http://www.swahilihub.com/image/view/-/4885690/medRes/2191604/-/10wpkcv/-/mjiji.jpg

 

Mji wa Busia kupata sura mpya baada ya kupokea ufadhili wa Sh110m kutoka Benki ya Dunia

Busia

Mwanamke apita karibu na shimo kubwa katikati mwa mji wa Busia kwenye barabara kuu ya Busia-Kisumu Novemba 15, 2018. Gavana Sospeter Ojaamong amefichua kuwa serikali yake imepokea Sh110 milioni kwa ajili ya kuimarisha miundombinu mjini humo. Picha/GAITANO PESSA 

Na GAITANO PESSA

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  15:22

Kwa Muhtasari

Ufadhili huu utasaidia kuimarisha mji wa Busia.

 

BUSIA, Kenya

MJI wa Busia utanufaika kutokana na ufadhili wa Sh110 milioni kila mwaka kutoka kwa Benki ya Dunia baada ya kuingia katika kategoria au kiwango cha kuitwa manispaa, Gavana Sospeter Ojaamong amesema.

Hatua hii inajiri mwezi mmoja tu baada ya bunge la kaunti hiyo kupitisha mswada wa kupandisha mji huo hadi kiwango cha Manispaa kwa mujibu wa kipengee nambari 8 (I) kinachosimamia miji maarufu kama The Urban Areas and Cities Act.

Gavana huyo amefichua kuwa tayari serikali yake imepokea donge la kwanza la fedha hizo ambazo matumizi yake yanatuwama katika uimarishaji miundombinu katika mji huo.

“Wakazi wamekuwa wakilalamika kuwa mji wetu wa Busia umetelekezwa na serikali yangu lakini sasa tuna fedha zaidi ya Sh110m kuimariasha Busia,” alisema Ojaamong.

Matukio haya yana maana kuwa mji huo sasa unajiunga na mingine mingi katika mbio za kupata ufadhili kutoka kwa mpango wa kuimarisha miji wa Kenya Urban Support Programme ambao huhusisha ujenzi wa taa za miji, ufadhili wa vifaa vya zimamoto, mabomba ya majitaka, uimarishaji wa makazi hasa mitaa ya mabanda, masoko na vituo vya mabasi.

Wakazi wa Busia wamekuwa wakilalamikia hali duni ya mji huo wa mpakani hasa wakati wa mvua ambapo shughuli za uchukuzi hutatizika.