http://www.swahilihub.com/image/view/-/4661012/medRes/2043408/-/4imyjuz/-/aidani.jpg

 

Costech wazidi kutibua mazito utafiti wa Twaweza

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyekuze 

Na Ibrahim Yamola

Imepakiwa - Friday, July 13  2018 at  12:32

Kwa Muhtasari

Imekana kuhusika na utafiti wa kukusanya maoni ya wananchi

 

Dar es Salaam: Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imesema barua kwenda taasisi ya Twaweza iliyosambaa mitandaoni, kuhusu kutakiwa kujieleza, ni ya chombo hicho cha Serikali, lakini ikasita ikasema haihusiki na utafiti wa kukusanya maoni ya wananchi.

Costech pia imeeleza kushangazwa na kitendo cha barua hiyo kusambaa mitandaoni, lakini ikikataa au kujibu kw aufupi maswali ya wanahabari kuhusu sakata hilo.

Barua hiyo iliyosambaa kuanzia juzi, inaonyesha kuwa Costech imeiandikia Twaweza ikitaka itoe maelezo ndani ya siku saba kuhusu kufanya utafiti katika mradi wa Sauti za Wananchi, ambao matokeo yake yalionyesha kupungua umaarufu kwa viongozi wa Serikali, vyama na wabunge.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu aliyeongea na waandishi wa habari akiwa pamoja na mwanasheria wa tume hiyo, Zainab Bakari alieleza kusikitishwa na kusambaa kwa barua hiyo.

Dk Nungu, aliyesoma taarifa ya ukurasa mbele ya wanahabari, alisema baada ya kufuatilia katika mitandao ya kijamii, Costech imejiridhisha kuwa barua hiyo ni halali na ilipelekwa Twaweza ili kupata ufafanuzi wa utafiti wao.

“Tunasikitika kuona mawasiliano halali ya kiofisi yanapelekwa mitandaoni hata kabla ya kujibiwa rasmi,” alisema Dk Nungu.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema wamepokea barua hiyo na wanaifanyia kazi, lakini akakana kuisambaza mitandaoni.

Eyakuze alisema barua ambazo zimekuwa zikiwafikia hugongwa muhuri kuonyesha zimepokelewa lakini inayosambaa mitandaoni haina muhuri wa Twaweza na kuongeza kuwa wanaheshimu mawasiliano na wadau wao.

Matokeo ya utafiti huo wa Twaweza yaliyotangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita, yanaonyesha kuporomoka kwa ukaribu wa wananchi na vyama vya siasa, utekelezaji wa majukumu kwa viongozi walioko madarakani, kukubalika kwa utekelezaji wa majukumu wa Rais tangu alipoingia madarakani na uhuru wa kujieleza katika baadhi ya maeneo.

Hat hivyo, maswali ya waandishi wa habari jana kuhusu uhusiano wa utafiti huo na mamlaka ya Costech hayakujibiwa. badala yake, watendaji hao waliondoka.

Moja ya maswali waliyoulizwa ni kwa nini wameamua kuwaandikia barua Twaweza ikiwa utafiti huo unafanyika mara kadhaa?

Nungu: Sio mara ya kwanza Costech kuwasiliana na wadau wetu, lakini tunasikitika kuiona barua yetu katika mitandao, sidhani kama Mwananchi mawasiliano yenu yanakwenda mitandaoni. Twaweza si wa kwanza kuandikiwa barua za aina hiyo, ila huwa haziendi katika mitandao na nafikiri vyombo husika vitafuatilia na kuona nani kaipeleka na kwa nini.

“Tukianza kuongelea barua hiyo kabla ya kujibiwa sio (sahihi). Tuwape nafasi wao kujibu na kama usingeiona mtandaoni tusingekuwa hapa na kama wakijibu na kuona inafaa zaidi kuja katika media, tutakuja.”

Hata hivyo, Dk Nungu alipoulizwa kama Twaweza wanachofanya ni kukusanya maoni ya wananchi, je. televisheni zinapoendesha vipindi vya namna hiyo huomba kibali? Mkurugenzi huyo alisema: “Hatujasema kwamba ile ni opinion poll (maoni ya wananchi), hatujasema hivyo.

Mwandishi: Swali langu mimi nimeuliza, opinion poll ni tafiti za kisayansi?

Nungu: Kipindi cha Twaweza kwamba hatujawahi kukiratibu wala hatujawahi kukiandikia barua, kwa hiyo opinion poll ni opinion poll na tafiti ni tafiti.

Mwandishi: Opinion poll sio scientific research (utafiti wa kisayansi)?

Nungu: Opinion poll inabaki kuwa opinion poll na tafiti inabaki kuwa tafiti na barua yetu inabaki palepale inasema kwamba mdau wetu, ndio maana nasema sitaki kuiongelea. Ajieleze, sasa majibu yake ndio yatakuja na kusema nini ni nini na kama nilivyosema kama isingekuwa mitandaoni wala tusingekuwa hapa.

Kwa mujibu wa mwongozo wa usajili na utafiti wa Costech, “utafiti utaeleweka kama aina yoyote ya uchunguzi, majaribio na tathmini iliyoandaliwa kwa ajili ya kuendeleza au kuchangia katika maarifa”.

Costech inaeleza katika mwongozo huo kuwa utafiti huo utahusu sekta zote kama vile viwanda, dawa, kilimo, binadamu na sayansi ya jamii, ikiwa ni pamoja na majaribio ya kazi za maendeleo ambazo zitazalisha ubunifu mpya, bidhaa na michakato kwa ajili ya maendeleo ya ya binadamu.

Costech ni chombo cha umma kilichoanzishwa kwa Sheria Namba 7 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ya 1986 kuchukua nafasi ya chombo kilichokuwa kinaitwa Utafiti.

Costech kiko chini ya wizara inayohusika na sayansi na teknolojia na ndio chombo kikuu cha ushauri kwa Serikali kwa masuala yanayohusu utafiti wa kisayansi, ubunifu na maendeleo na uhamishaji wa teknolojia.