http://www.swahilihub.com/image/view/-/4919908/medRes/2214337/-/8y69t0z/-/vifaa.jpg

 

Chondechonde wafanyabiashara mwezi huu

Mfanyabiashara wa Soko la Mchikichini Ilala jijini Dar es Salaam akisubiri wateja wa kununua mahitaji ya Shule kwa ajili ya maandalizi ya mhula mpya wa masomo unaotarajia kuanza wiki ijayo kote nchini. Picha na Omar Fungo   

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Thursday, January 3  2019 at  13:02

Kwa Muhtasari

Bidhaa zinazoendana na maandalizi ya wanafunzi zisichukuliwe kama mtaji

 

Januari imeingia, msimu mpya wa masomo umewadia. Kipindi kama hiki kila mwaka wazazi na walezi huwa katika pilikapilika za kushughulikia mahitaji ya watoto wao wanaojiunga na ngazi mbalimbali za elimu.

Mwezi huu wale wanaojiunga na shule za awali, msingi na sekondari wote hutakiwa kuripoti shuleni katika tarehe zilizopangwa na kwa mwaka huu nyingi hususani za Serikali zimepangwa kufunguliwa Januari 7.

Pamoja na mambo mengine, kipindi kama hiki wazazi wengi huenda mbio kutokana na kupanda kwa gharama za vifaa vya shule. Ukigusa kiatu kinachotumika kama sare ya mwanafunzi shuleni hata kama katika nyakati zingine kilikuwa kikiuzwa kwa Sh5,000 sasa utaambiwa mwisho Sh10,000 chini ya hapo hupati.

Vivyo hivyo kwa vifaa vingine kama mabegi, madaftari, sare na vyote vinavyoendana na maandalizi ya mwanafunzi wakati kama huu hupandishwa bei. Huu ni utaratibu usiopaswa kuendelezwa na wafanyabiashara wa bidhaa hizo.

Ni muhimu kwa wale wote wanaohusika na uuzaji wa bidhaa hizo kutotatazama masilahi na faida kubwa tu, bali hata umuhimu wa bidhaa hizo katika kufanikisha ujenzi wa misingi ya Taifa kupata wataalamu wa baadaye. Bidhaa zinazoendana na maandalizi ya wanafunzi zisichukuliwe kama mtaji wa kupata fedha nyingi ndani ya muda mchache na kujitajirisha, itazamwe pia kama huduma muhimu kwa masilahi ya walio wengi.

Pamoja na kwamba biashara sasa ni huria, ipo haja kwa wafanyabiashara kuona umuhimu wa kufanya biashara isiyoumiza wengine. Wauze kwa wingi kwa bei nzuri.

Ikumbukwe kwamba Desemba ilizungukwa na mfululizo wa sikukuu muhimu za kijamii ambazo wazazi na walezi wengi walihusika katika maandalizi, hivyo ni vyema kuwapa ahueni.

Kwa upande mwingine kuingia kwa mwaka mpya wa masomo ni fursa nyingine kwa shule mbalimbali kujifanyia tathimini, kufanya maboresho, kuweka mikakati na kuchapa kazi kisawaswa ili kufuta sifuri na ufaulu wa chini wa wanafunzi wao kuanzia katika mitihani ya ndani na hata ile ya kitaifa.

Shule za Serikali zikiwamo za msingi na sekondari hasa zile za kata, zinapaswa kutambua kwamba ndilo tegemeo la wananchi wengi, hivyo zijipange kuwaandaa watoto sio tu kwa ajili ya kufaulu mitihani, bali pia kufanikisha kupatikana kwa wataalamu walioandaliwa vyema kuanzia ngazi za chini hadi kufikia katika ubobezi.

Hata hivyo, hatutarajii kuona upungufu uliojitokeza mwaka uliopita ukijirudia mwaka huu kwa baadhi ya halmashauri kutajwa kuhusika na hadaa za mitihani ili zionekane zinafanya vizuri, badala yake huu ni wakati wa kujiandaa vyema kuwaivisha wanafunzi ili hatimaye waweze kufanya kile wanachotakiwa kufanya. Njia bora zibuniwe kutoa hamasa katika ngazi tofauti.

Tunawatakia heri wanafunzi wote wanaoanza au kurejea katika masomo ya ngazi mbalimbali. Wasome kwa bidii wakitambua wazazi, Serikali na jamii kwa jumla imekuwa ikiumiza kichwa kuhakikisha wanapata haki yao ya msingi ya elimu.

Waepuke vishawishi vinavyoweza kuwaingiza katika kundi la kutimuliwa ama kwa ulevi, mimba au uesharati. Wazingatie masomo, wasome kwa bidi ili hatimaye waje kuwa tegemeo kwa nchi mbalimbali.