Changamoto tasnia ya habari zimalizwe

Imepakiwa - Friday, May 3  2019 at  10:45

 

Leo, wanahabari nchini wanaungana na wenzao duniani kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, ambayo huiadhimisha kwa namna mbalimbali, ikiwamo kuwakumbuka wenzao waliopoteza maisha wakipigania haki za wananchi kupitia kalamu zao.

Vilevile, siku hii huitumia kuzikumbusha Serikali katika nchi zao na jumuiya ya kimataifa kuweka mazingira wezeshi kwa waandishi wa habari ili waweze kutekeleza majukumu yao bila vikwazo vyovyote.

Wanahabari pia hukumbushana uzingatiaji wa sheria, kanuni na miongozo inayosimamia taaluma yao ili pale wanapotekeleza majukumu yao, wajikite katika utekelezaji wa misingi ya haki huku wakizingatia utu na maadili.

Bahati mbaya ni kwamba, tasnia ya habari ambayo ni kama mhimili wa nne katika taifa lolote kutokana na majukumu iliyotwishwa, watendaji wake ambao ni wanahabari wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali zikiwamo za kisheria, kuuawa na hata kutekwa ili tu wasiripoti habari au matukio ambayo watu wachache wanadhani ni tishio kwao.

Changamoto hizo ndizo zinazowafanya wanahabari, wakati mwingine, wajione kuwa wanyonge na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, kwa mujibu wa sheria, kanuni na hata maadili ya kitaaluma.

Kwa upande wa sheria, hata hapa nchini zipo ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wanataaluma kwamba ni kikwazo katika kutimiza kazi zao kwa ufanisi. Sheria kama ile ya Huduma za Habari ya 2016, ya Takwimu ya 2018 na ya Makosa ya Mitandao ya 2015 zinalalamikiwa kuwanyima uwanja mpana wanahabari kutekeleza majukumu ya kitaaluma.

Kidunia, kumekuwa na matukio mengi ya nayokwaza utendaji kazi wa wanahabari. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), waandishi wa habari 1,307 wameuawa kuanzia mwaka 1994 hadi 2018.

Mwaka jana pekee, kwa mujibu wa Unesco, wanahabari 99 walipoteza maisha ikiwa ni matukio yanayohusishwa na hali ya mamlaka za nchi kutojali uhalifu dhidi ya waandishi wa habari wawapo kazini.

Aidha, wanahabari wengi wamekuwa wakipotea katika mazingira ya kutatanisha duniani na kwa hapa nchini bado tukio la mwanahabari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited wilayani Kibiti, Azory Gwanda lingali mioyoni mwa wanatasnia wenzake.

Wakati tukiadhimisha siku hii muhimu kwa tasnia ya habari, tunaziomba mamlaka za nchi kuongeza nguvu katika ulinzi wa wanahabari katika mazingira yao ya kazi ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Tunasema hivyo kwa sababu umuhimu wa mhimili huu ndani ya jamii unamgusa mwananchi mmojammoja na Taifa zima kwa ujumla, kiuchumi na kijamii. Msukumo unaotokana na habari hubadili mazingira ama kwa kuyaboresha zaidi au kuibua mijadala inayosaidia kubadilisha mambo.

Tunaiomba Serikali, kwa nafasi yake kuziangalia upya sheria na kanuni zinazolalamikiwa na wanatasnia ambazo zinagusa shughuli zao za kila siku wawapo katika ukusanyaji na uchakataji wa habari.

Mwisho ni kwa wanahabari kusimamia maadili, sheria na kanuni pale wanapotekeleza majukumu yaou ikiwa ni miongozo muhimu ya kuwawezesha kufanikisha wajibu wao kwa jamii. Maendeleo ya Taifa letu yanawategemea kwa kiasi kikubwa na ni wajibu wa kila mmoja kuitanguliza mbele Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.