’ (kulia) akiwa na Ben Pol 

Na Charity James

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  11:39

Kwa Muhtasari

Ben Pol anatajwa kuwa Mtanzania wa kwanza kutia timu kwa Salt Bae.

 

MIAKA ya nyuma kama unatoka mkoani ama nje ya nchi kuja jijini Dar es Salaam, halafu una pigo za kijanja ni lazima utatia timu mitaa ya Posta pale Klabu Billcanas kupata burudani.

Ndio wajanja wa mjini wote walikuwa wakikutana pale, lakini kwa sasa ndio hivyo kuna mjengo wa maana unashuka na Billcanas imebaki stori tu.

Lakini, kwa sasa mambo yote ni Dubai kule Falme za Kiarabu ambako mastaa wa dunia na watu wazito, wenye pochi zao wanakwenda kula bata. Ndio! Kwa sasa mpango mzima ni Dubai tena kama unatia timu kisha ukashindwa kwenda kwenye mgahawa maarufu wa Nusr-Et, basi utakuwa huna cha kusimulia kabisa.

Achana na mgahawa huo unaomilikiwa na Nusret Gökçe maarufu Salt Bae, ambaye amejijengea umaarufu mkubwa kutokana na huduma yake, hasa kwa mastaa wa wakubwa wa soka duniani.

Staa gani wa soka unayemfahamu ambaye hajatia timu kwa Salt Bae? Romelu Lukaku, Paul Pogba, Lionel Messi, Ronaldo, Maradona, Luka Modric, Frank Ribery, Anthony Martial, Sergio Ramos, Luka Modric na David Beckham wote wametia timu na kula raha sana. Mgahawa huo una burudani kibao, lakini kubwa ni staili ya kuchoma na kukata nyama inayotumiwa na Salt Bae na ule unyunyizaji wa chumvi kwenye msosi huo ndio utapenda mwenyewe.

Ukiwa kwenye mgahawa huo, kuna wahudumu kibao lakini unapohudumiwa na Salt Bae mwenyewe unakuwa umepewa heshima ya aina yake.

Sasa iko hivi. Kwa hapa Bongo ni staa mmoja tu ambaye ametinga kwa Salt Bae na kula bata huku akihudumiwa na mzee mzima mwenyewe kisha kipande kimoja cha nyama kikashushwa kwenye kinywa chake na kuanza kutafuna kwa mapoziiii. Ndio, achana na Diamond Platnumz, AliKiba ama Mbwana Samatta, Ben Pol ndio anatajwa kuwa Mtanzania wa kwanza kutinga kwa Salt Bae.

Ben Pol, ambaye anatajwa kuibuka na mrembo matata mwenye pesa zake, wiki iliyopita alikuwa kwenye mapumziko yake kule Dubai na mara paap akazama kwa Salt Bae na kufanya yake. Kwa kifupi ni kwamba, Ben Paul ameingia kwenye anga za mastaa duniani waliotinga kwa Salt Bae akiwemo Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro.

Kuhusu Salt Bae

Amezaliwa mjini Erzurum, Uturuki akiwa mwenye asilia ya Kurdish. Familia yake ilikuwa na kipato cha kawaida huku baba yake akiwa mfanyakazi wa kwenye migodi. Akiwa darasa la sita tu, alilazimika kukatisha masomo na kwenda kufanya kazi kwenye duka la nyama (Bucha) katika eneo la Kadıköy, jijini Istanbul.

Baadaye mwaka 2007 hadi 2010, Salt Bae alizunguka kwenye nchi kadhaa ikiwemo Argentina na Marekani ambako alikuwa akifanya kazi kwenye hoteli kama mhudumu. Jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba, Salt Bae hakuwa akilipwa mshahara kwani, alikuwa akifanya kazi kwa kujitolea ili kupata uzoefu kwenye kazi hiyo.

Mwaka 2010, Salt Bae alirejea kwao Uturuki baada ya kukusanya maujuzi kisha akatia timu Dubai na mwaka 2014 alifungua mgahawa wake wa kwanza. Ndani ya mgahawa huo alikuwa na wafanyakazi wachache huku mwenyewe akiwa mstari wa mbele kuhakikisha kila idara iko vizuri.