http://www.swahilihub.com/image/view/-/4611958/medRes/2008579/-/a0lv6fz/-/mbuzi.jpg

 

Biashara ya mbuzi yapasua vichwa

Mbuzi wakiwa mnadani 

Na Ngollo John

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  12:41

Kwa Muhtasari

Ongezeko la ushuru na uchache wa wateja kumepunguza hata idadi ya mbuzi

 

Mwanza. Imezoeleka kuwa biashara ya mbuzi na bidhaa nyingine za vyakula hushamiri kila inapokaribia siku za sikukuu za kidini lakini kipindi hiki cha kuelekea Idd-el Fitri hali imekuwa tofauti kwa kuwa hakuna wateja.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara kwenye mnada huo, David Mashigala alisema jana kuwa licha ya uhaba wa wateja, biashara pia imedorora kutokana na uchache wa mbuzi na kondoo kutoka wafugaji wa vijijini.

“Wafugaji na wananchi huku vijijini hawauzi mifugo yao kwa sababu hawana shida kutokana na kuvuna mpunga, mahindi na pamba; mbuzi na kondoo wameadimika; hivyo kumesababisha bei pia kupanda kwa kati ya Sh10,000 hadi Sh15,000 kutegemeana na ubora na ukubwa wa mbuzi na kondoo,” alisema Mashighala.

Pamoja na kuadimika kwa mbuzi kutoka kwa wafugaji huko vijijini, Mashighala anataja ongezeko la ushuru kutoka Sh4,000 ya awali hadi Sh6,500 hali iliyosababisha kupanda kwa bei ya mifugo.

“Awali tulilipa Sh2,000 hapa mnadani na Sh2,000 nyingine machinjioni; lakini hivi sasa tumeongezewa ushuru wa Sh2,500 kwa ajili ya mnada wa Nyamatara; Wilaya ya Misungwi tunakotakiwa kuhamia,” alisema Mashighala.

Ongezeko la ushuru na uchache wa wateja kumepunguza hata idadi ya mbuzi wanaouzwa mnadani hapo kwa siku kutoka zaidi ya mbuzi 25 hadi kufikia 10 pekee kwa siku.

Mmoja wa wafanyabiashara, John Mahengere alisema mbuzi ambaye awali aliuzwa kwa Sh30,000 hadi 35,000 hivi sasa anauzwa kati ya Sh40,000 hadi 45,000.

Alisema mbuzi waliokuwa wakiuzwa kati ya Sh60,000 hadi Sh80,000 wiki mbili zilizopita hivi sasa wanauzwa kati ya Sh100,000 hadi Sh120,000.