Diamond anastahili kupongezwa, kupigiwa mfano

Nassib Abdul ‘Diamond’ 

Imepakiwa - Monday, October 8  2018 at  10:05

Kwa Muhtasari

Amekuwa nembo ya nchi yetu kwani amekuwa mbeba bendera wa kujivunia katika mataifa mbalimbali

 

Mwanamuziki Nassib Abdul, maarufu Diamond sio miongoni mwa wasanii wakongwe nchini. Amekuwa kwenye ramani ya sanaa kwa miaka tisa tu lakini mchango wake katika fani hiyo, ujenzi wa Taifa na kuipeperusha bendera yetu ni wa kupigiwa mfano.

Alianza kupata umaarufu baada ya kutoa wimbo Nenda Kamwambie ukifuatiwa na Mbagala zilizompa tuzo ya mwanamuziki chipukizi mwaka mmoja baadaye. Tangu hapo hakurudi nyuma kwani mbali ya kuendelea kushinda tuzo, pia amekuwa nembo ya nchi yetu kwani amekuwa mbeba bendera wa kujivunia katika mataifa mbalimbali ambako amekuwa akitumbuiza na kushinda tuzo.

Kwa mfano, katika ukanda wa Afrika Mashariki, ndiye msanii mwenye rekodi ya kushinda tuzo nyingi kubwa zikiwamo za Channel O, MTV Base, MTV Europe na Afrimma.

Mchango wake katika tasnia ni wenye tija, wala sio wa kuutafuta kwa tochi. Mafanikio yake binafsi, kwa wasanii wenzake na ajira anazotoa katika nyanja mbalimbali unaonekana wazi. Kwa mfano, kupitia kampuni yake ya WCB ameajiri wanamuziki wenzake, watangazaji na wapigapicha. Wanamuziki wanaofanya vizuri chini ya usimamizi wake ni pamoja na Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Queen Darlin na Lavalava.

Mbali ya jitihada hizo, mwanamuziki huyo alifanya jambo kubwa na la kupigiwa mfano katika jamii. Katika mwendelezo wa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa alitoa msaada mkubwa kwa watu jamii aliyokulia, Tandale jijini Dar es Salaam.

Alitoa bima za afya za mwaka mmoja kwa watu 1,000, mikopo ya kati ya Sh100,000 mpaka 200,000 kwa wanawake 200 na bodaboda 20 kwa vijana.

Miaka 20 iliyopita, ilizoeleka misaada kama hii kutolewa na mashirika, kampuni au wafadhili kutoka nje. Enzi hizo, kwa kiwango kikubwa wanamuziki walionekana watu wasio na mchango wowote katika jamii isipokuwa waharibifu wa maadili.

Ilipotokea msanii akafanya hivyo alikuwa kutoka nje ambaye pia lengo lake la kutoa msaada lilikuwa kujitangaza au kutangaza alichokuja kukifanya kama ilivyokuwa kwa rapa maarufu wa Marekani, Jay Z na mkewe Beyonce ambao walifika Tanzania mwaka 2011 na kutoa msaada wa kisima cha maji huko Mwananyamala, Dar es Salaam.

Kutoa uhakika wa matibabu kwa watu 1,000 miongoni mwao 300 wakiwa ni watoto, ni jambo kubwa achilia mbali mikopo na bodaboda zinazokwenda kuajiri vijana wengine wa Kitanzania.

Wasanii wote tuliowataja hapo juu chini ya Diamond wameajiri wacheza shoo, wapiga picha, maDj na wabunifu wa mavazi. Maana yake hapa ni kwamba ametengeneza wigo mwingine wa ajira kwa Watanzania wengine wengi.

Mbali na kutoa ajira kupitia muziki, amefanya hivyo pia kwenye biashara zake nyingine kama televisheni ya Wasafi, Diamond Karanga na manukato aina ya Chibu.

Wahenga walisema, kutoa ni moyo, usambe ni utajiri. Tunaamini kwamba Diamond amefanya yote hayo kwa kiu yake ya kutaka kuona kila mmoja anafaidi matunda ya mafanikio yake.

Kwetu huu ni mfano wa kuigwa si kwa wasanii tu, bali kwa Watanzania wote ambao wamefanikiwa kimaisha. Wakumbuke walikotoka na waone kwamba wana dhima ya kusaidia jamii waliyoiacha.

Tunaamini kwamba kwa kufanya hivyo, tutaipunguzia Serikali mzigo mzito wa kuwapelekea wananchi maendeleo na kuiacha ibebe jukumu kubwa la kuwafikishia miundombinu mikubwa.

Wito wetu kwa Serikali ni kuendelea kujenga mazingira ambayo tayawezesha kupatikana kina Diamond wengi zaidi. Hayo ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufanya shughuli za sanaa ikiwamo kuimarisha vyuo vya sanaa, kujenga kumbi kubwa zenye sura ya kitaifa na uwekezaji katika kuibua na kukuza vipaji.