http://www.swahilihub.com/image/view/-/5116244/medRes/2344199/-/1lyyubz/-/boresha+pic.jpg

 

Boresha mnada wa Dakawa kuongeza mapato

Na Mwandishi wetu

Imepakiwa - Wednesday, May 15  2019 at  13:21

 

Eneo la mnada wa ng’ombe, mbuzi na kondoo wa Dakawa ni maarufu kwa kuwa watu wa kada tofauti wakiwamo viongozi wa Serikali wamekuwa wakienda kwa ajili ya kununua mifugo na hata kula nyama na kupata vinywaji mbalimbali.

Umaarufu wa mnada huu ambao hufanywa kila Ijumaa unachangiwa na kuwapo wataalamu wa kuchoma nyama kutoka jamii za Kimasai na Kigogo, ukiwa kando ya barabara kuu ya Morogoro – Dodoma ambayo watu wengi wakiwemo viongozi hupita.

Mbali na mnada huo kuwa wa ng’ombe, mbuzi na kondoo pia vitu mbalimbali vinauzwa vikiwamo vinywaji, nguo na bidhaa zinazotokana na mazao ya mifugo.

Pamoja na umaarufu wa mnada huu, bado mazingira yake hayaridhishi kutokana na kuwapo tope hasa nyakati za mvua lakini pia huduma ya maji na vyoo hailingani na hadhi na wingi wa watu wanaokwenda pale.

Mabanda mengi ya wachoma nyama yameezekwa kwa nyasi lakini pia majiko yanayotumiwa ni ya kuni, hivyo kumekuwa na moshi mzito unaozunguka kwenye mabanda haya jambo ambalo ni kero.

Baya zaidi, wachoma nyama wengi hawana sahani za kuwawekea nyama wateja na hivyo kutumia mifuko ya plastiki maarufu kama rambo ambayo huchanwa na kugeuzwa sahani jambo, ambalo ni hatari kwa afya itakuwa balaa zaidi ukomo wa mifuko hiyo utakapofika Mei 31, mwaka huu.

Hata ulinzi si wa kuridhisha hasa ukizingatia wafanyabiashara wamekuwa wakifika kwenye mnada huu, wakiwa na fedha nyingi kwa ajili ya kununua mifugo, hivyo ni vema ukawekwa utaratibu mzuri wa kuwa na askari wa kutosha ili mnada huu uwe salama.

Naamini Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, wasimamizi wa mnada huu wamekuwa wakikusanya sehemu ya mapato ya mnada huu hivyo ni lazima waboreshe mazingira, miundombinu na kusimamia suala la usafi na usalama ili waweze kukusanya mapato makubwa.

Katika kuboresha miundombinu hiyo, ni vema halmashauri ikaongeza idadi ya vyoo, kuchimba kisima na kuweka matanki ya kutosha ya maji badala ya kutegemea bomba moja ambalo halitoshelezi mahitaji na wingi wa watu.

Suala jingine halmashauri inapaswa kumwaga vifusi na kufukia mashimo kwenye madimbwi ya maji ya mvua na kutoa maelekezo kwa wafanyabiashara ya kuboresha mabanda ili yaweze kuezekwa kwa bati na kuwa imara badala ya nyasi.

Pia wafanyabiashara wanapaswa kutumia sahani na majiko ya kisasa ya kuchoma nyama na kuhifadhi kitoweo hicho wakati ikisubiri wateja, tofauti na ilivyo kwa sasa ambapo wamekuwa wakitumia majiko ya kuni, kutundika nyama kwenye miti na kutumia mifuko ya plastiki kama sahani.

Ikiwa mazingira ya mnada huu yataboreshwa naamini wafanyabiashara wengi watapeleka bidhaa na wateja wataongezeka na hivyo halmashauri ya wilaya ya Mvomero itakusanya mapato ya kutosha yatakayosaidia kwenye shughuli nyingine za maendeleo.

Si tu kwa mnada huu lakini pia minada mingine kama hii inapaswa kuboreshwa kwa kuwa watu wengi wanaonekana kuvutika kwenda si tu kwa ajili ya kununua mifugo lakini pia kwa ajili ya kuburudisha kwa nyama choma na vinywaji.

Ijapokuwa baadhi ya watu wanadai kuwa mazingira yaliyopo sasa ndio kivutio kikubwa na kwamba yatakapoboreshwa yanaondoa mvuto kwangu, mimi naona si kweli kwa kuwa yapo baadhi ya maeneo kwenye miji mbalimbali hapa nchini yanayochomwa nyama ambayo yameboreshwa na bado watu wamekuwa wakienda kwa wingi.

ladyhamida@yahoo.com

0715681287