http://www.swahilihub.com/image/view/-/4611716/medRes/2008334/-/q3gkuh/-/choo.jpg

 

Elimu Bure isiwe kisingizio cha kutoboresha miundombinu

 

Na Sada Amir

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  11:08

Kwa Muhtasari

  • Wafanyabiashara kujenga matundu 3,148 ya vyoo katika shule 80 nchini Tanzania
  • Mvulana mwenye umri wa miaka 10 amefariki Alhamisi Juni 14, 2018, baada ya kuanguka katika choo wazi katika shule ya msingi ya Mukoyani, kaunti ya Kakamega; wazazi waandamana huku polisi wakipeleka maiti katika mochari

 

MWANZA, Tanzania

WAFANYABIASHARA wa maduka ya vifaa vya ujenzi na wamiliki wa mashine za kufyatua matofali, wamelazimika kujichangisha vifaa na fedha ili kujenga matundu 3,148 ya vyoo katika shule za msingi 80 za jijini hapa.

Wakati jumla ya matundu ya vyoo yanayohitajika ni 4,170, yaliyopo ni 1,022 ambayo yanatumiwa na wanafunzi 107,000.

Katika harambee iliyoongozwa na mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha wafanyabiashara hao walichanga mifuko 183 ya saruji, matofali 1,200, kilo 70 za misumari, ndoo 29 za rangi za lita 20, malori saba ya mchanga na maboksi matano ya vigae na nondo tano.

Kaimu Ofisa Elimu Msingi Jiji la Mwanza, Omari Kwesi aliwaomba wafanyabishara na wamiliki wa mashine za kufyatua matofali zaidi ya 200 kutoka kata 18 za jiji, kuisaidi Serikali kukabiliana na changamoto za ubovu wa miundombinu katika shule za umma.

Akizungumza na wafanyabiashara hao, Tesha aliwaomba wakazi wa jiji hilo kujitolea ili kuboresha miundombinu ya kufundisha na kujifunza katika shule za umma.

“Baadhi ya watu wamepokea ndivyo sivyo Sera ya Elimu Bure wakidhani wazazi hawana jukumu la kuboresha elimu ya watoto wao; nashukuru Mwanza tumeanza kuelewa na leo tumechangia vifaa vya ujenzi kukabiliana na upungufu wa matundu ya vyoo katika shule zetu,” alisema Tesha.

Mmiliki wa duka la vifaa la ujenzi, Martin John alisema iwapo kila mzazi atachangia kiasi kidogo alichonacho kwa hiari, tatizo la miundombinu katika shule za umma litapatiwa ufumbuzi.