Chama cha Wanasheria na mfupa uliomshinda fisi

Imepakiwa - Wednesday, April 10  2019 at  13:20

 

Wiki iliyopita Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilipata viongozi wapya wa kukiongoza kwa mwaka mmoja. Kama walivyoeleza wanasheria hao na kuonyesha kwa kura zao, sisi wengine tunaamini viongozi hao watasimama imara kuhakikisha utawala wa sheria unatamalaki nchini.

Nimeipa makala hii kichwa cha habari ‘TLS na mfupa uliomshinda fisi’ nikimaanisha hiki ndio chombo muhimu si kwa Tanzania tu, katika nchi nyingi duniani, chenye uwezo wa kutafuna mfupa uliomshinda fisi.

Malalamiko ya vyama vya siasa tunayoyasikia sasa, kelele za kukandamizwa kwa haki za binadamu na za kiraia na kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari si kiashiria kizuri cha utawala wa sheria, hiyo wanasheria ndio wanabaki kama nguzo ama ya kuonyesha mfano au ya kuyatetea na kuyafanikisha.

Manung’uniko yanayojitokeza sasa kuhusu maamuzi ya Bunge yanaangukia katika utawala wa sheria, watu kujichukulia sheria mkononi ni kulegalega kwa utawala wa sheria na hata ukiukwaji wa Katiba.

John Carey ambaye ni profesa wa Sayansi ya siasa katika Chuo kikuu cha Dartmouth anasema moja ya njia muhimu ya kutafsiri demokrasia katika nchi yoyote ile ni uwepo wa utawala wa kweli wa sheria.

Anasema wakati wanademokrasia wakichagua viongozi wao na wawakilishi kupitia chaguzi, utawala wa sheria unatafsiri uhusiano kati ya wawakilishi (wabunge na madiwani) na raia katikati ya uchaguzi.

Profesa Carey anatafsiri maana ya utawala wa sheria na kuwa ni pale sheria inapokuwa kama msumeno ikikata mbele na nyuma hata kwa watendaji wa Serikali na wawakilishi tuliowachagua.

Katika uchaguzi wa wiki iliyopita, mawakili walimchagua kwa kura nyingi, Dk Rugemeleza Nshala kuwa Rais wa TLS. Wengi tunaitazama TLS mikononi mwake tukiamini pengine kipele kimepata mkunaji.

Tunatarajia kwa kupitia njia sahihi, atatuondoa katika wingu ili tujue makatazo yale ya mikutano ya vyama vya siasa yako kwa mujibu wa sheria? Kilichofanywa na Bunge dhidi ya CAG ni sahihi kisheria.

Aristotle, aliyekuwa mwanafalsafa wa Kigiriki aliyeishi zaidi ya miaka 2,000 iliyopita, naye aliwahi kutamka maneno haya “utawala wa sheria ni bora kabisa kuliko utawala wa mtu binafsi”.

Hayati Lord Denning (1899- 1999) ambaye alikuwa Jaji wa Uingereza naye aliwahi kusema maneno yafuatayo kuhusu utawa wa sheria “Once great power is granted, there is a danger of it being abused.”

Kwa tafsiri yangu ni kwamba “Pale ambapo madaraka makubwa yanatolewa, ipo hatari kubwa kwamba yanaweza kutumiwa vibaya”

Nchini mwetu sasa kumeanza kuonekana viashiria vya uwepo wa upendeleo kwa vyombo vya dola katika kusimamia “vibali” vya mikutano ya kisiasa kati ya chama tawala na vile vya upinzani.

Inatakiwa uwepo uwezekano wa kuwabana walio madarakani ili wasitumie vibaya madaraka waliyopewa kisheria, ikiwa ndio hatua ya kwanza ya kusimika utawala wa sheria kwa Tanzania na kokote duniani.

Kwanza, sheria zinazotoa madaraka lazima zitafsiriwe na mahakama kwa usahihi dhidi ya wale walio madarakani ili wasidhulumu au kukandamiza haki za raia ambazo ndiyo tunda la amani.

Pili, watawala wasikubaliwe kutenda chochote ambacho hakiko katika sheria. kama ilivyosisitizwa mwaka 1765 na Jaji Mkuu wa Uingereza, Lord Camden kuwa, kama ni sheria basi ionekane kwenye vitabu.

Ndio maana ninaushauri uongozi huu mpya wa TLS, kwa kuwa umeweza kuendana na matakwa ya wanachama wake, uchukue jukumu la kuwa balozi mzuri na kuisaidia nchi, ili kuhakaikisha utawala wa sheria ambao ndiyo suluhu ya amani yetu, unatamalaki nchini.