http://www.swahilihub.com/image/view/-/4396226/medRes/1940915/-/jun9ggz/-/kongwa.jpg

 

Nyani mkongwe Dandize asema usimamizi bora utaimarisha soka Kenya

Abdulaziz Swaleh

Mwanasoka mkongwe, Abdulaziz Swaleh (kati) akiwa na mashabiki wa mchezo huo hapo kale, Swaleh Bameda (kulia) na Mzee Iddi kwenye maskani ya Dandize Cafe, Majengo Libati mjini Mombasa. Picha/ABDULRAHMAN SHERIFF 

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

Imepakiwa - Monday, April 16  2018 at  17:04

Kwa Muhtasari

Hali ya mchezo wowote inaweza kuimarika ikiwa viongozi wake wanakubali kupoteza nyakati zao kwa sababu ya kusaidia mipango ya kuinua michezo hiyo.

 

UONGOZI bora wa mchezo wowote unahitaji maafisa wenye kujitolea.

Hali ya mchezo wowote inaweza kuimarika ikiwa viongozi wake wanakubali kupoteza nyakati zao kwa sababu ya kusaidia mipango ya kuinua michezo hiyo.

Kutokana na sababu hiyo, usimamizi wa kandanda nchini Kenya unahitaji watu walio tayari kujitolea kwa ajili ya mchezo huo upate kuimarika na kufikia viwango sawa na vile vya mataifa mengine.

Hayo ni maoni ya aliyekuwa kipa maarufu mkoani Pwani, Abdulaziz Swaleh almaarufu Dandize anaamini maongozi bora yakipatikana, hali ya soka hapa nchini itaimarika na timu za taifa za umri mbalimbali zitawika.

“Ninaamini hivi sasa tunahitaji viongozi wa kujitolea sawa na alivyokuwa aliyekuwa mwenyekiti wa soka mkoani Pwani, marehemu Sadla Khamis kwa sababu yeye alikuwa amejitolea kidhati kuhakikisha soka limeimarika sehemu hii yetu,” akasema Dandize.

Kipa huyo wa kale aliyewahi kuchaguliwa katika kikosi cha timu ya mseto ya Mombasa anasema ni jukumu la maafisa waliochaguliwa wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kuhakikisha wanatumikia na kuzisaidia klabu katika juhudi za kujiimarisha.

“Nyakati zilizopita, akina Sadla na wenzake walikuwa mara kwa mara wakitembelea makao ya klabu mbalimbali kuhakikisha klabu hizo zinafanya vizuri kwenye ligi zinazoshiriki,” akasema veteran huyo mwenye kumiliki biashara ya kuuza chakula katika maskan yake ya Dandize Café.

Wakati wake, Dandide aliyezaliwa mwaka 1960, alichezea klabu tatu zilizokuwa maarufu eneo la Majengo zilizokuwa zikiulikana kama Libati Heroes, Cosmos na Majengo Heroes. “Ningeliendeleza kipaji changu kama si kusafiri kwenda Arabuni kufanya kazi,” alisema.

Jagina huyo aliyewahi kucheza na baadhi ya wanasoka waliocheza Ligi Kuu katika klabu ya Shabana FC akina Salim Mabrouk na Orao Taita, anasema angelifikia kiwango cha kipa Mahmoud Abbas kama hakwenda kufanya kazi Arabuni.

“Nilihitajika na klabu nyingi lakini sikuweza kuweka saini yangu kwa sababu miaka hiyo klabu zilikuwa hazilipi mishahara kwa wachezaji wake. Wakati huo ukitoka kiwanjani utakuwa unapewa, ‘Well play mazee’, hakuna marupurupu yoyote utakayopata,” akaeleza.

Dandize anakumbuka vizuri kusajiliwa na aliyekuwa mchezaji wa AFC Leopards, Alex Nabakwe katika Shirika la Reli la Kenya akiwa mchezji. “Nilichezea timu ya Railways kwa miaka minne kabla ya kupata kazi ya kwenda Arabuni,” akasema.

Veterani huyo alisema nyakati hizi kumekuwa na wadhamini wachache wenye kuzisimamia timu, kinyume na zamani ambapo katika kila timu kulikuwa na watu maalum waliokuwa wakisimamia timu.

Akitoa mfano, Dandize alisema klabu ya Cosmos ilianzishwa na aliyekuwa kiongozi wa soka wa Pwani, Abdillahi Khamis Jinni ambaye alikuwa akiisaidia kwa mahitaji yake pamoja na matakwa ya wachezaji.

“Tukipata watu mfano wa kina Jinni, basi hali ya soka ya sehemu zote nchini itaimarika kwa kasi. Tunawajibika kuwatafuta watu aina hiyo kutoka kila sehemu ya nchi na hakuna kitakachozuia kwa Kenya kusifika kisoka,” akasema.

Ujuzi

Alimtaka Rais wa FKF, Nick Mwendwa ahakikishe timu za taifa zinachaguliwa kulingana na ujuzi wa wachezaji na wala kusiweko kutumika urafiki ama ujamaa. “Hatuwezi kuendelea ikiwa uteuzi wa timu za taifa hautafanyika kwa njia za uwazi na haki,” akasema.

Anasema hakuna matumaini yatakayokuwako kwa soka la Kenya kuwa imara kama wahusika wa kuchaguwa wachezaji wa timu za taifa hawatateua wanasoka kwa kutumia haki.

“Litakuwa jambo la busara kama kutakuwako kamati maalum ya makocha ambao watakuwa sehemu zote za nchi kuhakikisha ni wachezaji bora pekee ndio wanachaguliwa timuni,” akasema Dandize.