Bunge la Bajeti ni muhimu kwa wananchi

Imepakiwa - Wednesday, April 3  2019 at  08:21

 

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeanza vikao vyake jijini Dodoma jana likiwa na ajenda mbalimbali zinazolenga mustakabali wa maisha ya Watanzania, lakini kubwa ikiwa ni kujadili na kupitisha bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2019/20.

Mkutano huo wa 15 utakaomalizika Juni 28 pia utajadili utekelezaji wa bajeti za wizara kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali ya mwaka 2019/20.

Pia, Bunge litajadili hotuba ya hali ya uchumi wa Taifa na kupitisha miswada miwili ya sheria ambayo itasomwa kwa hatua zake zote ukiwamo ule wa Sheria ya Fedha za Matumizi wa mwaka 2019 na wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019.

Katika yote ni kuwa Bunge hili ndilo kubwa ambalo limebeba mustakabali wa maisha ya kila siku ya wananchi kutokana na mambo ambayo huwa yanajadiliwa wakati wa bajeti.

Wakati tukilitakia majadiliano mema yanayotakiwa kuongozwa na hekima na busara za wawakilishi hao wa wananchi, ni matarajio yetu kwamba mambo muhimu kama kero na vilio vikubwa vya wananchi katika maisha yao, yatazingatiwa.

Tunatarajia kwamba wabunge, mawaziri na hata wenyeviti, Spika na wasaidizi wake watasimamia vyema miongozo waliyojiwekea kupitia kanuni na sheria mama, ambayo ni Katiba ya nchi, kufanikisha shughuli za Bunge, ingawa kubwa tunalolitarajia ni busara na hekima kutawala.

Kwa upande mwingine, umuhimu wa Bunge hili unatazamwa na kila mtu. Kila Mtanzania katika eneo lake la uzalishaji na maisha anasubiri kujua nini kitakachoibuka, kujadiliwa na kupitishwa ndani ya Bunge.

Wafanyabiashara wanataka kujua masuala ya kodi na unafuu watakaoupata katika utekelezaji wa majukumu yao, wakulima watahitaji kufahamu pembejeo na utaratibu utakaotumika kuzipata kwa urahisi, wavuvi wanataka kujua kipi kitakachojadiliwa katika sekta yao, walimu na watu wa kada nyinginezo nao wanatega sikio katika maeneo yao.

Ni kutokana na umuhimu huo, macho na masikio ya Watanzania yameelekezwa Dodoma kufuatilia kinachoendelea. Hata hivyo, ufuatiliaji wao unaweza kuwa mzuri zaidi iwapo wataona na kusikia moja kwa moja majadiliano hayo, yaani kutangazwa moja kwa moja na vituo vya redio na televisheni.

Tunasema hivyo tukiamini kwamba majadiliano ya wazi kuhusu bajeti yanayofuatiliwa vyema na wananchi kupitia runinga juu ya mustakabali wa maisha yao ndiyo shauku yao na hasa kwa kuwa yatakuwa yanagusa maisha wanayoishi au wanayotarajia kuyaishi baada ya Bunge hilo.

Bunge likionyeshwa mubashara, mathalan pale bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara itakapokuwa inajadiliwa, itakuwa ni fursa nzuri kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa viwanda kujua mambo gani watapaswa kuyazingatia na kuyapa kipaumbele katika shughuli zao.

Aidha, iwapo kutakuwa na mabadiliko yoyote ya kisera au kikodi, watakuwa wamehabarishwa haraka kupitia runinga na kuanza kujipanga vipi watakavyotimiza wajibu wao. Dunia inavyokwenda kwa kasi, watu hawapaswi kusubiri habari zichapishwe baadaye ndipo watimize wajibu wao.

Isitoshe, nguvu kubwa ya mubashara inasaidia kujenga mijadala ya wananchi na hivyo kuiweka hai hoja husika katika mioyo ya wananchi.

Ni matumaini yetu kwamba hili litazingatiwa ili kuwapa fursa Watanzania kufuatilia jinsi mgawanyo wa keki ya Taifa unavyofanyika na hivyo kuwa tayari kufanya shughuli zao kwa kadiri ilivyoamuliwa na wawakilishi wao.