http://www.swahilihub.com/image/view/-/4802488/medRes/2138249/-/yuysdz/-/mo.jpg

 

Dewji alivyotikisa ndani na nje ya nchi

Mfanyabiashara maarufu na mwekezaji wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji  

Na Waandishi Wetu

Imepakiwa - Friday, October 12  2018 at  10:02

Kwa Muhtasari

Wengi wamekuwa wakijiuliza maswali mengi kuhusu chanzo cha tukio hilo ambacho bado hakijafahamika


 

Dar/mikoani. Tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji si tu limezua hofu ya usalama wa raia, ila limetikisa ndani na nje ya nchi.

Mfanyabiashara huyo mwenye utajiri unaokadiriwa kuwa Sh3.5 trilioni alitekwa jana saa 11 asubuhi na watu wasiofahamika katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo la mfanyabiashara huyo anayefahamika zaidi kwa jina la MO limezua hofu maeneo mbalimbali nchini na watu wamekuwa wakijiuliza maswali mengi kuhusu chanzo cha tukio hilo, ambacho bado hakijafahamika.

Habari za kutekwa kwa Dewji (43), zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii jana saa moja asubuhi, kabla ya kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa saa mbili asubuhi.

Akizungumza na waandishi wa habari hotelini hapo, kamanda huyo alisema Dewji ambaye ni mwekezaji wa klabu ya Simba alifika hotelini hapo kwa lengo la kufanya mazoezi kwenye gym iliyopo hapo na kupatwa na janga hilo.

Mambosasa ambaye aliliambia Mwananchi kuwa wanawashikilia watu 12 kutokana na tukio hilo alisema waliomteka mfanyabiashara huyo ni Wazungu wawili.

“Asubuhi ya leo (jana), Wazungu wawili walikuwa na gari aina ya (Toyota) Surf. Kulikuwa na magari mawili, moja lilikuwa ndani (ya uzio) na jingine nje. Gari la ndani liliwasha taa ghafla na lile lililokuwa nje likaingia na kwenda kupaki karibu na gari la Mo Dewji lililokuwa limepaki,” alisema Mambosasa.

“Wazungu wawili wakatoka na kumbana MO Dewji baada ya kutoka ndani ya gari lake na kisha kumpakia katika gari lao aina ya Surf kisha wakaondoka naye kusikojulikana,” alisema Mambosasa.

Dereva wa Uber asimulia alivyotekwa

Maelezo hayo yanatofautiana na ya dereva mmoja anayeendesha magari ya kukodisha ya mtandao wa Uber, ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.

Dereva huyo aliyekuwa anakwenda kumshusha abiria katika hoteli hiyo saa 11 asubuhi alisema, “Tulikuwa tunakaribia eneo hilo, mara mbele yetu tukaona watu wanne wameshuka kwenye gari dogo wakiwa wamejifunika usoni, wakapiga risasi moja juu, wale askari wa hoteli kila mmoja akakimbia.

“Waliingia ndani ya hoteli na kutoka na mtu, ambaye nilimjua kuwa ni Mo,” alisimulia dereva huyo ambaye alidai muda mwingi alikuwa amejiinamia kwenye gari akihofia maisha yake.

Alisema baada ya watu hao kumchukua mfanyabiashara huyo, waliondoka na gari kwa kasi kuelekea maeneo ya Masaki.

Hali ilivyokuwa nyumbani

Nyumbani kwa Dewji maeneo ya Oysterbay, ulinzi uliimarishwa huku ndugu, jamaa na marafiki wakifika na kuondoka katika nyumba ya bilionea huyo.

Sauti za kulia zilisikika kutoka ndani na kadri muda ulivyokuwa ukisogea sehemu ya maegesho ya magari ilikuwa ikijaa kutokana na wingi wa waliofika nyumbani hapo. Baadhi ya ndugu hao waligoma kurekodiwa wakisema ndani kwa Mo hakuna taarifa sahihi za alipo ndugu yao.

Baba yake azungumza

Gulam Dewji Hussein, baba wa Mo alipozungumza na Mwananchi kuhusiana na tukio la kutekwa kwa mtoto wake, alisema hawezi kulitolea maelezo tukio hilo kwa sasa.

“Sina cha kuzungumza, naomba muwatafute polisi wao wanaweza kuwa na maelezo zaidi,” alisema Gulam.

