http://www.swahilihub.com/image/view/-/2950712/medRes/1172516/-/1568wyvz/-/TOP40CAROLINEMUTOKO%25282%2529.jpg

 

Caroline Mutoko: Mwanahabari nguli wa kike nchini Kenya

Caroline Mutoko

Mwanahabari mwenye uzoefu Bi Caroline Mutoko. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Monday, April 16  2018 at  06:00

Kwa Muhtasari

Caroline Mutoko alijiundia jina katika mawimbi ya vyombo vya habari baada ya serikali kukubali kuweka huru sekta ya utangazaji na ikatoa leseni kwa wamiliki wa kibinafsi.

 

CAROLINE Mutoko alijiundia jina katika mawimbi ya vyombo vya habari baada ya serikali kukubali kuweka huru sekta ya utangazaji na ikatoa leseni kwa wamiliki wa kibinafsi.

Hapo ndipo Wakenya wengi walipata fursa kumjua; hasa akiwa katika kipindi chake cha asubuhi cha Kiss 100.

Wengi walisifu sauti yake nyororo na uelewa wake wa masuala chungu nzima.

Mutoko alizaliwa Januari 4, 1973.

Huandika makala katika gazeti la The Star na ambapo huwa na wafuasi wa hisia mseto kuhusu maoni yake ya masuala kama siasa, uchumi na yale ya kijamii kwa ujumla.

Kufanya kazi katika shoo moja na mwanasarakasi Walter Mong’are almaarufu kama Nyambane kulimpa fursa adimu ya kutambulika upesi.

Amesomea katika shule za hadhi kama Harvard Business School na UCLA Anderson School of Management, Chuo Kikuu cha Strathmore na pia Chuo Kikuu cha Nairobi.

Alisomea elimu yake ya sekondari katika shule ya Loreto Convent Valley Road na pia akawa katika kazi ya mauzo katika kampuni ya Radio Africa ambayo inamiliki Kiss 100 na vituo vingine kadhaa sambambamba na gazeti la The Star.

Ashateuliwa na serikali kuwakilisha masilahi ya wanawake katika tasisi mbalimbali, ikiwemo ile ya utalii na ile ya taasisi ya masomo ya utangazaji ya KIMC.

Sio mengi yake ya ndani hujulikana kuhusu Caroline Mutoko, masuala kama mchumba wake au mume kamili na masuala mengineyo kuhusu hayo, lakini ni mama mlezi wa mtoto mmoja. Ni mtoto ambaye alirithi kutoka kwa mhisani mnamo Agosti 26, 2011, akiwa na umri wa miezi minane pekee.

Kulea

Mutoko husisitiza kuwa amejituma kumlea mtoto huyo kwa hali na mali na ndiye nguzo yake kuu katika kujituma kusaka hela za kimaisha ili ampe mtoto huyo maisha yanayomfaa.

Mkatoliki, vyombo vya udaku vimekuwa vikimnyemelea kuhusu hili au lile la mitaani, akijitokeza kukabili fichuzi hizo kwingine akikiri ni ukweli, kwingine akisema ni uongo wa kipuzi.

Mutoko amefichua kuwa wazazi wake ni Bw Criss Mutoko naye mamake akiwa ni Rose Mutoko.

Anaorodheshwa miongoni mwa watangazaji ambao huvuna kitita cha juu zaidi kama mshahara, anayeelewa kuhusu siasa za ajira na ambapo husemwa kuwa karibu sana na mameneja katika safu ya ajira.

Husema kuwa hakuangukia bahati yake ya mihela kama mshahara wala akacheza kwa lolote lingine ili afanikiwe, bali alijituma, akafanya kazi kwa bidii na akawa na uadilifu kazini.

Mutoko husema kuwa simu yake ya kwanza ilikuwa Erickson T18 na kabla ya aanze kujulikana, alikuwa akiumia polepole nyuma ya umaarufu wake wa sasa ambapo alikuwa akichapa kazi Capital FM kwa bwanyenye Chris Kirubi na ambapo kwa miezi sita, hakupata malipo ya aina yoyote.