Bomba la mafuta ni letu tulilinde sote

Na GAZETI LA MWANANCHI

Imepakiwa - Monday, August 7  2017 at  12:30

Kwa Mukhtasari

JUZI Rais John Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni walizindua mradi wa ujenzi wa mafuta kutoka Hoima Uganda hadi Bandari ya Tanga.

 

Bomba hili lenye urefu wa kilomitta1,149 kwa upande wa Tanzania litapita katika mikoa minane na wilaya 24, wakati kwa upande wa Uganda litakuwa na urefu wkilomita  296 kwenye wilaya nane.

Kwa hapa nchini, bomba litapita katika Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida ,Dodoma , Manyara na Tanga.

Katika hafla ya kuweka jiwe la msingi iliyofanyika juzi katika eneo la Chongoleani mkoani Tanga,  Rais Magufuli alisisitiza umuhimu wa bomba hilo na akafafanua kwa urefu  jinsi ilivyokuwa vigumu wa bomba hilo kufikia uamuzi wa kulijenga kupitia Tanzania kuliko Kenya. Aliongeza kuwa kulikuwa na ushindani mkubwa ulikuwapo kati ya nchi hizo mbili.

Kwa mujibu ya Rais Magufuli, katika mazungumzo na Uganda  walikubaliana kwamba Tanzania  itapata dola  za Marekani 12.5 kwa kila pipa litakalosafirishwa  kupitia bomba hilo ambalo kwa kuanzia litakuwa likisafirisha mapipa 216,000 kwa mwaka.

Vilevile Uganda  ambayo wataalamu wake walitumika kwa kiwango kikubwa  kugundua mafuta hayo itatoa wataalamu wake kufanya uchunguzi katika maziwa ya Tanganyika na Eyasi na  endapo yatapatikana mafuta pia yatasafirishwa kupitia bomba hilo.

Kana kwamba haitoshi, Rais Magufuli alimweleza Rais Museveni kuwa akitaka kupata gesi asilia kutoka Mtwara, Tanzania kwenda Uganda na itasafirishwa kupitia njia ile ile na hivyo alimhakikishia ulinzi wa bomba hilo litakalohusisha askari 1,115.

Pamoja na kuwapo kwa askari hao, sisi tunaami kuwa wananchi wote, wale wanaoishi karibu na eneo linakopita  na wengine wengine kwa jumla, kwa kuwa hili ni bomba la Watanzania wote, manufaa yake yatakakuwa kwa ajili yetu sote.

Ni kutokana na umuhimu huo, sisi tunaami Watanzania wanatakiwa kulitazama kama fursa muhimu ya kiuchumi kwa manufaa ya mtu mmoja mmoja na ya taifa kwa jumla.

Vivyo hivyo Watanzania wanatakiwa kujipanga kutumia fursa mbalimbali zitokanazo na mradi  huo kwa sasa  wakati wa ujenzi na hata baada ya ujenzi wa mradi kukamilika.

Mathalan mbali na ajira wakati wa ujenzi na ulinzi, wananchi wanatakiwa kuuza huduma kama za chakula, matunda, vinywaji, matibabu, usafiriishaji, vifaa vya ujenzi  kwa makandarasi na wafanyakazi wao.

Pia kampuni mbalimbali za ujenzi na uhandisi zinatakiwa kutazama mapema jinsi gani zitahusika na kunufaika na mradi huo  mkubwa wa dola za Marekani 3.5 milioni sawa na Sh8 trilioni.

Kamwe hatutarajii kuona vibweka vyovyote vya kuukwamisha mradi huu lakini kama kuna watu wanaostahili fidia zozote kabla hawajapisha mradi huo  walipwe bila vikwazo vyovyote.

Vilevile hatutarajii kuona watu ambao  wanataka kujenga nyumba au kuwa na miradi mingine  kwenye eneo la mradi ili kutega fidia.