Wanasiasa washtushwa

Wanasiasa mbalimbali nchini walitoa maoni wakionyesha kusikitishwa na tukio hilo.

Zitto Kabwe, January Makamba, Hussein Bashe na Nape Nnauye ambao ni wabunge walitumia mitandao yao ya Twitter kuzungumzia tukio hilo la kutekwa kwa Mo Dewji ambaye amekuwa akitajwa na Jarida la Forbes kuwa miongoni mwa mabilionea vijana Afrika.

Makamba, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ameandika, “Nimezungumza na baba yake Mohammed Dewji. Habari za kutekwa kwa rafiki yetu Mo ni za kweli. Nimesikitishwa sana. Naamini polisi watatoa taarifa kamili. Mohammed ana familia na watoto wadogo.”

Mbunge huyo wa Bumbuli amemalizia ujumbe wake kwa kusema, “Tumuombee yeye na familia yake. Tusaidie kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake.”

Godbless Lema, ambaye ni waziri kivuli wa Mambo ya Ndani aliandika katika Twitter, “Kama waziri kivuli wa Mambo ya Ndani, ninafuatilia kwa karibu suala la kutekwa mfanyabiashara Mo Dewji.”

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe aliandika, “Nimeshtushwa na kuumizwa na habari za kutekwa kwa ndugu yetu Dewji leo alfajiri akiwa anakwenda mazoezini hapa Dar es Salaam.”

“Kila mmoja wetu mwenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kumwokoa asaidiane na vyombo vyetu vya dola. Mola atamsaidia MO na familia yake katika mtihani huu.”

Bashe, Mbunge wa Nzega Mjini aliandika, “Inasikitisha na kushtua tukio hili la Dewji kutekwa. Aina hii ya uhalifu inaota mizizi, ana familia, ana watoto, ana ndugu tuendelee kumuombea kwa Allah na kila mmoja wetu kutoa taarifa yoyote atakayopata ambayo itasaidia kumpata akiwa salama Allah amlinde.”

Bashe aliweka picha ya Mo Dewji kisha akaandika ‘Oooh GOD’ na alama inayooshea kutoa machozi.

Utekaji kimataifa

Matukio ya utekaji kwa watu maarufu yametokea pia katika baadhi ya nchi duniani

Mwaka 2015, aliyekuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Francois Bizimana alitekwa nyara mjini Bujumbura na watu wanaodaiwa kuwa na uhusiano na Serikali.

Bizimana alikuwa miongoni mwa viongozi wa upinzani nchini Burundi waliokuwa wakipinga uongozi wa Rais Pierre Nkurunziza.

Nako Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 2016, Padri wa Kanisa katoliki, Sebastian Yebo alitekwa na watu wasiojulikana muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza misa katika Parokia ya Mtakatifu Robati huko Mashariki mwa mji wa Kinshasa.

Padri mwingine, Havugimana Ngango Celestin alitekwa nyara 2018 na waasi wasiojulikana katika maeneo ya Kihondo wilayani Ruchuru, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Alitekwa akiwa kwenye gari lake katika barabara inayoelekea Kihondo eneo la Nyarukwangara siku ya sherehe za Pasaka.

Nchini Mexico, 2009 mtaalamu wa kuzuia utekaji nyara, Felix Batista naye alitekwa na watu waliokuwa wamevaa vinyago vyeusi.

Batista alikuwapo nchini humo kuendesha semina kama mfanyakazi wa kukodiwa wa kampuni ya usalama yenye makao yake huko Texas ASI Global LLC.

Mwaka huu alitekwa Rais wa Shirika la Polisi wa Kimataifa (Interpol) Meng Hongwei akiwa nchini China.

Hongwei ambaye ni raia wa China alitoweka ghafla alipokuwa kwenye ziara ya kikazi nchini humo, tangu Septemba 29 kwa mujibu wa Serikali ya Ufaransa kulipo ofisi za makao makuu ya Interpol.

Chombo kimoja cha habari cha nchini humo kijulikanacho kwa jina la The South China Morning, kilisema Hongwei (64) anashikiliwa nchini humo kwa ajili ya uchunguzi.

Chanzo hicho cha habari kilisema rais huyo alipofika China, alikamatwa na kupelekwa kwenye mamlaka ya nidhamu kwa ajili ya kuhojiwa.