CECAFA itathmini mfumo wa mashindano yake

 

Imepakiwa - Monday, July 2  2018 at  11:28

 

Michuano ya Kombe la Kagame imeanza mwishoni mwa wiki iliyopita na inafanyika kwenye Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Chamazi Complex nao unaotumiwa.

Michuano hiyo inafanyika baada ya kukosekana kwa miaka miwili, tangu ilipochezwa mara ya mwisho mwaka 2015.

Klabu za Simba, Azam na Singida United zinaiwakilisha Tanzania Bara wakati Zanzibar inawakilishwa na JKU.

Tunachukua nafasi hii kulipongeza Baraza la Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa kufanikiwa kurejesha michuano hiyo mikongwe barani Afrika.

Michuano hiyo pamoja na ile ya timu za taifa, Kombe la Chalenji, imekuwa ikikabiliwa na matatizo makubwa ya uendeshaji kutokana na kukosekana kwa wadhamini na hivyo kuifanya Cecafa kushindwa kugharimia mambo muhimu.

Mara kadhaa Tanzania Bara imekuwa ikinusuru mashindano hayo kutokana na mtaji mkubwa ilionao wa wanazi wa soka, ambao uingiaji wao viwanjani huiwezesha Cecafa kupata fedha za angalau kumudu gharama muhimu kama za malazi ya timu, waamuzi na maofisa wengine.

Wakati mwingine, viongozi wakuu wa nchi kama Rwanda, Ethiopia na Sudan wamekuwa wakisaidia uendeshaji kutokana na Serikali zao kukubali kulipia baadhi ya gharama za uendeshaji.

Kwa hiyo, Cecafa ina changamoto kubwa ya kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanakuwa na ufanisi kwa kupata wadhamini wa uhakika na pia kuwa na uwezo wa kuuza haki za televisheni ili kujipatia uwezo wa kifedha.

Kwa miaka miwili, Cecafa imekuwa ikishindwa kupata wadhamini wa uhakika na wakati mwingine hata nchi zinazoomba kuandaa kujitoa katika dakika za mwisho na hivyo kusababisha mashindano kukosa mwenyeji.

Pamoja na Cecafa kufanikiwa kuyarudisha mashindano hayo mwaka huu, tunadhani kuwa bado ina jukumu kubwa la kuangalia upya mfumo wa mashindano yake.

Kwa sasa kote ulimwenguini hakuna mashindano ya klabu yanayokutanisha timu zaidi ya kumi kwenye kituo kimoja. Ni mashindano ya timu za taifa tu.

Kwa hiyo, mfumo wa sasa unaweza kuwa umepitwa na wakati.

Kwa hiyo Cecafa pia haina budi kama mfumo huo ni bora, hasa kipindi cha Juni na Julai ambacho hutumiwa zaidi na mashirikisho ya kimataifa --Fifa na CAF-- hukitumia sana kwa mashindano yake, kama ilivyo mwaka huu Kagame imegongana na Kombe la Dunia.

Ni muhimu kwa Cecafa kuangalia kama itaweza kuendesha mashindano yake kwa mtindo wa ligi itakayochezwa nyumbani na ugenini. Yaani Cecafa ikubaliane na nchi wanachama ili ligi zao zisimamame wiki fulani kupisha michuano ya Cecafa-- iwe mwishoni mwa wiki fulani au katikati ya wiki.

Pia nchi za Cecafa ndizo zinaruhusiwa kushirikisha timu mojamoja katika michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika na Kombe la Shirikisho.

Kwa kuendesha kwa mtindo wa ligi, maana yake Cecafa inaweza kuruhusu hadi mshindi wa tatu au wa nne kushiriki ligi yake.

Maana yake ni kwamba Ligi ya Cecafa (kama itaanzishwa) inaweza kushirikisha timu bora na nyingi zaidi ambazo zitaongeza ushindani, kuvuta mashabiki wengi na wadhamini pia.