EDWIN ODERO: Mui huwa mwema

Edwin Owino Odero

Msanii Edwin Owino Odero. PICHA/ BENSON MATHEKA 

Na BENSON MATHEKA

Imepakiwa - Monday, March 20   2017 at  21:15

Kwa Mukhtasari

UKIONA vyaelea, jua vimeundwa. Ukimpata Edwin Owino Odero akinogea kwenye sanaa yake ya uimbaji, utafurahi sana na hautafahamu kuwa nyuma ya sauti hiyo mna pazia iliyofunika maisha yake ya hapo awali ambayo akikusimulia, utatokwa  machozi, hadi roho igeuke ya Firauni.

 

Bwana huyu alikuwa mlanguzi sugu wa dawa za kulevya tangu akiwa darasa la sita na kwa sasa ni muinjilisti anayeheshimika

"Babangu alikuwa mvutaji wa sigara. Licha ya kuwa daktari huko Kitui na kufahamu fika madhara ya sigara, bado alikuwa akivuta sana.

Alikuwa akinituma dukani kumnunulia sigara mara kwa mara, na mimi kwa kufuata nyayo zake, zile za mtoto wa nyoka kuwa nyoka, nilianza kuvuta kisiri nikijificha chooni," aeleza  Owino mwenye umri wa miaka 38.

“Baba alipata uhamisho kutoka huko Kitui hadi Homabay ambako nilipatana na watoto wa shangazi na wajomba wangu ambao walikuwa walanguzi wa bangi.

Nayo bendera hufuata upepo. Nilijiunga nao nami pia nikawa natumia bangi pamoja na sigara nikiwa miaka kumi na mitano hivi. Nilianza kufanya vibarua vya hapa na pale sanasana kwenye mijengo ili nipate pesa za kukimu maisha haya," asimulia.

Alifika Nairobi 1998 na kutua mtaa wa mabanda wa Dandora kujaribu bahati yake maishani. Ni kwenye harakati za kutumia bangi na kutafuta maeneo yaliyokuwa yakiuzwa ambako alikutana na walanguzi sugu kumliko.

“Hawa sasa walikuwa majambazi wa bunduki ambao walikuwa wabaya sana hadi kuwa 'wanted' na polisi nyakati hizo. Jamaa hawa walimfunza pia kutumia cocaine. Lakini sikuwahi shirikiana nao kwenye shughuli za wizi,” alieleza.

Kunusurika

Mikono mirefu ya serikali iliwamaliza wezi wale kwa kupigwa risasi mtaani Eastleigh mjini Nairobi. Alibahatika kunusurika kwani hakuwa nao lakini maisha yake yalibadilika.

Hakuwa na marafiki wowote sasa. Wote waliomjua walimtenga kwa sababu ya uhusiano wake na hao waliokuwa marafiki wake. Wakati huo alikuwa akiuza 'PlayStation' na magazeti kwenye soko la Mtindwa huko BuruBuru. 

Kuna wakati alikuwa mgonjwa na madaktari wakamwambia kuwa suluhu ilikuwa tu ni kuacha kuvuta sigara. Japo alijaribu, kiu  ya fegi ilimvuta tena na akajipata akitumia dawa za kulevya tena, pasi na kujali afya yake.

Macho ya chuki kutoka kwa waliomjua na kule kukosa marafiki kulimwathiri hadi akaamua kujiua. Alitenga siku ya Jumapili Aprili 23 2000 kama siku yake ya mwisho duniani.

Anasema alinunua sigara mbili na tembe ishirini za 'piriton' ili asihisi uchungu wa kufa. Kwanza alivuta sigara zile kisha akaweka kanda za nyimbo za 'reggae' alizozienzi, kwa sauti kubwa kisha akalala kabla ya  kumeza tembe hizo.

Alipelekwa kanisani

"Kabla ya kumeza tembe alfajiri  niliamshwa na jirani mmoja ambaye alikuwa bado hajanitenga walivyokuwa wamefanya watu wengine.

Jirani huyu aliingia chumbani kwa sababu sikuwa nimefunga mlango na akanisihi nimpeleke kwa mzee wa  kanisa aliloshiriki.

Nami nilizima redio na kuandama  naye ili nikirudi, nimeze tembe hizo. Tulipofika huko, tulipata washirika kadhaa wakiabudu akiwemo mke wa mchungaji wa kanisa hilo.

Lazima ilikuwa Roho wa Mungu aliyenielekeza mahala pale kwa sababu, mara aliponiona mke wa mchungaji, aliniuliza.

“Kijana, mbona wataka kujiua na Mungu anakupenda? Nilinyamaza kwa kimako. Sikuwa nimemwambia mtu yeyote. Hata jirani huyo hangeweza kuziona dawa zile kutoka mvunguni mwa kitanda.

Kila mtu aliniangalia nami nikatokwa na machozi. Papo hapo niliombewa na nikamwamini Mungu kama mchungaji wa maisha yangu.

Baadaye niliporudi nyumbani, nilizitupa tembe kwenye choo na nikavunja kanda za muziki wa densi. Tangu siku hiyo sijawahi kutumia dawa za kulevya," alisema Owino.

Anasema tangu siku hiyo maisha yake yalibadilika..Akawa muimbaji mtajika wa nyimbo za injili   barani Afrika. Amezuru  Zambia, Zimbabwe, Uganda, Tanzania na Afrika Kusini. Akiwa nchini Zambia,  kipawa chake kiliwavutia waliomwalika na wakamfadhili kusomea muziki katika  chuo kikuu cha Zambia.

Kuwakomboa vijana

Bw Owino amejitwika jukumu la kuwaondoa vijana kutoka jinamizi la dawa za kulevya kupitia ushauri nasaha. Amekuwa  akitembelea vyuo vikuu na shule za upili kuwashauri wanafunzi. Anakiri kuwa haikuwa rahisi kuamua kuacha kutumia,mihadharati.

Hata hivyo ushauri wake kwa wote waliotekwa  na midharati ni :  “Kwanza badilisha marafiki. Tafuta wapya ambao watakubadilisha.

Tena tafuta kazi yoyote ile ya kibiashara, hata ikiwa ni vibarua, bora halali. Hii itakutoa mafikira ya kuwa na kiu ya kutumia dawa hizi.

Pia, jiunge na kanisa nzuri ambalo litakushika mkono hadi uache jinamizi hili. Usiwe na kiburi na mori unaotokana na dawa hizi ili ukubali mafunzo.

Kwanza mtu hukumbwa na shida kama kutetemeka na kuumwa na kichwa sana kutokana na kiu lakini ukiwa na maono ya kuacha, utafanikiwa."

Kwa sasa, Owino ametoa albamu yake ya nyimbo za injili iitwayo 'Great Overflow' iliyo na nyimbo saba.  Siku za usoni, anapania kufungua chuo cha kuwafunza watu kuimba nyimbo za kusifu na kushauri vijana.