http://www.swahilihub.com/image/view/-/4699202/medRes/2070210/-/p4hdhi/-/canaan.jpg

 

Canaan Sodindo Banana: Rais wa kwanza wa Zimbabwe

Canaan Sodindo Banana

Marehemu Canaan Sodindo Banana. Picha/MTANDAO 

Na SAMMY WAWERU, MASHIRIKA na KABRASHA LA HISTORIA

Imepakiwa - Monday, August 6  2018 at  06:18

Kwa Muhtasari

Wiki iliyopita wapigakura nchini Zimbabwe walishiriki uchaguzi mkuu.

 

WIKI iliyopita wapigakura nchini Zimbabwe walishiriki uchaguzi mkuu.

Rais Emmerson Mnangagwa aliyeshinda kura za uchaguzi wa Julai 30, 2018, mwanzo alitwaa wadhifa huo tangu 2017 baada ya Robert Mugabe kung'olewa mwezi Novemba na jeshi la nchi hiyo.

Mugabe aliingia mamlakani 1987 na kuwa Rais aliyeongoza taifa hilo kwa muda mrefu.

Kadhalika, Mugabe ni kiongozi ambaye amekuwa madarakani kama Rais kwa muda mrefu zaidi Barani Afrika. Katika uchaguzi wa Julai 30, 2018 Mnangagwa aliyetetea wadhifa wake kwa tiketi ya chama tawala cha ZANU-PF aliibuka mshindi kwa kuzoa asilimia 50.8 ya kura zilizopigwa. Asilimia hiyo ikiwakilisha kura 2,460,463 huku mpinzani wake wa karibu Nelson Chamisa wa Movement for Democratic Change (MDC) akipata asilimia 44.3, sawa na kura 2,147,436.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa tume ya uchaguzi Zimbabwe, ZEC ambapo mwenyekiti wake Bi Priscilla Chigumba alizitangaza Ijumaa Agosti 3. Licha ya MDC kupinga matokeo hayo, Rais Mnangagwa alieleza kufurahishwa kwake na ushindi wake. "Nimefurahi, huu ni mwanzo mpya. Japo tulitofautiana debeni tuko pamoja kuafikia ndoto zetu," akasema.

MDC chini ya kiongozi wake Chamisa, inashikilia kuwa wizi wa kura ulitekelezwa katika shughuli hiyo hivyo basi matokeo yaliyotolewa ni ghushi.

Endapo Mnangagwa ataapishwa rasmi, atakuwa Rais wa tatu wa Jamhuri ya Zimbabwe. Rais Mugabe aliyetawala taifa hilo chini ya ZANU-PF alikuwa Rais wa pili, ambapo alimrithi Canaan Banana. Mugabe alikuwa Waziri Mkuu chini ya utawala wa Rais huyo.

Banana ambaye alikuwa mwanasiasa na Msomi wa Maswala ya Dini, ndiye Rais wa kwanza Mwafrika Zimbabwe, ambaye pamoja na Mugabe na Mnangagwa walipigania uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa serikali ya mkoloni. Aidha, Zimbabwe ilipata uhuru 1980.

Kiongozi huyo anayejulikana kwa jina Canaan Sodindo Banana, alizaliwa Machi 5, 1936, Esigodini, Southern Rhodesia kama ilivyojulikana Zimbabwe chini ya utawala wa Wabeberu.

Alisomea shule ya msingi ya Kimishonari ya Mzinyati, kisha akajiunga na ya sekondari ya Tegwani. Baadaye alisomea taaluma ya ualimu kabla ya kujiunga na taasisi ya mafunzo ya Dini ya Epworth, Harare.

Uhuru

Mwaka 1962 msomi huyo wa maswala ya dini alitawazwa kuwa 'Waziri' wa muungano wa Kimishonari wa Methodist. Hata hivyo, kati ya 1960-1970, Banana alikuwa akijihusisha na maswala ya siasa hasa ya kutetea uhuru wa Zimbabwe.

Kwa ushirikiano na Askofu Abel Muzorewa waliunda United African National Council (UANC). UANC ilifanya mipango yake kwa karibu na Zimbabwe African People's Union (Zapu), chama kilichoundwa na mwanasiasa Joshua Nkomo. Kwa wakati huo ZANU ilikuwa imeundwa, Mugabe akiwa kiongozi wake.

Banana baadaye akigura UANC na kujiunga na Zanu. Chini ya katiba mpya iliyozinduliwa, msomi huyo alitawazwa kuwa Rais wa kwanza Zimbabwe ambapo alitawala taifa hilo kati ya 1980-1987.

Mugabe alipomrithi, alibadilisha Zanu kuwa Zanu-PF.

Licha ya kuwa Rais wa kwanza na mwanzilishi wa Zimbabwe, Banana alikabiliwa na tuhuma za ushoga wakati akiwa mamlakani. Alifunguliwa mashtaka 11 mwaka 1997 lakini akayakanusha. Hata hivyo, baada ya kufanya mkutano na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Marehemu Nelson Mandela alimshawishi kukubali mashtaka yake.

Alihukumiwa kifungo cha miaka 10 Januari 18, 1999, japo kikapunguzwa hadi miezi sita pekee.

Banana aliaga dunia Novemba 10, 2003, baada ya kuugua ugonjwa wa Saratani.