http://www.swahilihub.com/image/view/-/4395758/medRes/1940600/-/15u1mh7z/-/editha.jpg

 

Edith Matiba ameishi na dukuduku moyoni

Edith Matiba

Edith Matiba ameishi na dukuduku moyoni. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Monday, April 16  2018 at  11:41

Kwa Muhtasari

Izingatiwe kuna wakati Rais Mstaafu Daniel arap Moi aliomba msamaha kwa yaliyomkuta mwanasiasa Kenneth Stanley Njindo Matiba.

 

KUNA shujaa mwingine katika maisha ya Kenneth Stanley Njindo Matiba ambaye kwa sasa taifa linamwomboleza kufuatia kifo chake cha Jumapili jioni akiwa na umri wa miaka 85 katika hospitali ya Karen, Nairobi.

Shujaa huyu ni Bi Edith Wanjiru ambaye ni mkewe marehemu.

Huyu ni mwanamke ambaye alisimama na Matiba katika harakati zake zote za kupambania demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa, wakati mwingine akihangaishwa na utawala wa Kanu na hata kuumizwa mwili kwa kuwa na ‘kosa’ moja tu—kuwa mkewe Matiba.

Edith ambaye husema kuwa alivumilia hayo yote ya mahangaiko hadi kumwona bwanake akigeuzwa kuwa kabeji na utawala huo kupitia kuwekwa ndani bila mashtaka yoyote, akateswa na kufukarishwa na kutwikwa mzigo wa afya mbovu, kwa nguvu za Maulana ambaye ndiye mwandani wake katika maombi.

Anasema kuwa alikubali kuwa mwokovu ndani ya imani ya Kikiristo bado akiwa mchanga na alipoolewa na Matiba mwaka wa 1961, hakutarajia kuwa maisha yake ya kifamilia ingegeuka kuwa ya mahangaiko  chini ya utawala uliokuwa mamlakani kuongoza watu walio na haki zao.

“Kwa masaibu hayo yote nilibakia kuomba Mungu atupe nguvu za kustahimili. Sio mara moja niliona mkono wa Mungu ukitunusuru mauti ya mapema kwa bwanangu. Mungu ni mwema kuwa alituhifadhi kuwa na kiongozi wetu wa familia hadi Jumapili ya Aprili 15 alipoaga dunia,” asema.

Anasema kuwa baraka kuu ya Mungu kwa familia yake ilikuwa kumwona Matiba akivumilia Stroke kwa wiki nzima akiwa takika gereza kuu la Kamiti mikononi mwa wabaya wake waliofahamu wazi kuwa ugonjwa huo ulikuwa na hatari ya kumuua Matiba.

“Kwa hayo yote, nilijua Mungu alikuwa nasi, kuwa alikuwa anamtumia Matiba kama Malaika wa kutekeleza afueni kwa Wakenya na yote aliyopitia na tukapitia pia kama familia yalikuwa yanafuatiliwa na Mungu aliyempa ujasiri wa kupambana na utawala hasi wa wakati huo,” asema.

Anasema kuwa alimjua Matiba akiwa katika kidato cha kwanza; Edith wakati huo akiwa katika shule ya msingi.

Matiba alikuwa Alliance High School naye Edith alipohitimu elimu ya msingi akaitwa katika shule ya upili African Girls (Alliance Girls leo) na wakawa majirani aghalabu kielimu.

Chuoni

Walikutana katika chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda na uhusiano wao ukaimarika na ukaishia kuwa ‘kitu’.

Hatimaye Matiba aliajiriwa kama mwalimu, naye Edith akijipatia ajira ya serikali katika Kaunti ya Bungoma kama afisa wa kijamii.

Anasema kuwa mwaka wa 1979 aliomba Mungu anuisuru Matiba dhidi ya kuamua kuingia kwa siasa lakini alipogundua kuwa alikuwa ameamua kuingia kwa mchezo huo ambao husemwa ni mchafu, “nilikubali tu na nikaomba kuwa sasa Mungu atupe ujasiri wa kuvumilia mipigo ya kisiasa.”

Anasema kuwa “Matiba na Moi walikuwa marafiki wa dhati wakati huo lakini anasema kuna wale wa uchawi wa uhusiano wa kirafiki ambao waliingia katikati ya urafiki huo na wakakoroga yao iliyoishia kugeuza Moi kuwa hasidi Mkuu wa Matiba.”

Anasema kuwa Matiba akijitoa kwa serikali ya Moi 1988 alikuwa ameahidiana na aliyekuwa Waziri wa Afya wakati huo, Mwai Kibaki wajitoe pamoja lakini Kibaki akabadilisha mawazo dakika za mwisho na akabakia ndani ya serikali Matiba akienda zake nje.

Edith anasema kuwa kwa wakati huo wote baada ya masaibu ya kukamatwa na kuwekwa kwa mateso gerezani, alikuwa akimwambia nyumbani kuwa “nikipata nafasi ya kukutana na Moi nitamuuliza ni wapi aliacha kunichukulia kama rafiki na akanigeuka kwa ukatili huu wote wa kimaisha na kiuchumi.”

Anakumbuka kuwa Juni 13, 1990, kuna uvamizi ulitekelezwa nyumbani kwao katika eneo la Limuru na ambapo baada ya Matiba kuwa hayuko nyumbani, yeye Edith ndiye alipigwa na genge hilo la wanaume 10 lililosema kuwa lilikuwa limeingia kumwangamiza Matiba.

Genge hilo lilisema kuwa lingepewa Sh10 milioni, lingewanusuru.

Alishambuliwa pamoja na wasichana wawili waliokuwa katika nyumba hiyo baada ya kukosa pesa hizo lakini kwa bahati njema, hawakupata Matiba ambaye tena habari ziliibuka kuwa alikuwa tayari amekamatwa na alikuwa amezuiliwa katika gereza kuu la Kamiti.

Anasema kuwa serikali ya Moi ilimwachilia Matiba akiwa katika hali mbaya kwa kuwa hangeweza kuongea wala kuandika.

“Alikuwa amerudi kuwa mtoto. Sina chuki na Moi kwa leo lakini swali langu ni moja tu: Mbona utawala wa Kanu ukafanya hayo?”

Anasema amekutana na Rais Mstaafu Daniel Moi mara mbili tu lakini hakuweza kumuuliza swali hilo.

“Nilikutana naye mara moja tukiwa abiria ndani ya ndege na wakati wa kumuomboleza Njenga Karume. Sikupata nafasi ya kumuuliza swali hilo lakini nikipata nafasi nitamuuliza,” asema.