http://www.swahilihub.com/image/view/-/5057738/medRes/2303178/-/wsn8yk/-/uchambuzi+05+pic.jpg

 

Bila umeme wa uhakika viwanda havitakuwa na maana

Na Anthony Mayunga

Imepakiwa - Friday, April 5  2019 at  09:34

 

Machi 19 mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alimkabidhi mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima cheti cha ushindi wa nafasi ya pili kwa mikoa ya Tanzania Bara kwa kuanzisha viwanda vidogo vingi.

Katika kikao cha tathmini ya kitaifa ya kufuatilia utekelezaji wa mpango wa uanzishaji wa viwanda 100 kwa kila mkoa, ilibainika mkoa huo umefanikiwa kuanzisha viwanda vidogo 377.

Viwanda hivyo licha ya kuwa vidogo vinatengeneza ajira hata kama ni za muda mfupi, huku vikikuza uchumi wa familia, wilaya na Taifa.

Kutokana na mafaniko hayo, wanastahili kupongezwa wakiwamo waliohamasisha, kushauri, kusaidia na usimamizi wa utekelezaji.

Hadi mwisho wa mwaka huu, viwanda hivyo vidogo vinaweza kuongezeka kwa kuzingatia fursa na malighafi zinavyopatikana.

Licha ya kuwapo viwanda hivyo, naamini nishati ya umeme inahitajika katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku ili wamiliki wakue na kuanzisha viwanda vya kati na hatimaye vikubwa.

Hata hivyo, juhudi hizo za kuifanya Mara ibaki imara kiviwanda hazitazaa matokeo mazuri kama tatizo la umeme halitafanyiwa kazi kwa ufanisi.

Huenda kasi ya kuporomoka ikawa kubwa zaidi kuliko kuanzishwa kutokana na tatizo la umeme, maana kwa hali ilivyo sasa wapo watakaoshindwa kulipa mikopo waliyochukua kuanzisha viwanda kwa sababu ya kushuka kwa uzalishaji unaochangiwa na tatizo la umeme.

Kama tusipozingatia ubora katika kusambaza umeme, mikakati ya kuelekea uchumi wa kati katika Taifa linalojitegemea, itabaki kwenye makaratasi.

Umeme kwa siku unakatika zaidi ya mara saba, tatizo ambalo limedumu kwa zaidi ya wiki mbili katika mazingira hayo waliokopa mitaji watarejesha kwa uzalishaji gani?

Athari za kutokuwa na umeme wa uhakika hadi sasa waathirika ni watumiaji wote hata wale ambao wamefungiwa kwenye nyumba za tembe.

Pia, suala la kukatika umeme linachangia gharama kubwa kwa watumiaji ikiwamo majenereta ili kuendesha shughuli zao za kila siku kwa gharama zile zile.

Kwa wamiliki wa baa, migahawa na nyumba za kulala wageni, vinyozi, wafyatua tofali, wachomeleaji, wauza juisi zisizokuwa na jenereta wanakimbiwa na wateja chanzo kikiwa ni kutokuwapo kwa uhakika wa umeme, lakini kodi za Serikali na wenye nyumba ziko palepale.

Pamoja na hali hiyo, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani Mara halitoi taarifa yoyote kutokana na adha hiyo.

Matokeo yake wananchi wanajiandaa kusaka aina nyingine za nishati watakazotumia hasa usiku. Kuna haja ya kuangalia upya utendaji wa Tanesco wenye ufanisi.

Mwaka jana waziri mwenye dhamana alitoa tamko kuwa umeme ukikatika siku za sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya meneja wa mkoa huo hana kazi, lakini hajawahi kutoa mrejesho wa tamko hilo.

Ni kweli Serikali inajivunia kuweka umeme hadi nyumba za tembe, lakini haijajikita kushughulikia huduma zinazotolewa kama zinakwenda sambamba na mkakati wa nchi wa kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda.

Umeme ni uchumi bila kuweka mikakati mizuri watu wengi walioanzisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa badala ya kutengeneza faida watapata hasara na waliokopa mali zao zitaishia kuuzwa.

Hata hao wenye nyumba za tembe hautawahamasisha kuboresha makazi kwa kuwa hawataona tofauti kabla na baada ya kuweka umeme, maana wanalazimika kutumia vibatari na taa za chemli.

Kama hakutafanyika maboresho ambayo yatahimili kasi ya uanzishwaji wa viwanda na shughuli nyingine zinazotegemea nishati hiyo ya uhakika, kuna hatari ya kuweka historia ya kuanzisha viwanda vingi ambavyo havitakuwa na tija kwa Taifa.

Anthony Mayunga ni mwandishi wa Mwananchi wilayani Serengeti anapatikana kwa simu namba 0787- 239480