http://www.swahilihub.com/image/view/-/3848096/medRes/1624472/-/h5b07a/-/RWE.jpg

 

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilivyojiimarisha kuwa  kitovu cha Kiswahili

Profesa Rwekaza S. Mukandala

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza S. Mukandala akihutubu awali. Picha/ HISANI 

Na GADI SOLOMON

Imepakiwa - Monday, March 20  2017 at  11:52

Kwa Mukhtasari

MABADILIKO yanayohusu lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki, Afrika na dunia kwa kiasi kikubwa chimbuko lake ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

 

Chuo hicho kikongwe nchini kilichopo chini ya uongozi wa Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Rwekaza Mukandala, kimefanikisha lugha ya Kiswahili kupiga hatua nchini na ulimwenguni kutokana na kuzalisha wataalamu ambao wamekuwa chachu ya kueneza Kiswahili mataifa mbalimbali duniani kama vile Zimbabwe, Afrika Kusini, Rwanda, Ujerumani na Marekani.

UDSM kupitia Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki), kimekuwa chachu ya mabadiliko kutokana na kusaidia Kiswahili kukua na kutanuka. Chuo hicho kimeimarisha ushirikiano na mataifa hayo kupitia wanazuoni wake ambao wamekuwa katika mapambano kuhakikisha Kiswahili kinafundishwa kwenye vyuo vikuu.

Tafiti za kisayansi na machapisho mbalimbali ambayo yametolewa tangu ilipokuwa ikitambulika kama Idara ya Kiswahili na baadaye kuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) na kuleta mabadiliko makubwa kuwa Tataki ni miongoni mwa mambo ambayo yamekifanya chuo hicho kuendelea kuwa kitovu cha lugha ya Kiswahili duniani.

Kwa wanafunzi wengi wanaotoka nje ya nchi, chuo hicho kimekuwa kimbilio lao kama sehemu ya kujifunzia lugha ya Kiswahili.

Katika utawala wa Makamu wa Chuo, Profesa Mukandala tumeshuhudia mabadiliko mengi katika taasisi ya Kiswahili kwa kuamua kitumia lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya mawasiliano chuoni hapo kwenye vikao mbalimbali vya utawala na vinavyohusu wanafunzi na menejimenti.

Kutokana na mafanikio hayo, bila shaka vyuo vingine vinaweza kuamua kuiga jambo hilo  lenye masilahi kwa Taifa. Hiyo ni hatua kubwa katika maendeleo ya Kiswahili nchini na duniani.

Uamuzi kutumia Kiswahili katika baadhi ya kozi

Kuamua kuanza kufundisha baadhi ya kozi kwa Kiswahili ni jambo linalokifanya chuo hicho kuwa cha kwanza nchini kuendeleza lugha ya Kiswahili. Jambo hilo ambalo lipo kwenye mipango ya chuo hicho bila shaka likianza utekelezaji wake litaiwezesha Kiswahili kuthibitika kwamba ndipo chimbuko lake.

Uamuzi huo umeamsha hisia kwamba lugha ya Kiswahili ambayo imekuwa ikipigwa teke kwa miaka mingi, kwa sasa inawezekana kutumika katika nyanya mbalimbali kama vile uchumi, elimu, sheria, sayansi, teknolojia na maeneo mengineyo  ya mawasiliano

Utafiti uliofanya na wanataaluma kutoka maeneo mbalimbali duniani inaonyesha kwamba, mwanafunzi akifundishwa kwa lugha yake ya kwanza hupenda kujifunza zaidi na huelewa vyema jambo hilo. Kilichobaki ni Watanzania kuamua wenyewe.

 

Profesa Mukandala na Kiswahili

Profesa Mukandala ni miongoni mwa viongozi nchini ambao wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mawanda ya matumizi ya Kiswahili yanaongezeka.

Kiongozi huyo amekuwa na kiu kuona kwamba lugha ya Kiswahili inaheshimika ndani ya mipoka ya nchi na nje ya Tanzania.

Tataki

Taasisi hiyo iliyopo chini ya Mkurugenzi wake, Ernesta Mosha imefanya mambo mengi ikiwapo kufanikisha machapisho ya vitabu vya masomo yote kwa lugha ya Kiswahili hususan yanayofundishwa katika elimu ya sekondari.

Taasisi hiyo imekuwa na mchango mkubwa kutokana na kuwaunganisha wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili nchini.

Hivi karibuni iliandaa Tuzo za Mabati Cornel ambazo zililenga kuhamasisha wananchi kuwa na mwamko wa uandishi wa kazi za fasihi.

Tanzania ilitoa washindi watatu waliowasilisha muswada wa kazi zao ambazo zilipigiwa kura na jopo la wachambuzi, huku mshindi wa kwanza akiibuka na kitita cha Sh10 milioni.

Ushirikiano wa taasisi hiyo na taasisi zingine uwewezesha kuwaunganisha wazungumzaji wa Kiswahili nchini na kujisikia wakithaminiwa na kuonekana wa thamani kutokana na kuzungumza lugha ya Kiswahili.

 

Mdahalo wa kitaifa wa Kiswahili

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuona umuhimu wa kuwa na mdahalo wa Kiswahii, kiliamua kushirikiana na wadau wengine wa Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kufahamu zaidi kuhusu mwelekeo wa lugha yao.

Mada iliyoandaliwa kujadiliwa  katika mdahalo huo, itwapa nafasi wananchi kutoa maoni iwapo Kiswahili kinafaa kwa matumizi katika nyanja zote au la!

Mdahalo huo unatarajiwa kuwa na pande mbili, wanaopinga na wanaokubali kuhusu kutumia Kiswahili katika nyanja mbalimbali.

Mdahalo huo utakaorushwa mubashara kwenye vyombo vya habari utatoa fursa kwa Watanzania kujadili kwa uwazi.

Matokeo ya mdahalo huo

Mdahalo huo utawawezesha watunga sera kuamua iwapo waendelee kutumia lugha za kigeni katika nyanya mbalimbali kama vile sheria, uchumi, teknolojia, elimu kwani jambo  hilo likipitishwa kwa kauli moja na wananchi walio wengi huenda watunga sera wakalifanyia kazi na kutungia sheria.

 

Washiriki wa mdahalo

Mdahalo huo ulioandaliwa na Chuo Kikuu kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Kiswahili-Kanda ya Tanzania umelenga kuwashirikisha wananchi wa kawaida, wasomi, wataalamu kutoka nyanja mbalimbali. Pia wageni kutoka mataifa ambayo tayari yamepiga hatua kwa kutumia lugha zao.

 

Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki

Kuundwa kwa kamisheni hiyo ambayo iliridhiwa na nchi wananchama, imekuwa chachu kwa kuanzishwa vyama mbalimbali katika kila nchi wanachama.

Chama cha Waandishi wa Habari za Kiswahili Kanda ya Tanzania kimekuwa chachu katika kutekeleza majukumu yake ikiwamo kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini.

Chama hicho kinachoundwa na waandishi wa hababari, watayarishaji wa vipidi vya Kiswahili kimeleta hamasa mpya nchini kutokana na kuona umuhimu wa kuwa sehemu ya waandaaji wa mdahalo huo.

Kamisheni hiyo yenye makao makuu yake Zanzibar, imefanikiwa kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika nchi wananchama na kuleta hamasa mataifa kama vile Rwanda kuongeza kasi ya kujifunza lugha ya Kiswahili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.