Bima ya mazao ni mkombozi kwa wakulima nchini

Imepakiwa - Monday, May 20  2019 at  10:26

 

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameliambia Bunge kwamba wizara yake kwa kushirikiana na wadau imeanza mchakato wa bima ya mazao utakaosaidia wakulima kukabiliana na hasara inayotokana na majanga kama vile ukame, mafuriko, magonjwa na wadudu waharibifu.

Hasunga alisema katika kukabiliana na changamoto hizo, nchi nyingi duniani zimeanzisha na kutekeleza mfumo wa bima za mazao ambazo humwezesha mkulima kulipwa fidia anapopata hasara na pia kumwezesha kupata mkopo kutoka taasisi za fedha kwa urahisi.

Alisema tayari wizara imeshafanya vikao na wadau kwa ajili ya maandalizi ya awali ya kuanzisha utaratibu wa Bima ya Mazao ili waanze na baadhi ya mazao na maeneo machache.

Pia, alisema ili utaratibu uwezekane, kutahitajika takwimu sahihi za hali ya hewa pamoja na uzingatiaji wa kanuni bora za kilimo.

Hivyo, kunahitajika ushirikiano wa karibu na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) pamoja na maofisa ugani kutimiza wajibu wao kikamilifu.

Hii ni habari njema kwa Taifa kwa kuwa sekta ya kilimo inabeba zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanaotegemea ajira kupitia kilimo kama uti wa mgongo kwa Taifa.

Lakini, Tanzania ina wakulima wa aina mbili, wakubwa wanaotumia vifaa vya kisasa katika kilimo pia kuna wakulima wanaotumia jembe la mkono ambao ndio wengi.

Tunaamini mpango huu wa bima ya mazao utawalenga wote, hakutakuwa na ubaguzi kama Waziri alivyoliambia Bunge kwamba suala la bima ya mazao litawezekana kwa maofisa ugani kutimiza wajibu wao kikamilifu.

Rai yetu kwa maofisa ugani watekeleze wajibu wao ili bima hiyo iweze kuwanufaisha wakulima wote hasa wadogo. Tunajua Serikali imekuwa na nia njema kwa wakulima ndio maana imekuwa ikiajiri kwa wingi maofisa ugani.

Takwimu zilizowahi kutolewa bungeni na naibu waziri wa kilimo, mifugo na uvuvi Septemba 2017, William ole Nasha, alionyesha kuwa Serikali hadi kufikia mwaka wa fedha wa 2016/2017 ilikuwa imeajiri maofisa ugani 8,756 sawa na asilimia 43 ya mahitaji ya maofisa ugani 20,374 katika ngazi ya kijiji, kata na wilaya.

Nchi yetu siku zote inasisitiza kuleta mapinduzi ya kilimo ikiwamo kuondoa tozo zilizokuwa kero kwenye sekta hiyo, hivyo ujio wa bima ya mazao ni mkakati mwingine wa mapinduzi katika sekta ya kilimo.

Mkakati huu ambao umepangwa kuanza mwaka 2019/20 ni vema wakulima nao wakaandaliwa kwa kupewa elimu kuhusu umuhimu wa bima ya mazao, faida zake na namna ya kujiunga.

Tunadhani kusubiri hadi hatua za mwisho ndio elimu ianze kutolewa hatutafanikiwa, ni vizuri maandalizi yakaanza mapema kwa maofisa ugani kuanza kutoa elimu hiyo kwenye maeneo yao ya kazi.

Pia, TMA kama alivyoeleza Waziri Hasunga kwamba wanatakiwa kutoa takwimu sahihi za hali ya hewa ili wakulima wajue ni wakati gani wa maandalizi ya kilimo badala ya kusubiri ‘bahati nasibu’ ya mvua.

Mbali na maandalizi, TMA wanapaswa nao kujipanga jinsi watakavyofikisha taarifa za hali ya hewa hasa katika kilimo kwa wakulima. Ni vizuri TMA katika taarifa zao wakaweka wazi kuwa ni mvua zipi zinafaa kwa kilimo na zipi hazifai.

Tunaamini mkakati huu umekuja wakati mwafaka ambao kilimo kinahitajika sana kwa kuwa Taifa letu limeendelea kupiga hatua za maendeleo ili kufikia uchumi wa viwanda.

Rai yetu kwa wizara maandalizi yao yaendane na maandalizi kwa wakulima hasa wale wadogo. Na tungependa suala hili lisiwe la kisiasa, lifanyike.