Elimu itolewe ndugu kupata fedha zilizopo kwenye simu za mikononi

Imepakiwa - Tuesday, April 30  2019 at  11:29

 

Hivi sasa simu ya mkononi zimekuwa njia rahisi zaidi ya utunzaji wa fedha na hutumika pia kwa ajili ya kufanya miamala mbalimbali. Zinatumika kulipa ada na tozo kama vile karo za shule, ankara za maji, umeme au ulipiaji wa vifurushi vya muda wa maongezi.

Kwa miaka zaidi ya 10, huduma hiyo imekuwa ikitolewa na kampuni zote zinazotoa huduma za simu za mkononi nchini. Ni jambo jema na moja ya matunda ya maendeleo ya teknolojia, kwani sasa siyo lazima anayehitaji kulipia huduma kwenda benki na kupanga foleni. Kila kitu sasa kinamalizika kwa kutumia simu.

Jana katika toleo la gazeti hili ilielezwa jinsi fedha nyingi zinavyoweza kupotea baada ya wamiliki wa simu za mkononi kufariki dunia na hasa wanaofariki dunia ghafla huku ndugu wakiwa hawajui wafanye nini kuzipata fedha hizo.

Mara ndugu anapofariki dunia wafuatiliaji wengi wa mirathi hususan katika kipengele cha fedha wamekuwa wakikimbilia kujua kinachoachwa kwenye akaunti za benki, madeni ya marehemu yatokanayo na kukopesha fedha na kadhalika, lakini hawajishughulishi na zile zilizopo kwenye mitandao ya simu.

Hili linatokea kwa kuwa watu wengi hawana elimu ya kutosha juu ya nini wafanye ili kupata fedha zilizopo kwenye akaunti za simu za ndugu zao baada ya mmiliki wa simu kufariki dunia, huku ndugu wakiwa hawafahamu namba za siri za akaunti.

Kutokana na hali hiyo inahitaji kuwepo kwa haja ya kutoa elimu kwa watumiaji wa simu za mkononi na jamii kwa jumla, ili watu wajue haki yao juu ya fedha hizo na nini kifanyike kupitia utaratibu wa kisheria ili wapate fedha za ndugu, jamaa au wapendwa wao wanapofariki dunia.

Serikali kupitia taasisi zinazosimamia huduma za simu za mkononi kama Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kushirikiana na taasisi za kifedha na mitandao ya simu, wanao wajibu wa kuwafanya watumiaji wa huduma zao kufahamu haki hizo.

Elimu endelevu itolewe kwa wote ili kila mtu ajue anapaswa kuchukua hatua gani kuzipata fedha za ndugu au mwanafamilia aliyefariki dunia akiwa na fedha katika simu yake ya mkononi. Kama hilo likifanyika, litasaidia na kuirahisishia familia ya marehemu na wategemezi aliowaacha kupata haki yao.

Mbali na kutoa elimu, ni muhimu pia kutazama njia zingine zitakazowezesha ndugu wa mteja wa huduma za fedha katika simu anavyoweza kupata haki ya ndugu yao.

Kwa mfano, kampuni za simu zinaweza kutangaza katika vyombo vya habari orodha ya akaunti na majina ya wateja wao ambao wamepitisha muda mrefu bila kuzitumia. Kufanya hivyo kutawapa fursa wanaohusika kufuatilia kwa wakati.

Mbali na elimu, sheria na taratibu zirahisishwe ili kuwawezesha wananchi hususan waliopo katika maeneo yaliyo nje ya miji mikubwa kumudu kufuata taratibu hizo na kupata haki za ndugu zao.

Ushuhuda uliotolewa na ndugu mmoja wa marehemu katika habari iliyochapishwa ndani ya gazeti hili, kuwa kama siyo kukumbushwa na hakimu, basi fedha za marehemu kaka yake zinazofikia Sh4.48 milioni zilizokuwa katika mitandao ya simu zingepotea, ni ushahidi kuwa wapo wengi wanaoacha kufuatilia na kupoteza fedha nyingi. Ni vyema utaratibu rahisi uwekwe ili kurahisisha upatikanaji wa fedha ambazo tunadhani zinastahili kuendelea kusaidia familia ya marehemu.