http://www.swahilihub.com/image/view/-/5015304/medRes/2274131/-/ubxvx0z/-/kinga+pic.jpg

 

Elimu kwa mama kinga ya kwanza saratani ya kizazi

 

Na Mwanishi wetu

Imepakiwa - Friday, March 8  2019 at  13:02

 

 Saratani ya shingo ya uzazi ni aina ya ugonjwa unaoongoza kuua wanawake wengi kuliko aina nyingine ya saratani.

Awali, wanawake walikuwa wanapoteza maisha baada ya kupatikana na ugonjwa huu, tofauti na ilivyo sasa. Idadi ya wanaopoteza maisha imepungua kutokana na kampeni zilizofanyika ili kuinua uelewa wa magonjwa ya saratani na hasa ya kizazi.

Naipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuhakikisha wananchi wanahabarishwa na kupata uelewa kuhusu ugonjwa huu.

Wanawake hawana sababu ya kuendelea kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huu, lakini kwa bahati mbaya bado wanaendelea kufa.

Saratani ya shingo ya kizazi inaendelea kutishia maisha ya wanawake nchini kutokana na ripoti za karibuni zilizotolewa na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC), kueleza kuwa maelfu ya wanawake wa Kitanzania wapo hatarini kupatikana na saratani ya kizazi katika miaka michache ijayo.

Sababu kubwa inaelezwa ni wanawake kukosa taarifa na uelewa kuhusu saratani ya kizazi hasa waishio maeneo ambayo upatikanaji wa habari ni duni.

Saratani ya shingo ya uzazi ni aina ya ugonjwa ambao huanzia na kukua kwenye mlango wa uzazi au maarufu kama cervix kwa kitaalamu. Hii ni sehemu nyembamba yenye uwazi inayoanzia kwenye uke hadi kwenye mfuko wa uzazi.

Saratani hii ikigundulika mapema inakuwa na uwezekano mkubwa wa kupona.

Imethibitika kuwa saratani ya shingo ya kizazi inazuilika kirahisi kuliko saratani nyingine zote.

Njia pekee ya kuzuia na kujikinga na saratani hii ni kupata chanjo ya HPV; HPV (Human Pappiloma Viruses).

Kutokana na ukweli kuwa, saratani ya shingo ya uzazi ni moja ya saratani zinazowashambulia wanawake pekee, hivyo ni dhahiri kuwa kihatarishi cha kwanza ni kuwa mwanamke. Saratani ya shingo ya kizazi mara nyingi hutokea katika umri wa kati.

Mwandishi wa makala haya ni daktari kutoka TMJ SUPER SPECIALIZED POLYCLINIC.