DTL yasafisha Dandora na kuwapa vijana ajira

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Monday, December 21  2015 at  14:57

Kwa Muhtasari

Dandora Transformation League (DTL) ni kikundi cha vijana ambacho kimeanzisha mpango wa kubadilisha mtaa wa Dandora kutoka dhana ya kale ya uchafu na kuwa eneo lenye usafi, usalama, mabustani ya miti na maua, mbali na kutoa nafasi za ajira kwa vijana.

 

WENGI wanapofikiria kuhusu mtaa wa Dandora uliyoko Mashariki mwa jiji la Nairobi, picha inayowajia machoni ni ya jaa kubwa la taka, uhalifu, vijana wasio na ajira na viwango vya juu vya urtovu wa usalama.

Lakini dhana hii inaelekea kufikia kikomo, kwa mujibu wa juhudi za Dandora Transformation League (DTL), kikundi cha vijana ambacho kimeanzisha mpango wa kubadilisha mtaa huu kutoka fikra hiyo ya kale, na kuwa eneo lenye usafi, usalama, mabustani ya miti na maua, mbali na kutoa nafasi za ajira kwa vijana.

Kikundi hiki kinahusisha vijana waliojikusanya na kujigawanya kwa vikundi kadha kuanzisha mfumo wa vitalu yaani courts, sawa na unaoshuhudiwa katika mitaa mingine ya watu wenye mapato wastani.

Kufikia sasa kikundi hiki kimefaulu kuunda zaidi ya vitalu 139 huku kila eneo likiwa na kitalu chake chenye majina ya kipekee kama vile Mustard Seed, Tunawiri, Gift miongoni mwa mengine.

“Tulijikusanya kama vijana wa kitalu cha Mustard Seed na tukaanzisha mradi huu kwa kusafisha eneo letu. Lakini hatukuwa na fedha za kutosha na hapo ndipo tukatafuta ufadhili kutoka kwa wakfu wa Awesome Foundation,” aeleza Charles Gachanga, Mwenyekiti wa Kitalu cha Mustard Seed na afisa mkuu mtendaji wa DTL.

Kulingana na Bw Robert Eshialimba, mwanzilishi wa shirika la Awesome Foundation-Nairobi Chapter, baada ya kutazama jitihada za vijana hawa walianza kuwa na ndoto ya kutekeleza haya katika eneo lote la Dandora.

Ni hapa ndipo waliamua kuwahusisha vijana wengine ambapo walihimizwa kuanzisha vitalu vyao na kuvisajili ambapo mitaa yote 17 ya Dandora imewakilishwa katika bodi ya DTL.

Vigezo

Kati ya vigezo wanavyotumia kuchagua vitalu vinavyopaswa kutuzwa ni pamoja na usafi, uwazi wa eneo la kuegesha magari na usalama ambapo kitalu kinachoonyesha sifa nzuri zaidi kinapata tuzo.

Kufikia sasa mradi huu umefanikiwa kubadilisha takriban vitalu 139 huku mojawapo ya vyanzo vyao vya fedha ikiwa ada ndogo inayotolewa kutoka kila nyumba.

“Kila nyumba hutozwa Sh 100 kila mwezi ambapo pesa hizo tunazigawanya mara tatu. Sh50 tunazielekeza kwa usalama, Sh 30 kwa usafi na Sh 20 zinawekwa kama akiba ya kugharamia uhifadhi wa vifaa vingine kama vile makafuli, malango na upakaji rangi.

Kadhalika pesa zao zinatokana na uegeshaji magari ambapo kila gari linatozwa Sh100 kila usiku ambapo tayari wanafanya mipango na baadhi ya kampuni za matatu ambazo zimeahidi kuanza kutumia huduma zao.

Mradi huu umewawezesha vijana waliokuwa wanakaa mtaani kupata ajira, mbali na kuhakikisha usafi na usalama.

Katika harakati hizo mradi huu umepelekea vijana wengi waliofahamika kuwa wezi sugu kubadili mienendo yao.

Mbali na hayo juhudi za DTL zimefanikisha mpango wa Nyumba Kumi mtaani Dandora.

“Maeneo yanayoendeleza mpango wa Nyumba Kumi mtaani humu ni yale yaliyo chini ya DTL ambapo kupitia mfumo huu kadhalika tunajua idadi na maelezo ya watu wanaosihi kwa kila nyumba na hivyo ni ngumu kwa uhalifu kutendeka,” aeleza Gachanga.

Ni mradi ambao wanatumai kuelekeza hata kwenye jaa maarufu la taka la Dandora na tayari mipango ipo ambapo ifikiapo mwezi Februari 2016 kwa ushirikiano na UN Habitat wanapanga kuwa wa kwanza kuunda barabara kwa kutumia muunganisho wa plastiki wa cabro.